Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Rombo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwa sababu nami ni mara yangu ya kwanza kuzungumza baada ya Mheshimiwa Rais kuniteua kuwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kutoa shukrani nyingi kwa Mheshimiwa Rais kwa uteuzi huu na kumwahidi kwamba tutafanya kazi kwa bidi, timu yote, kwa ajili ya kuleta mabadiliko ambayo sote tunayatarajia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda vilevile kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa fedha hizi za ahueni ya UVIKO ambazo sekta ya elimu kwa ujumla wake ndani ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na TAMISEMI tumepata zaidi ya bilioni 300 ambayo kwa kweli inatusaidia sana kusonga mbele, hasa katika suala la miundombinu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeisikiliza vizuri Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii. Tunamshukuru sana Mwenyekiti, Mheshimiwa Stanslaus Nyongo na Wajumbe wote kwa taarifa nzuri ambayo tutazingatia sana ushauri ambao wameutoa. Napenda kukuhakikishia vilevile tutazingatia ushauri ambao umetolewa na Waheshimiwa Wabunge kwa mapana yake katika utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kueleza vitu vichache ambavyo vinahitaji ufafanuzi. La kwanza ambalo linaweza likawa linazusha taharuki ni kuhusu transition ya wanafunzi kutoka darasa la kwanza mpaka la saba kuanzia form four kwenda form five, form six, kwamba tuna dropout kubwa sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu zetu hazioneshi kama net enrollment rate hata gross enrollment rate Tanzania ni mbaya. Tulipata peak kubwa sana ya enrollment baada ya Serikali kutangaza kutoa elimu bure, na enrollment iliongezeka sana mwaka 2016. Ili tuweze kuona picha vizuri najaribu kutoa takwimu za wanafunzi waliofanya mtihani Darasa la Nne na waliofanya mtihani Darasa la Saba. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukiangalia wanafunzi waliofanya mtihani Darasa la Nne mwaka 2018, walikuwa ni 1,362,642 na walipofika Darasa la Saba 2021, waliofanya mtihani ni 1,132,084. Noteworthy alarming lakini haturidhiki na transition hiyo na hao ambao wame-drop hapo katikati. Hata hivyo, figure siyo kubwa kama ambavyo imekuwa alluded to, hapo mwanzoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hizi takwimu ni vizuri kama tunataka kuziangalia kwenye NBS, net enrolment rate ambayo inaonesha watu ambao kwa umri fulani walitakiwa wawe darasa fulani, na wangapi bado wapo katika darasa hilo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hivyo, ningependa nieleze kwamba Serikali hasa chini ya Uongozi wa Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, imejikita sana kuhakikisha kwamba wale wote ambao wana-drop shuleni kwa sababu mbalimbali, wanarudi shuleni. Ndiyo maana ya maelekezo ya Mheshimiwa Rais tumetoa mwongozo, tumeusambaza, kuonesha namna gani ya kuwarudisha tena wanafunzi ambao waliacha shule kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na wale ambao walipata ujauzito; na wengine kwa sababu walikuwa na changamoto ambazo hawakuzijua. Kwa mfano, mwanafunzi alikuwa na matatizo ya kusoma hakujua kwamba anahitaji miwani, akaacha shule. Baadaye akagundua kumbe nahitaji miwani, anataka kurudi shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunajaribu kutoa fursa kwa kila mwanafunzi ambaye hata kama alikuwa ameshaacha shule, aweze kurudi shule na kuendelea kusoma ili tuhakikishe kwamba namba zinaongezeka kutoka hizi namba ambazo nilikuwa nimezieleza hapo katikati. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imeshauri sana suala la kuongeza ajira hasa ya walimu; na ni kweli kuna upungufu mkubwa wa walimu. Serikali imewekeza sana sasa hivi kama tulivyoona katika miundombinu ya ufundishaji hasa madarasa na vifaa vilevile vimenunuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, ukweli ni kwamba bado tuna upungufu mkubwa wa walimu. Wengine mtakuwa mlimsikia Mheshimiwa Rais wakati anapiga simu kuongea na walimu na wanafunzi wa Benjemin Mkapa Secondary School pale Dar es Salaam. Alieleza kwamba baada ya miundombinu, kazi kubwa sasa hivi ni kuajiri walimu ili kuhakikisha kwamba tunapata walimu wa kutosha.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba dakika moja nielezee suala la mitaala ambalo kidogo ni muhimu, niache haya mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati vilevile imeeleza na Waheshimiwa Wabunge wamesisitiza tumalize mapema iwezekanavyo mapitio ya mitaala na ndicho tunachojaribu kukifanya. Hata hiyo tarehe ambayo imewekwa tungetaka tumalize kabla ya hapo. Pia ningependa tuzingatie kwanza kwamba mitaala hii inaongozwa na Sera. Sera ya 2014 inafanyiwa mapitio, Sheria, halafu mitaala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, ukiangalia Sera ya 2014 inaelezea miaka sita ya elimu ya msingi; elimu ya lazima mpaka Form Four. Maana yake ni kwamba hata mitaala inapotengenezwa lazima izingatie suala hili, endapo sera itakapofanyiwa mapitio, tutabaki na vigezo hivyo hivyo. Kwa hiyo, tunafanya mapitio ya sera na wakati huo huo tunapitia mapitio ya sheria na tunapitia vilevile mitaala. Pia kama Kamati ilivyoshauri, tunapitia mitaala siyo kwenye elimu ya msingi tu, ni pamoja na Vyuo na Vyuo Vikuu, na miongozo imetolewa na kazi inaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naona kengele imeshagongwa, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)