Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Hai
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SAASHISHA E. MAFUWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia kwenye taarifa za Kamati hizi mbili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natokea Kamati ya Utawala na Serikali za Mitaa, tumepokea taarifa kutoka halmashauri zote nchini juu ya utekelezaji wa Miradi ya UVIKO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Raisi Mama Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa kwa kweli aliyoifanya na ubunifu mkubwa sana, lakini niwapongeze Mheshimiwa Waziri na watumishi wote kwa namna ambavyo wamesimamia fedha hizi. Tumepokea taarifa kutoka kwenye halmashauri kwa kweli wamefanya kazi nzuri, hongereni sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo madarasa yamejengwa, vituo vya afya vimejengwa, miradi ya maji imekwenda, nampongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri aliyoifanya na niseme kwa style hii hii Mheshimiwa Rais atafute fungu lingine alitupie kule kilimo. Kule kilimo tukipata kama shilingi trilioni moja naamini sasa tumemaliza kazi nchi hii itasonga kwa speed kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri kwenye eneo la asilimia 10; fedha hizi ambazo ni nyingi tumeambiwa hapa ni karibu ni bilioni 70 zimekopeshwa. Utaratibu wake bado hauridhishi, tumepokea taarifa kwenye kamati yetu, tunaona namna halmashauri inavyojikanganya wengine wanakiri kabisa hawana taarifa sahihi kwenye jambo hili. Sasa mimi nashauri mambo yafuatayo: -
(i) Taasisi yetu inayohusika na TEHAMA kwa maana ya e-government watengeneze mfumo wa ku–capture taarifa zote kutoka kwenye Halmashauri ili tuweze kujua fedha ambazo zimepatikana ni asilimia 10, fedha za marejesho ni kiasi kadhaa, vikundi vilivyokopeshwa ni kiasi kadhaa na majina yao ili kukwepesha ujanja ujanja, hii kazi e-GA wanaweza kuifanya waifanye ili tuweze kufanya maboresho. (Makofi)
(ii) Pia tutazame sheria, hii sheria imefanya vizuri, lakini kuna kundi linaachwa, tunasema vijana wanaokopeshwa ni kuanzia umri wa miaka 18 mpaka 35, lakini miaka 35 na kuendelea na tunaamini miaka 35 – 45 ndio kundi lenye sasa limetulia linataka kufanya kazi, kundi hili la wababa halimo. Niombe tutazame namna ya kufanya marekebisho ili na hao wanaume nao waweze kukopesheka wafaidi fedha hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu sana na mimi kwenye jimbo langu la Hai wamenituma, wakina baba wanasema tumeaacha kwenye eneo hili. Tafadhalini sana tulete hiyo sheria tuifanyie mabadiliko hapa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hili ambalo limejitokeza, sasa hivi tunapokea taarifa ya masoko yetu kuungua na wenzangu wamechangia hapa. Niende kwenye suluhu, baada ya matukio haya nimejifunza kitu nikaenda kwenye historia; kwanza nikatazama majukumu ya Jeshi letu la Zimamoto, nikajiuliza hivi tunahitaji makamishna, tunahitaji mabrigedia, tunahitaji maafisa kwenye kuzima moto kweli. Nikagundua mwaka 1950 kazi ya kuzima moto na uokoaji ilikuwa inafanywa na halmashauri, na ilifanya vizuri, baadae mwaka 1982 wajibu huu ukahamishwa TAMISEMI, wakaendelea kufanya vizuri. Sasa hivi najiuliza administrative cost za chombo hiki zingeweza kuhamishwa zikaenda kukunua magari ya fire. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri sasa Serikali itazame upya namna ya kurudi kule kwa mwaka 1950, jukumu hili lishushwe halmashauri ambayo inakusanya, inaweza ku-manage na kuajiri watu ambao wanaweza kufanya kazi ile. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini watumishi au vibarua wanaweza kufundishwa ukiancha ile top layer wakafanya kazi hii kuliko kuwa na maafisa wengi wana consume a lot, halafu tunashindwa ku operate. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana watuletee sheria tuone upya namna ya jukumu hili lirudishwe kwenye Halmashauri, mfano Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam zikipewa jukumu hili zinaweza kufanya vizuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naomba niishie hapo na niunge hoja mkono, ahsante. (Makofi)