Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

Hon. Jenista Joackim Mhagama

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Peramiho

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, vilevile nishukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwa na imani na mimi na Msaidizi wangu Mheshimiwa Deo Ndejembi na hasa kutuamini kwamba tunaweza tukafanya kazi ndani ya ofisi yake. Tunamwahidi kutembea katika kiapo ambacho tulikula mbele yake utii, uaminifu, uzalendo na utendaji kazi uliotukuka, tutafanya kazi kwa bidii sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuchaguliwa na Wabunge, Naibu Spika na kipekee nipongeze Mwenyekiti wangu wa Kamati kwa kuchaguliwa na Kamati yetu kuongoza Kamati hiyo na Makamu Mwenyekiti, pia na Wenyeviti wengine wote wapya naamini tutakwenda sawasawa. Nawapongeza sana Wajumbe wa Kamati kwa kweli nimekutana na Kamati inayoweza kufanya kazi kwa nguvu sana, naomba niwahakikishie ushirikiano mimi na timu nzima ya Ofisi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani nianze kwanza kwa kuungana na Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote wanaompongeza sana Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan. Naomba nikiri kwamba tunaye Rais mwenye maono, Rais mzalendo, Rais ambaye anatamani kuiona nchi yake inapata maendeleo kwa haraka sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyasemi hayo kwa unafiki, naomba hayo kwa mifano halisi ya namna ambavyo Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa kweli. Ninayo mifano hasa inayotoka ndani ya Ofisi yangu, Ofisi ya Rais ambayo inashughulika na masuala ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda wa mwaka mmoja tu, Taifa letu limeweza kushika nafasi ya 87 kwa kufanya vizuri kwenye masuala la utawala bora ikizishinda nchi nyingi tu duniani kati ya nchi 180; na imeshika nafasi ya pili katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Tunafanya vizuri. Tunaposema masuala ya utawala bora ni masuala pia ya utendaji haki kwa kutumia vyombp na taasisi zilizoko ndani ya Ofisi ya Rais. TAKUKURU iko ndani ya Ofisi ya Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Waheshimiwa Wabunge, mmetuambia tuongeze resources; tuongeze watumishi. Tumeshaajiri watumishi wapya, tunaongeza wengine. Vilevile tumekubaliana na TAKUKURU tutaongeza fedha ya mafunzo. Tunataka tuwe na wapelelezi, waendesha mashitaka wabobezi ili kweli tatizo la rushwa liweze kuzuiwa vizuri na liweze kukomeshwa ndani ya nchi yetu ya Tanzania, ukizingatia tunayo miradi mingi, mikubwa ya kimkakati. Mama anatafuta fedha nyingi sana, zinatakiwa kulindwa na wale wote wanaozikodolea macho washindwe kuzipata na Taifa liweze kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wamezungumzia kazi nzuri iliyofanywa na Mheshimiwa Rais katika ujenzi wa madarasa, ujenzi wa zahanati na ujenzi wa vituo vya afya. Naomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais ameshatuagiza, hatutakubali, naye hayuko tayari miundombinu hiyo ianze kufanya kazi bila kuwa na rasilimali watu, yaani watendaji na watumishi katika miundombinu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshakubaliana na tunatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais, kabla ya mwaka huu wa fedha ni lazima tuwe tumeajiri watumishi, walimu, madaktari, manesi na wahudumu wote katika vituo hivyo vyote ambavyo tumevijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Waheshimiwa Wabunge kaeni tayari, hayo maeneo ye nu na Majimbo yote ni lazima tutekeleze agizo la Mheshimiwa Rais. Tutaleta hao watumishi waanze kufanya kazi katika hivyo vituo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hii imejidhihirisha katika kipindi kifupi sana cha mwaka mmoja; Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa kweli kwenye sekta hii ya rasilimali watu. Rasilimali watu ndio inayotunza rasilimali nyingine zote nchini. Kama siyo rasilimali watu, hata rasilimali nyingine haziwezi kufanya kazi. Katika kipindi kifupi cha mwaka mmoja, ameeleza Mheshimiwa Mbunge Dkt. Alice, ameweza kupandisha madaraja watumishi 190,781, haijapata kutokea. Tumetumia fedha za Kitanzania zaidi ya shilingi bilioni 39 kwa kazi hiyo. Naomba niwahakikishie Watumishi wa Umma, kazi inaendelea, tutaendelea kuwapandisha madaraja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ameweza kufanikiwa kubadilisha kada za watumishi 19,386. Tumetumia zaidi ya shilingi bilioni 1,330. Waheshimiwa Wabunge kazi inaendelea, ni lazima tujenge hiyo rasilimali watu tuliyonayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kulikuwa na kero kubwa ya malimbikizo ya mishahara kwa walimu, manesi na wafanyakazi wengine kwenye kada mbalimbali. Mheshimiwa Rais huyu lazima apongezwe. Kwa muda mfupi sana; na tumekaa muda mrefu kazi hiyo haijafanyika; ameweza kulipa malimbikizo kwa watumishi 65,394 na tumetumia fedha za Kitanzania karibu shilingi bilioni 91,087, kazi inaendelea, hatutaishia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema kazi inaendelea kwa sababu gani? Waheshimiwa Wabunge mwezi huu Februari tayari Mheshimiwa Rais amesema ni lazima tulipe shilingi billioni 32,690 kama malimbikizo ya mishahara kwa watumishi wengine 19,226. Kazi inaendelea, Waheshimiwa Wabunge, haturudi nyuma na tuko imara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge, wamezungumza eneo hilo la ajira mpya. Kama nilivyosema tumeshapokea maelekezo ya Mheshimiwa Rais, tunajipanga. Kabla ya mwaka wa fedha huu haujaisha, ni lazima tutoe ajira mpya nyingine. Tumetoa ajira mpya kwa awamu iliyopita takribani kama watumishi 12,236, lakini tutaajiri watumishi wa kutosha kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha na tutakuja kutoa taarifa hapa Bungeni baada ya kuwa maelekezo yote ya Mheshimiwa Rais tumeshayatekeleza na tumeyaweka sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais anafanya kazi kubwa sana katika kujenga rasilimali watu nchini. Sasa tumekubaliana, pamoja na ujenzi wa rasilimali watu nchini ni lazima pia na watumishi wa Serikali sasa waanze kuwajibika ipasavyo ili kuleta tija katika maendeleo ya Taifa. Ndiyo maana tumeamua kutekeleza agizo la Mheshimiwa Rais la kufanya maboresho ya mfumo wa upimaji wa utendaji wa kazi kwa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa OPRAS ambao uliasisiwa mwaka 2004 tunaufanyia maboresho na kuutengeneza upya. Tunakuja na mifumo miwili; mfumo mmoja utapima utendaji kazi kwa mtumishi mmoja mmoja na mfumo mwingine utapima utendaji wa taasisi zetu zote nchini, tuone taasisi hizi tulizozikasimu kusimamia matamko ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi, Dira ya Maendeleo na Mipango yao ya Kitaasisi katika kuendeleza Taifa letu. Tunataka kuona taasisi hizo zinatekeleza na hazizembei katika kufanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutawapima kila mwaka taasisi moja mpaka nyingine na tutazitangaza nchi nzima ya Tanzania zilizofanya vizuri na ambazo hazifanyi vizuri katika kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunatengeneza mfumo mwingine ambao utatusaidia kufanya tathmini ya hali ya rasilimali watu tuliyonayo nchini. Lazima tufanye manpower audit tujue tumejipangaje? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, nimekuwa nikipokea malalamiko kwamba maeneo ya vijijini hakuna watumishi, maeneo mengine watumishi wamejaa, wako wengi. Tunataka kupata hii picha, hali ikoje? Tumepanga vipi rasilimali watu katika nchi yetu ya Tanzania ili kila mtu alipo aweze kufanya kazi na tuwe na tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Taasisi yetu ya Watumishi Housing. Tumeamua taasisi hiyo sasa ianze kujenga nyumba mpaka kwenye Wilaya mpya na Halmashauri mpya kupunguza tatizo la nyumba... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Jenista malizia.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea ushauri wa e-GA kushughulikia mikopo ya asilimia 10 na tumeshaanza kutengeneza mfumo utakaotusaidia kusimamia hayo vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo ni mengi na kazi inaendelea na Mheshimiwa Rais anatusimamia. Tunaahidi kutekeleza yote kwa faida ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)