Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Prof. Kitila Alexander Mkumbo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ubungo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii. Kwanza niungane na Mwenyekiti wa Kamati yetu, kupongeza sana juhudi za Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa miundombinu ya shule na hasa madarasa yale ambayo tumeyapata. Katika Halmashauri ya Ubungo tumeweza kupata madarasa 151 ambayo yamesaidia sana kupunguza changamoto hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ambalo nataka nichangie kwa dakika ambazo ninazo, ni haja ya Serikali kushughulikia upotevu katika mfumo wetu wa elimu. Kuna upotevu mkubwa sana na nitatoa mifano mitatu. Mfano wa kwanza, wanafunzi waliofanya mtihani wa Form IV mwaka 2021, walianza shule ya msingi mwaka 2011. Walianza wakiwa 1,500,000; waliofanya juzi mwaka 2021 ni wanafunzi 483,820. Inamaanisha watoto 1,000,000 na zaidi wamepotea wakiwa na umri wa miaka 13.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa pili, katika wanafunzi waliofanya mtihani wa Kidato cha IV 483,820, katika nchi hii huwa tunapima ufaulu katika madaraja manne; daraja la kwanza, la pili, la tatu na la nne na la mwisho la kufeli. Daraja la nne huwa tunaita ufaulu hafifu. Kwa hiyo, kwa maana ya ufaulu proper, daraja la kwanza mpaka la tatu katika wanafunzi waliofanya mtihani huo, 483,820 waliofaulu daraja la kwanza mpaka la tatu ni wanafunzi 173,000 peke yake sawa sawa na 35.8%. Inamaanisha katika eneo hilo pia, watoto takribani 300,000 wamepotea. Kwa hiyo, mpaka unafika form four umeshapoteza watoto 1,300,000, zaidi ya 70%. Big wastage!

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano wa tatu, mwaka 2021 Ofisi ya Waziri Mkuu wamefanya utafiti mzuri sana, unaitwa utafiti wa nguvu kazi katika nchi yetu; na wakabaini kwamba Tanzania tuna watu milioni 33 hivi ambao ni nguvu kazi wanaoweza kufanya kazi ambao ni 54% ya population yetu. Katika hao, 16% ya nguvu kazi hiyo hawajawahi kwenda shule kabisa; 65% ndiyo Darasa la Saba na 15% ndiyo form four. Inamaanisha kwamba mpaka hapo 96% ya nguvukazi yetu ni nguvukazi ambayo imepita katika mfumo wa elimu bila stadi zozote za kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya ufundi, VETA hii ambayo tunaizungumzia, waliopita katika nguvukazi ni 1%; elimu ya juu ya kati ni 1% nyingine. Vyuo Vikuu ambavyo mnadhani tuko wengi sana, nguvu kazi yetu ni 2% peke yake. Kwa hiyo, ni 4% ya nguvukazi yetu unaweza ukasema angalau wamepita katika mfumo fulani wa stadi za kazi na maisha. Very big wastage Maana yake nini? Ni kwamba mfumo mfumo wetu wa elimu haujasambaa. Ni mfumo ambao uko vertical, ukishakosea sehemu moja, unatoka katika mfumo. Kwa hiyo, lazima tatizo hili kama Serikali tulione. Ushauri wangu, badala ya kushughulikia changamoto hizi nusu nusu, tuupitie na kuupanga upya mfumo wetu wa elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili siyo geni. Mwaka 1982, Rais wetu wa Kwanza Mwalimu Nyerere aliunda Tume ya Makweta, maarufu kama Makweta Commission ikaupitia mfumo wetu wa elimu. Ilifanya kazi zaidi ya mwaka mmoja, ikatoka na taarifa ambayo ilitusaidia kwa miaka 20. Ndiyo iliyotupa Sera ya Elimu na Mafunzo ya 1995. Sera ya elimu na mafunzo Mheshimiwa Waziri wa Elimu ya 2014 siyo product ya research yoyote; sera pekee ambayo ni product ya research ni ya 1995. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwa bidii kwamba Waheshimiwa Mawaziri na Serikali tumshauri Mheshimiwa Rais akubali kuunda a Presidential Commission ambayo itapitia upya mfumo wetu wa elimu tupange upya. Jambo hili kugusa tu mtaala wa Primary na Sekondari, haiwezi kututoa. Tunahitaji elimu ambayo ita-fit katika karne ya 21 na ambayo itatupeleka miaka 20 mingine ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri dira yetu inaisha mwaka 2025, kwa hiyo, na hii itatupa nafasi ya kwenda sambamba na dira yetu ya mwaka 2025.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuyasema hayo, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)