Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nikushukuru kwa nafasi hii. Kabla ya kusema lolote nipongeze kwanza Kamati zote mbili kwa taarifa ambazo kimsingi ndizo kazi tunazozifanya katika Kamati na ndizo kazi za Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ninayo machache ya kutoa mchango wangu katika Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa. Ninaomba nishauri jambo; tumepokea miradi mingi sana ya maendeleo katika maeneo yetu kupitia Serikali za Mitaa lakini kuna changamoto kubwa kwamba wataalam wetu walioko katika Wizara hii ya TAMISEMI wamekuwa wakigawa mafungu haya kwa ulingano, kwa maana ya kwamba kama tunajenga shule ya msingi au darasa la shule ya msingi ama sekondari, tunaletewa pesa ambayo inafanana nchi nzima, lakini mazingira ya nchi nzima hayafanani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Wilaya za Lushoto, Makete, Kyerwa nadhani na Tarime, yale maeneo ambayo zaidi yanalimwa kahawa ni maeneo ambayo ni ya milima. Ukiwapa pesa sawa na sehemu ambayo ni tambarare maana yake haziwezi zikawa na tija ile iliyokusudiwa. Kwa hiyo, tuwaombe sana wataalam wetu waangalie haya wakati wanapanga mipango hii ya Serikali wazingatie jiografia ya baadhi ya maeneo ili tusipewe pesa ambayo inalingana na maeneo mengine hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo lingine ambalo ningependa kutoa mchango wangu ni eneo la mapato ya halmashauri kwa maana ya mapato ya ndani asilimia 20 ambazo zinapaswa kurudi kwenye Serikali za Vijiji. Fedha hizi zilikuwa kipindi cha nyuma wakati halmashauri nyingi zilikuwa zinawajibika kuwalipa Madiwani, zilikuwa hazipatikani vizuri kurudishwa katika vijiji. Sasa kwa kuwa Serikali imebeba mzigo wa kulipa posho za Madiwani tungependa kuona sasa asilimia 20 ikisimamiwa kurudi kwenye Serikali za Vijiji. Maana huko ndiko ambako miradi hii ya Serikali inakwenda kutekelezeka na wasimamizi wakubwa ni Wenyeviti wa Serikali za Vijiji pamoja na Wenyeviti wa Vitongoji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzetu hawa na ambao wenyewe wanachaguliwa kama sisi, wanakuwa hawapati ruzuku yo yote kutoka Serikalini. Hata hivyo, tunaamini kwa mwongozo uleule uliopo ambao mwanzoni ulikuwa unatumika kulipa Madiwani na sasa dhamana ya Madiwani imekwenda Serikali Kuu hii asilimia 20 basi ni vyema ikarudishwa kwenda kulipa Wenyeviti kwa msisitizo na kusimamiwa kwa mujibu wa sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ningependa kulichangia katika mchango wangu ni suala la asilimia 10 ya fedha hizi za halmashauri ambazo zinakwenda kwenye Mfuko wa Vijana na Wanawake na zile asilimia mbili kwa Wenye Ulemavu. Eneo hili bado lina changamoto, nipo katika Kamati ya LAAC ambako mara kadhaa tumekuwa tukizihoji halmashauri. Unaona mara zote fedha hizi zinaonekana zinaendelea tu kutoka japokuwa kwa tafsiri Mfuko huo unaitwa Revolving Fund, ni fedha ambayo inatakiwa itoke kisha irudi, lakini mara zote tukija tunaona tu kwamba zinatoka zile zinazorudi halmashauri zimekuwa na usimamizi hafifu katika kusimamia sheria na kufanya zile fedha zirudi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi ningependekeza, kwamba hili jambo kwanza msisitizo uwepo kwenye Revolving Fund kwamba fedha zikishakopesha zirudi. La pili, Serikali itazame model nzuri zaidi ya kuja na jambo hili. Sasa hivi halmashauri zote zinatenga sawa asilimia 10, lakini hazilingani mapato, nadhani wangetumia model ya Mfuko wa Jimbo ambao unatumia population.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli inawezekana Wilaya ya Lushoto ina population kubwa lakini mapato yake ni madogo na kuna wilaya nyingine ni ndogo, lakini mapato yake ni makubwa. Sasa huu wingi wa vijana ukawa unatofautiana, hivyo wa Lushoto pamoja na wingi wao wakapata kidogo kwa sababu mapato yao ni madogo. Kwa hiyo ni lazima kuja na mpango wa ku-centralize haya mapato yote labda katika Mfuko Maalum halafu sasa yaende kwenye makundi haya ya vijana kwa kuzingatia hata fani ambazo wanasoma katika Vyuo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mathalan, sasa hivi tuna vyuo ambavyo wame-graduate mainjia wengi, tunaweza tukaanzisha kampuni ndogo za mainjinia, wakapelekwa katika miradi midogo midogo labda ya barabara, ya usambazaji umeme vijijini, ya maji na kadhalika kwa kupitia Mifuko hii na baadaye tunaweza tukaiona tija kubwa zaidi kuliko ambayo tunayoiona sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja Kamati zote mbili. Ahsante sana. (Makofi)