Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nanyumbu
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. DUA W. NKURUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kabla sijaanza kuchangia katika Wizara hii nitumie nafasi hii kuishukuru sana Wizara ya Afya kwa sababu Wilaya yetu ya Nanyumbu, tangu ianzishwe tulikuwa tunafuata huduma za Hospitali ya Wilaya kwenye Wilaya ya jirani ya Masasi kwa kipindi chote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata nilipochaguliwa, wananchi wa Wilaya ya Nanyumbu, miongoni mwa vipaumbele ambavyo walivitaka nivifuatilie ni kukisajili Kituo cha Afya cha Mangaka kuwa Hospitali ya Wilaya. Naishukuru sana Wizara kwa sababu baada ya kilio hiki cha siku nyingi tumewasiliana nao, tumewaeleza, mimi mwenyewe nimefanya mazungumzo nao na hatimaye sasa kwenye bajeti hii, Kituo cha Afya cha Mangaka kimepata usajili na kuwa Hospitali ya Wilaya ya Nanyumbu.(Makofi)
Mheshimiwa Waziri, naishukuru sana Wizara yako kwa niaba ya watu wa Nanyumbu, sisi ambao tulikuwa tunataabika, tunapata shida, mama zetu wanajifungua njiani kuelekea Masasi, watu wanafariki njiani kuelekea Masasi na Ndanda, kwa kweli kwa kitendo hiki tunaishukuru sana Serikali. Naomba kasi hii iendelee ili Watanzania wote katika maeneo yao walipo ambapo wanakosa hizi huduma, wapate Hospitali za Wilaya kama sisi watu wa Nanyumbu ambapo tumeshapata bahati mwaka huu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukurani hizo naomba nianze kuchangia. Wizara ya Afya kama walivyosema wengine, ndiyo uhai wa Watanzania. Wizara yetu inashughulika na afya za watu. Kwa hiyo, tunategemea hata watumishi kwa sababu wanagusa uhai wa watu ni lazima wawe waadilifu, lakini pia tuwajengee moyo wa kufanya kazi ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi tunaoutegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza ambayo naiona katika Wizara hii, ingawa ni vigumu sana kuijadili Wizara hii peke yake na ukaacha kuigusa TAMISEMI; changamoto ya kwanza ni kukosekana kwa zahanati za kutosha katika maeneo yetu. Kwa mfano Wilaya ya Nanyumbu ina vijiji 93, lakini tuna zahanati 17. Kwa hiyo, kuna vijiji vingi vinakosa zahanati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa tuna vituo vya afya vitatu, kimoja sasa kimeshapata kuwa Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, tuna vituo vya afya viwili, tuna Kata 19. Kwa hiyo, utakuta kuna uhaba mkubwa wa majengo ya zahanati. Naiomba Wizara, ingawa jukumu hili wameliacha kwa TAMISEMI, lakini tuangalie baadaye uwezekano wa Wizara hizi mbili kukabidhiana majukumu haya vizuri. Tuwe na program ya kiuhakika ambayo itaihusisha Serikali kuu namna ya kujenga Zahanati kule vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri kamwe haziwezi kujenga Zahanati hizi ambazo tunazisema leo, haziwezi, kwa sababu mapato yao ni madogo lakini pia hata zile pesa ambazo zinatoka Serikalini kama ceiling zinakuwa pia ni ndogo. Kwa hiyo, lengo letu la kujenga zahanati kila kijiji, kama hatutajipanga vizuri, Bunge hili litamaliza muda wake tukiwa na zahanati chache sana katika vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali tuandae mpango maalum utakaoanzia Wizarani wa kupeleka pesa Halmashauri na Halmashauri pia zitenge pesa za mapato ya ndani kuongeza idadi ya zahanati kule vijijini. Mheshimiwa Waziri Ummy atakuwa ametenda kitu kikubwa sana na akinamama na wananchi wote wa Tanzania hawatamsahau. Kwa hiyo, hiyo itakuwa ni historia kubwa ambayo atakuwa ameifanya kwa kuongeza idadi kubwa ya zahanati katika vijiji vyetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto nyingine ambayo naiona hasa katika Wilaya ya Nanyumbu ni uhaba wa Watumishi wa Afya. Wilaya ya Nanyumbu ina uhaba wa watumishi wa afya zaidi ya asilimia 55. Kwa hiyo, utakuta sasa watumishi hawatoshi wanafanya kazi kwa nguvu kuliko uwezo wao. Hii inapelekea waichukie kazi yao; na mtu anayefanya kazi akiwa na chuki, hata lugha yake inakuwa mbovu. Tunajikuta tunawalaumu kwa sababu hawazungumzi lugha nzuri kwa wagonjwa, lakini ni kwa sababu amechoka. Mtumishi utamkuta kwenye zamu yuko mmoja, atafanya kazi mpaka jioni, usiku, mchana, muda wowote. Kwa hiyo, kwa sababu ya uchovu kuna kipindi kibinadamu anazungumza maneno ambayo mgonjwa hakutarajia ayasikie. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili kukomesha hii hali, ni lazima tuongeze idadi ya watumishi hasa Nanyumbu ambako tuna upungufu wa watumishi zaidi ya asilimia 55. Kwa hiyo, hii ni changamoto kubwa katika Wizara hii ya Afya kwa sababu tuna uhaba mkubwa wa watumishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika Wilaya yangu kuna baadhi ya vijiji, kwa mfano Kijiji cha Marumba, Kijiji cha Maratani, Kijiji cha Mkumbaru na Kijiji cha Lumesule. Vijiji hivi zahanati zake Mganga anayetoa huduma ni Nurse; yeye ndiye anaandika dawa, yeye ndiye anayetoa dawa tunategemea nini katika hali hii? Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-windup atambue kwamba tuna changamoto hiyo na naomba atakapotaka kuwagawa watumishi katika Halmashauri atambue kwamba Nanyumbu ina upungufu wa watumishi wa zaidi ya asilimia 55.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie kuhusu CHF. CHF ni tatizo katika nchi yetu. Hatuna namna ya kuremba kwenye hili, tuna tatizo kwenye hili eneo. CHF kwanza tumewaacha wenyewe wapange kiwango gani wanafikiri wachange ili Serikali iweze kuongeza. Wengi wanachanga sh. 10,000/= wanapewa ile card na Serikali imeweka Tele kwa Tele sh. 10,000/=; jumla sh. 20,000/=.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sh. 20,000/= ingawa wanaoumwa siyo wote, lakini haiwezi ikathamini afya ya mtu, sh. 20,000/= ni ndogo sana. Kwa hiyo, nafikiri kwa sababu tunawaandaa wananchi wetu kuweza kuchangia matibabu yao wenyewe, Serikali isitoe nusu, tuwaachie wananchi watoe asilimia 30 Serikali itoe asilimia 70. Tuanzie hapo! Nafikiri tukifanya hivyo, ule Mfuko wa CHF utakuwa na pesa nyingi itakakayoweza kuwasaidia wananchi kupata huduma nzuri za afya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mbunge, kwa sasa inaniwia vigumu sana kuwashawishi wananchi wajiunge na huu Mfuko kwa sababu wanakwenda hospitali wakiwa na bima yao hiyo hiyo ya CHF na hawapati dawa. Kuna kipindi inabidi uwe na moyo wa mwendawazimu kuwashawishi watu wajiunge na CHF, kutokana na hali halisi ambayo wananchi wanaiona kule hospitali. Kwa hiyo, naomba huu Mfuko tuufanyie ukarabati au tuuwekee muundo mwingine ambao utawafanya wananchi mara baada ya kujiunga wapate huduma sahihi ambayo walikuwa wanaitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu wamechangia kuhusu MSD, sitaki nipoteze muda katika eneo hilo. MSD pia ni tatizo, naiomba Serikali ipunguze madeni huko MSD ili kile chombo kiweze kufanya kazi ambayo tunaitegemea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo la On call Allowance, watu wengi wameichangia hapa. Mazingira ya watumishi wetu ni magumu lakini pia kiwango ambacho wanalipwa cha On call Allowance pia ni kidogo. Kwa mfano, katika mwaka huu wa fedha ambao tunataka tupitishe hapa, Wilaya yangu ya Nanyumbu inategemea kupata shilingi milioni tatu kwa mwezi, kwa watumishi wote hao. Hii ndiyo wapewe On call Allowance na hii zaidi ya nusu itatumika pale pale Makao Makuu ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, utakuta kiwango hiki hakitoshi na wengine watakosa, matokeo yake tunajenga chuki baina ya watumishi na Mganga Mkuu, kwa sababu wanaamini anakula, kumbe pesa haijakwenda ya kutosha. Matokeo yake sasa wanafanya kazi wakiwa na mori mdogo na wananchi wetu wanapata shida kwa sababu hawatumikiwi na watu ambao wana moyo wa kufanya kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kama kutakuwa na uwezo tuongeze kiwango hiki ambacho kitakwenda kama On call Allowance ili watumishi wetu wafanye kazi kwa moyo ili wananchi wapate huduma nzuri tunayoitegemea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nataka niutumie muda wangu vizuri, nataka nichangie eneo la wazee. Tulipokuwa tunanadi sera hizi tulizungumza vizuri sana kwamba tutawatumikia wazee. Nashukuru Wizara imejipanga namna ambavyo tutaweza kutoa huduma kwa wazee ikiwa ni pamoja na kuweka dirisha maalum la wazee.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tusiishie hapo, ni kweli tuweke dirisha maalum, lakini dawa zipatikane kwa wakati ili mtu aone kweli wazee tunawajali. Maana tutawawekea dirisha, hakuna dawa, bado tutakuwa hatujafanya chochote kile. Kwa hiyo, nashauri sana Wizara kwamba kwa sababu tunataka tuwajali wazee na tumewawekea dirisha maalum, tuhakikishe kwamba na dawa zinapatikana muda wote na dawa ni bajeti ya kuwa na pesa nyingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, napendekeza bajeti hii pia eneo la dawa ziongezwe ili wananchi wetu wapate huduma nzuri kama ambavyo Chama kiliahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana