Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana. Wenzangu waliotangulia kwenye Kamati wamezungumza kuhusu usimamizi wa asilimia 10, nami naomba tu kuongezea jambo dogo kwamba ukilisikiliza unaona ni jambo dogo lakini nataka nitoe mfano wa halmashauri yangu. Halmashauri yangu inakusanya takribani bilioni nane mpaka bilioni 11 kwa mwaka, maana yake inatenga kati ya milioni mia nane na bilioni 1.1 kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukirudisha miaka mitatu nyuma ukawaambia naomba tuangalie akaunti hii ina shilingi ngapi hakuna hela na wanasubiri maombi mapya ya vikundi, wanasubiri makusanyo ya halmashauri ya quarter hiyo ndiyo wawagawie walioomba. Maana yake ni kwamba fedha hizi takribani bilioni tatu za miaka mitatu nyuma hazijarudi na kwa sababu zilifunguliwa akaunti ya kujitegemea maana yake ni kwamba hazipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili ni kubwa kuliko tunavyofikiri na tumeshauri kwenye Kamati, inawezekana watumishi wanaopewa kazi ya kusimamia Mfuko huu, ujuzi na uwezo wa kusimamia mafungu makubwa haya ya fedha hawana. Sasa ni juu ya Wizara kuangalia utaratibu mzuri wa kufanya jambo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine la pili nilizungumza mwaka jana wakati wa briefing kwamba Sheria ya Kodi Na. 332, sehemu ya kumi ambayo inawapa mamlaka TRA ya kukusanya fedha inagongana na Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa Na. 290 na Sheria ya Serikali za Mitaa Na. 288 na matokeo yake inasababisha wapangaji kwenye majengo ya halmashauri kuhama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili liko ofisini kwa Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na sheria hiyo ambayo imezipa mamlaka Halmashauri za Miji, Manispaa na Wilaya kubuni na kuanzisha vyanzo vya mapato imeipa pia Mamlaka ya Kodi ya Mapato kutokutozwa kodi. Sheria inasema kwenye Kifungu cha 6(1) kwamba all assets vested in the urban authority by virtue of this section… zimetajwa pale, anasema ni all moneys derived from any trade, industry, works, services and other undertaking properties owned by the Council, zimeelezwa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida inakuja sasa tafsiri ambayo wanakuja nao halmashauri wanasema kwamba pamoja na sheria kutoa mamlaka hayo, nashindwa kuisoma sheria kwa sababu ya muda, wanasema iwapo halmashauri imewekeza majengo makubwa na wameweka wapangaji wao wanakwenda kukusanya kodi kutoka kwa wale wapangaji kwenye kodi ya pango ambayo halmashauri inalipwa. Kwa hiyo, yule mpangaji anapolipa pango la halmashauri asipolipa withholding tax ya TRA wanafunga account.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria yake imeeleza vizuri lakini Ofisi ya Mwanasheria Mkuu tuliomba ufafanuzi kwenye jambo hili na ikaeleza vizuri ikasema kwamba kwa maoni yao wao wanafikiri kwamba sheria iko clear na TRA hawapaswi kutoza kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mwanasheria Mkuu atusaidie, Wizara ya Fedha itusaidie, halmashauri yangu wapangaji wanahama kwenye majengo kwa sababu wanalipa kodi mara mbili. Sisi hatutaki kujua kwa sababu sheria inatulinda kwa sababu tunataka tulipe hela tuliyoelewana nayo, anapotulipa anaambiwa akate hela ya halmashauri na matokeo yake asipolipa anafungiwa akaunti. Hii ni Serikali moja ni lazima tukubaliane, jambo hili kwa nini lifanyike Geita peke yake na lisifanyike sehemu nyingine? Kama ni sheria iwe uniform itangazwe ijulikane.
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho kama utaniruhusu…
MWENYEKITI: Malizia sentensi ya mwisho.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ni jambo la ajira, limezungumzwa vizuri kabisa na wenzangu. Tunaishukuru Serikali imeajiri Walimu 11,000, lakini Wizara ilikuja ikatufanyia presentation, mahitaji ya walimu ni 120,000 wa primary na sekondari.
Kwa hiyo utaona ni asilimia kumi ya walimu walioajiriwa, sasa ukiwa na deficit ya 90 percent ukategemea kutengeneza quality inayofanana na ujue hii 90 percent deficit ipo zaidi vijijini ambapo wale waliopo vijijini hawana access na tuition na mengine lazima utegemee product ambayo haifanani kwenye mtihani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba jambo hili liangaliwe vizuri. Nakushukuru sana. (Makofi)