Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Masuala ya UKIMWI kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia. Nitajikita kwenye mambo mawili, sana sana katika suala la ustawi wa jamii na suala la pili litakuwa kuhusu dawa za kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa huu mwezi wa kwanza tumekuwa tukishuhudia matukio mbalimbali ya watu kufanya mauaji kwa watoto wadogo, wanandoa na watu mbalimbali katika familia. Tunafahamu chanzo cha mauaji hayo na kwa taarifa zilizopo mengi yametokana na masuala ya mahusiano, migogoro ya ndoa, uchawi pamoja na mirathi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukianza kuangalia masuala haya kwa jicho la kawaida unaweza ukalichukulia hili kama ni suala dogo sana, lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda ndivyo wimbi hili litakavyokuwa linaendelea kuongezeka kukua kwa watu tofauti fofauti na mikoa tofauti tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kusema nini, najaribu kuonesha role ya watu wa ustawi wa jamii ilivyo muhimu kwenye jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ningependa nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia Wizara mpya ya Maendeleo ya Jamii ambayo ameitofautisha na Wizara ya Afya. Hapa nadhani ndipo roles za hawa watu wa maendeleo ya jamii na ustawi wa jamii zitakavyoanza kutofautishwa kwa uzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watu hawa wa ustawi wa jamii ni watu muhimu sana katika kufanya counselling kwa ajili ya ku-restore psychological status ya watu katika jamii zetu. Hata hivyo, unakuta watu hawa katika jamii hawatambuliki na hawapewi kipaumbele na hata bajeti yao ipo chini. Kwa hiyo kupitia taarifa hii ya Kamati ya Huduma ya Jamii nilitamani walichukue hili na kuweza kulifanyia utafiti vizuri au kulipa kipaumbele kwa namna tofauti ili watu hawa ajira zao ziongezwe, hata ikiwezekana wafikie angalau kwenye level ya kata ili wawe na uwezo wa kubainisha haya mambo yanayoendelea kwenye jamii haraka kabla mauaji hayajatokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa pia kuongelea suala la dawa za kulevya. Kama tulivyosikia kwenye taarifa, kwamba changamoto ya dawa za kulevya katika nchi yetu bado ni kubwa na hususan kwa watu wanaotoka mipakani suala hili limekuwa ni gumu zaidi kwa sababu vijana wengi wanaathirika na dawa za kulevya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema kuwa kuna ongezeko, japokuwa taarifa hazijawa bayana katika taarifa ya Kamati, lakini niseme tu kuwa ongezeko la dawa za kulevya ni kubwa na warahibu hawa wana athari nyingi kwenye jamii. Tumeanzisha clinic mbalimbali katika maeneo mbalimbali ambapo warahibu hawa wamekuwa wakiendelea kupewa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto inayokuja, unakuta mrahibu yuko kwenye methadone clinic lakini unakuta askari bado wanaendelea kumbughudhi na wakati huo huo wakimkamata na wakimpeleka Central Police wanamkatisha hii dozi ya methadone. Kwa hiyo natamani kwamba hili liweze kupewa kipaumbele, kwamba mrahibu anapokamatwa apewe fursa ya kwenda kupata huduma hii ya methadone kwenye zile clinic ili asiweze kukatisha ile dose yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizi methadone clinics hakuna huduma za lishe. Tunafahamu kabisa kuwa mtu ambaye anatumia dawa za kulevya anakuwa katika mazingira hatarishi ya kuwa na lishe duni. Anaweza akawa na overweight au akawa na underweight, kitu ambacho tunajua kabisa, kwamba uwezo na ufanisi wake wa recovery mwilini unakuwa chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, natamani kuona kwamba katika vituo hivi suala la lishe linapewa kipaumbele ili hawa wanapoendelea na matibabu wapone haraka, kama lishe itakuwa vizuri wataweza kupona haraka.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kumalizia naomba dakika moja tu.

MWENYEKITI: Haya, nakuongezea dakika moja Mheshimiwa Neema, malizia.

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hawa watu wakishapewa matibabu wanashindwa kurudi kwenye jamii kwa sababu wanakuwa hawana kazi.

Kwa hiyo kama tunaweza kutenga asilimia mbili za mikopo kwa walemavu, asilimia kwa vijana na wanawake, basi kungekuwa na hili kundi pia lipewe kipaumbele kwenye jamii kama sehemu ya kukopeshwa fedha ili waweze kuingia kwenye jamii wakiwa na kipato. Ahsante. (Makofi)