Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuongea siku ya leo. Kwanza nikupongeze wewe binafsi kwa kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia nimpongeze sana kaka yangu Mheshimiwa Zungu kwa kuchaguliwa na Chama chetu; Chama cha Mapinduzi, kuwa mwakilishi wa Chama cha Mapinduzi kwa nafasi ya Unaibu Spika. Naamini kabisa, kama kawaida, hiyo imekwisha hiyo, yeye ndiye Mungu amemeoneshea njia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nianze moja kwa moja na kuchangia katika Wizara yangu ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Mimi niseme tu namshukuru sana Mheshimiwa wetu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu kipenzi sana Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kutukubalia sisi wanakamati kwa kurasimisha ardhi kwa kila Mtanzania.
Mheshimiwa Spika, kwa wale wanaouliza Mheshimiwa Rais, Mama Samia kafanya nini; wanapaswa kujua kwamba kati ya shughuli au kazi nzuri au upendo mkubwa aliotuonesha Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ni huu wa kumtaka kila Mtanzania amiliki ardhi yake.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nampongeza sana mama, Mwenyezi Mungu aendelee kukubariki, unaupiga mwingi. Wale waliokuwa wanafikiri huwezi, unaweza, unatosha na chenji inabaki. Naamini 2025 kwa mapenzi ya Mungu mama tutakupa kura nyingi sana. Sisi kama Wana- Mara, nami kama mwakilishi wa wanawake kutoka Mara tutampa Mheshimiwa Rais kura za kishindo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa niongelee suala la ardhi. Kwa kweli Mabaraza ya Ardhi yamekuwa yakileta kero nyingi sana tena kero zenyewe ni chefuchefu na hasa pale Mabaraza yanapoendesha kesi kwa muda mrefu sana. Mabaraza haya yamekuwa yanaendesha kesi kwa muda wa miaka 10, 20 mpaka 30. Hii wakati mwingine hupelekea mtu mwenye kesi hiyo anafikwa na umauti hajafaidi ardhi yake; mtu mwingine anakuwa ameshazeeka na mtu mwingine anakuwa ameshazaa watoto na watoto wameshakuwa na wajukuu. Ni suala ambalo siyo zuri sana na ambalo linaleta shida kila siku kwenye ardhi na migogoro isiyokwisha.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, wao kama viongozi, kama waosimamia wasimamizi wa kesi za ardhi, tunawaomba wabadilishe taratibu zao. Hii yote ni kwa ajili ya kutengeneza rushwa ambazo hazijaisha katika ardhi yetu ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Waziri wetu, Mheshimiwa Mabula, lakini naomba afanye kazi kubwa sana katika mabaraza haya. Ikiwezekana awabadilishe badilishe, wasikae muda mrefu na ikiwezekana pia afuatilie kujua kwamba ni nani anayesababisha shida hizi zinaendelea? Kwa sababu shida hizi zinazoendelea ni baina ya masikini na matajiri. Ikionekana katika ardhi hiyo masikini au mtu wa hali chini alikuwa anaimiliki ardhi hiyo kama mmiliki namba moja, halafu akatokea tajiri, naye anakuwa na Hati, tena unaiona hati yenyewe inafanana kama ya wiki mbili, lakini inakuwa eti ni Hati ya miaka 20. Ni kitendo ambacho siyo kizuri sana, ni uonevu kwa Watanzania. Tum-support mama yetu Mheshimiwa Samia kwa upande wa umilikishaji kwa ili kila Mtanzania aweze kumiliki ardhi na hasa Watanzania wanawake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ushauri wangu kwa Serikali; naiomba Serikali ifanye auditing ya mara kwa mara kwa ajili ya kuangalia kesi hizi: Je, zimetumia muda gani? Zinaendaje? Kusudi kesi hizo ziwe zinatumia muda mfupi kwisha, siyo kesi zinakaa muda mrefu sana.
Mheshimiwa Spika, suala la ardhi limekuwa ni tatizo kubwa sana na hasa hapa Dodoma. Nasema Dodoma kwa sababu naamini kabisa hata sisi wenyewe Wabunge huku ndani, wengi sana tuna matatizo hayo. Sisi tunataka kulipia malipo ya Serikali ili tupate Hati, tulipie kodi za Serikali lakini wao wanakaa nazo maofisini muda mrefu bila ya kuzifanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili sulla linatakiwa liondolewe kwenye maofisi, wamekuwa wanakula rushwa kupitiliza. Kama wamepewa kazi mtoto wa baba, mtoto wa shangazi kwamba wote ni wakazi wa hapa hapa ambao hawatoki ndani ya ofisi hizo, basi wapishe, kuna watu wengi sana wanatembea na vyeti wamesoma Vyuo Vikuu, wengine ni Maprofesa wanatembea na vyeti vyao mkononi, wapewe kazi hizo wafanye kama wao kazi za ardhi zimewashinda.
Mheshimiwa Spika, pia mimi niseme tu kuhusu viongozi wangu wa Dodoma. Imefikia hatua viongozi kutoka ardhi muone aibu na haya. Kuna vitu mnavifanya vinapitiliza. Mimi kama Mbunge nina mfano hai. Nilinunua kiwanja miaka 10 iliyopita, lakini hawakuwa wanajua kama ni kiwanja cha Mbunge, bahati mbaya kipindi hicho mimi sikuwa Mbunge. Nikiwa Mbunge sasa nimekuja kufuatilia, eti kiwanja changu kimechukuliwa, kimepelekwa Polisi, kwamba Polisi wanafanya uchunguzi. Hivi sasa uchunguzi unachukua miaka, badala ya waniambie kwamba hiki kiwanja kama ni cha mtu, basi mimi kama Mbunge nitakubali mtu masikini akapewe kile kiwanja. Hata hivyo, ninavyo vielelezo vyote na document zangu ambazo ni original, ni kwa sababu tu kuna mtu alikuwa anataka kumilikishwa ambaye ameshawapa rushwa, sasa yamewakwama wameshindwa la kufanya.
Mheshimiwa Spika, kama natendewa mimi Mbunge, hivi raia wa kawaida wanatendewa nini? Wanafanyiwa vitu vingapi? Sisi kama Wanakamati kutoka Kamati ya Ardhi tumeshauri mara nyingi, basi wale Maafisa au viongozi walioko hapa maofisini, tunaamini kabisa wala rushwa wanawajua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hili suala linatokea kote ikiwepo hata kwangu Mkoa wa Mara. Kuna wamama masikini wanalia sana, wanaonewa. Kama yeye ni mmiliki namba moja, huyu mmiliki namba mbili anayekuja na Hati ambayo inaonekana ni kama Hati ya jana, lakini huyu mama ana Hati yake ya miaka mitano hadi sita ambayo yeye ndiye mmiliki namba moja. Basi yeye awe na haki kwenye haya Mabaraza ya Ardhi ili kusudi yeye apewe haki yake na huyu namba mbili wakamtafutie hivyo viwanja vya matajiri amilikishwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ardhi imenuka rushwa, imejaa rushwa. Naomba Mheshimiwa Waziri iwe ni sehemu yake ya kwanza sasa kuchanganua au kuwatoatoa wale watu ambao ni wala rushwa na wanafahamika.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
SPIKA: Ahsante sana.
MHE. AGNES M. MARWA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)