Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika hoja za Kamati zilizoko mbele yetu. Hali ya upatikanaji wa dawa hapa nchini katika hospitali zetu, vituo vya afya na zahanati kwa ujumla ni mbaya na dawa hazipo na wananchi hawapati huduma zinazostahiki. Tunafahamu tuna bohari ya dawa ambazo kazi yake ni kununua na kusambaza dawa na sasa tumeipa jukumu lingine, tumebadilisha sheria ya kuanzisha viwanda vya kutengeneza dawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba hii MSD imezidiwa. Mara nyingi hapa Bungeni tumekuwa tukisema tu Serikali ina idai MSD, labda ufanisi wa MSD hauonekani kwa sababu inaidai fedha nyingi. Mimi naona kama hicho ni kichaka tu cha kujifichia humo. Ni kweli kwamba inaidai Serikali na ripoti mbalimbali za CAG zimeonyesha, lakini MSD yenyewe pamoja na kidogo kinachopatikana, bado mfumo wake wa usambazaji wa dawa ni hafifu wa kizamani na hautoi matokeo yale ambayo wananchi wanayatarajia na huduma kule kwenye vituo vyetu, hazipatikani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hata Naibu Waziri wakati anajibu swali hapa akasema shida siyo fedha, fedha zipo lakini shida nadhani nyingine wanaijua. Kwa hiyo, nadhani iko haja sana ya kufanya kufumua MSD na kuiunda upya kwa kuangalia mahitaji ya leo na kuweka mfumo ambao usambazaji wa dawa utatosheleza na utafika kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kwenye Mkoa wangu wa Arusha, sasa hivi MSD wanapita kwenye vituo wanapeleka dawa. Wananchi wanaona gari limefika, linashusha dawa, lakini wanashusha dawa za wiki moja tu, magari yanaondoka. Hata hilo gari halijafika kwenye Bohari Kuu, huku nyuma dawa zimeisha na mpaka warudi, siyo leo. Kwa hiyo, tusitegemee tena wananchi watapata huduma. Kwa hiyo, ni lazima tuangalie namna gani tutahakikisha wananchi wanapata dawa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mwingine, tuliambiwa kwenye Kamati juzi; leo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuna uhaba mkubwa sana wa hizi blood bags, mifuko ya kuwekea damu; na wenyewe wamekiri kabisa pale Muhimbili hakuna, lakini maeneo mengine nchini inapatikana, iko mpaka ya ziada. Sasa unajiuliza, kuna nini? Maana yake kuna tatizo la mgawanyo na usambazaji na usimamizi wa dawa pamoja na vifaa vyote vya dawa hapa nchini. Kwa hiyo, iko haja sana ya kuitizama MSD na kuifumua na kuhakikisha kwamba inafanya huduma ambayo inatakiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, hapa juzi juzi tulisikia tamko la Waziri kuhusiana na kufunga maduka yote ya dawa zilizoko karibu na hospitali au vituo vya afya au vinginevyo; na amerejea sheria ambayo tuliipitisha hapa Bungeni. Hiyo sheria inaonesha kabisa kwamba duka la dawa kwenye hospitali itakaa mita 500; kwenye ngazi ya mkoa itakaa mita 400; kwenye ngazi ya wilaya itakaa mita 300; kwenye vituo vya afya na zahanati itakaa mita 200; na akaagiza kwamba ziondoke.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani hili tamko siyo sahihi, kwa sababu kwanza haya maduka ni Serikali wenyewe mmesaidia kuyafanya yashamiri na kustawi, kwa sababu maduka yetu ya dawa zilizopo ndani ya hospitali hakuna dawa. Kwa hiyo, mwananchi hayuko tayari mgonjwa wake afe kwa sababu hakuna dawa ndani ya hospitali eti asiende kutafuta kwenye duka la dawa. Kwa hiyo, nyie wenyewe mmesaidia kuyafanya yashamiri na hawa watu wanaendesha biashara kihalali, wako kihalali, mmewapa vibali wenyewe, wanalipa leseni, wanalipa kodi, leo mnawaambia waondoke. Hilo siyo suluhisho. Kuwaambia maduka haya yaondoke, siyo suluhisho la kuhakikisha dawa zinapatikana kwenye hospitali zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa ni kuimarisha MSD. Kuhakikisha MSD inatoa dawa zote na kwa wakati katika hospitali zetu. Hospitali zetu, vituo vya afya na zahanati zikiwa well equipped na dawa zote, haya maduka automatic yatapotea, hayatakuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nadhani Serikali kwenye hili jambo muiache kama ilivyo. Mwananchi yeyote hayuko tayari kuona eti mtu wake anafariki hapa kwa kukosa dawa asiende kutafuta dawa kwenye duka la dawa kwa sababu Serikali imetoa tamko, haiwezekani. Kwa hiyo, ni Serikali kuhakikisha MSD inaimarishwa, inasambaza dawa zote muhimu kwa wakati na wananchi wanapata dawa ambazo zinatakiwa kulingana na ugonjwa ambao anaugua. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni upungufu wa watumishi wa afya. Ripoti mbalimbali za CAG zimeonyesha tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya. inakaribia 52% ya watumishi wa afya ambao wanahitajika waajiriwe ili huduma muhimu na stahiki ziweze kutolewa kwenye vituo vyetu vya afya na katika maeneo yote ambayo tunatoa huduma za afya. Hata hivyo, bado ajira hizi hazijatangazwa. Maana yake ni kwamba, huku tuna changamoto ya dawa, huku hatuna watumishi; hivi mnawataka nini Watanzania hawa? (Makofi)
Mheshimwia Mwenyekiti, kama tunaweza kukopa fedha tukajenga SGR, tukajenga sijui Mwalimu Nyerere Stiegler’s Gorge, kwa nini tusiwekeze kwenye afya za Watanzania? Hata hiyo SGR na Stiegler’s Gorge tutakuwa tunamjengea nani kama Watanzania wote watakuwa wagonjwa, hakuna dawa? Itakuwa ni kazi bure. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Serikali iliweza kufanya maamuzi yale ikaweza kutafuta fedha kujenga SGR, kujenga Stiegler’s hivyo hivyo fanyeni uamuzi sahihi…
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Mheshimiwa Dkt. Mollel.
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza sipingani na mawazo mazuri ya Mheshimiwa Mbunge, lakini nilitaka tu nimpe taarifa kwamba unapoajiri, unaajiri kulingana na ukuaji wa uchumi wako na unapokopa, unasisimua uchumi ukue ili uweze kuajiri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa kwamba kwa mwaka huu tu tayari tumeruhusiwa kuajiri watu 21,000. Hata hivyo, ukikopa ukawekeza hizo fedha, kuna maeneo matatu ya kuwekeza ili uchumi ukue na uweze kuajiri wengi; uwekeze kwenye human resource capital, ambayo ndiyo imewekezwa sasa hiyo shilingi bilioni 1.3 kwenye elimu, afya na sehemu nyingine ambazo zinaenda kukuza na kukuza pato letu la Taifa; tunawekeza kwenye teknolojia na maeneo mengine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nakubaliana na mawazo yake, lakini anachokifanya Mheshimiwa Rais ni hicho hicho anachokisema yeye. (Makofi)
MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Cecilia Daniel Paresso, pokea taarifa.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Tunatambua kwamba uchumi hauwezi kuwa muhimu sana kuliko afya za Watanzania. Yaani inaweza ikawa inaenda sambamba, lakini naongelea hapa afya za Watanzania kwa ujumla wake. Mnaweza mkawa mmetoa hizo ajira, lakini bado uhitaji ni mkubwa. Si tuko kule tunaona kwenye vituo vyetu vya afya, zahanati na kila mahali.
Kwa hiyo, nadhani waipokee kama ushauri na Naibu Waziri utapata nafasi, utakuja kueleza hayo na tutaendelea kushauri na ndiyo wajibu wetu mkubwa wa Wabunge hapa Bungeni.
MWENYEKITI: Sasa endelea kuchangia Mheshimiwa Paresso baada ya kupokea taarifa nzuri ya Serikali.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa nasema suala la watumishi wa afya, ajira ni muhimu na ninaendelea kulisisitiza kwamba ni muhimu Serikali iajiri kuhakikisha Watanzania wanapata ajira.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nilikuwa naeleza kwamba kama tunaweza kuwekeza nguvu kubwa kwenye masuala ya kiuchumi kwa maana SGR, Stiegler’s, hawa Watanzania ambao wanategemewa waje watumie hayo kwa kuwa na afya njema, kama hatujawaandalia mazingira ya kuwa na afya njema kwa kuhakikisha dawa na huduma katika hospitali zetu zinapatikana inavyotakiwa, itakuwa ni kazi bure. Tutakuwa na Taifa la watu ambao ni wagonjwa, hakuna dawa. Tutakuwa na Taifa ambalo haya tunayoyatengeneza, hayatakuja kutumiwa kwa sababu watu wote wanaumwa hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoshauri ni kwamba uwekezaji kwenye sekta ya afya kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba watumishi wa afya wa kutosha kwenye sekta hii, itiliwe mkazo sawa sawa na mkazo ule ule kwenye sekta nyingine ambazo tunaziona kwa sasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo,...
MWENYEKITI: Kengele ya kwanza Mheshimiwa. Endelea, hiyo ni ya kwanza itagonga ya pili. Malizia.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee suala lingne kuhusu mtaala wa elimu ambao tunaufanyia marekebisho kwa sasa. Kama ambavyo Serikali imesema na kama ambavyo ripoti yetu imeonyesha, ni kwamba tunatarajia mtaala huu utakuja kuanza utekelezaji 2026. Najiuliza swali moja; Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Marehemu Hayati Dkt. Magufuli, kipindi hicho alitoa agizo kuhakikisha tunaingiza somo la historia kwenye mtaala wetu wa elimu na mtaala ufanyiwe maboresho. Jambo hilo lilitekelezwa within two months or three months na ikafanyika na Wizara ikatengeneza vitabu, ikachapisha, wanafunzi wakaanza kufundishwa, ikatekelezeka. Leo kwa nini tunashindwa kuhakikisha kwamba hii sera yetu ya elimu inayofanyiwa maboresho inaenda kutekelezwa on time? Kwa nini mpaka 2026? Kuna nini hapa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kinachoonekana ni kwamba hakuna utayari au utashi wa kuhakikisha suala hili linafanyika. Tukumbuke kwamba dunia ya leo inakimbia, sisi inawezekana tuko nyuma sana. Huko duniani watu wanakimbia, ugunduzi unaendelea, mambo yanaboreka kila siku. Profesa hapa ameeleza vizuri sana, kama tukiwa wagumu, tukiwa na urasimu wa kufanya mabadiliko na kukubali mabadilika kwa wakati…
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.
MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Nusrat Hanje.
T A A R I F A
MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba anachokisema ni ukweli na hata Sera ya Sayansi na Teknolojia ambayo ilitakiwa iwe Sera ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu imeishia kwenye Sera ya Sayansi na Teknolojia, lakini pia ni ya mwaka 1996, ina miaka 28. Hata Sheria ya COSTECH ni ya mwaka 2000. Yaani sera yenyewe tunayoizungumzia maana yake itakuwa outdated kabla hata haijaanza kutekelezwa, kwa sababu lifespan ya sera ni 10 years. Ahsante. (Makofi)
MWENYEKITI: Mheshimiwa Paresso, taarifa hiyo.
MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nimeipokea taarifa hiyo nzuri sana na naamini pia wameisikia. Hoja yangu hapa ni kwamba, sijui kwa nini Wizara wanakuwa wagumu au wazito na kunakuwa na urasimu mkubwa. Najua, inaweza ikawa ni mabadiliko ambayo yanahitaji mambo mengi, lakini tujaribu, tufanye huo uthubutu, tuhakikishe kwamba Sera ya Elimu tunaitekeleza kwa wakati na tuendane na dunia na teknolojia ya leo, kuhakikisha kwamba tunazalisha na tunatoa wataalam ambao wanakubalika duniani katika kuingia kwenye soko la ajira na kuisaidia nchi kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hayo tu, nakushukuru sana, na naunga mkono hoja ya Kamati.