Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

Hon. Dr. Joseph Kizito Mhagama

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Madaba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuhusu Shughuli zake kwa Mwaka 2021

MHE. JOSEPH K. MHAGAMA – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuja kuhitimisha hoja. Kwanza kabisa niwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliopata nafasi ya kuchangia hoja hii jumla ya Wabunge sita walichangia hoja hii na niwatambue kwa majina Mheshimiwa Olelekaita Edward, Mheshimiwa Rashid Shangazi, Mheshimiwa Jacqueline Msongozi, Mheshimiwa Salim Shafii, Mheshimiwa Joseph Tadayo na Mheshimiwa Asha Abdulla Juma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia niishukuru Serikali nimepata fursa ya kufafanua hoja mbalimbali lakini pia imepokea maoni na ushauri wa kamati na ipo tayari kwenda kutekeleza na niwatambue Mheshimiwa Dkt. Selemani Jafo Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mheshimiwa George Simbachawene Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Balozi Daktari. Pindi Chana Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu na Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kwa kufafanua baadhi ya hoja na kwa kukubali kuchukua hoja za Kamati ya Katiba na Sheria kwenda kuzifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaielekeza au sijaiomba Serikali kuhusu hizi hoja za kamati katika ujumla wake, kuna mambo kadhaa ambayo ni vizuri kamati ikaweka msisitizo kwa kuzingatia ushauri wa wajumbe wa kamati lakini Wabunge walioweza kuchangia kwenye Bunge lako na hoja ambazo zimetolewa na Mawaziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kuna suala la uwezeshaji vijana, Mheshimiwa Waziri Profesa Joyce Ndalichako ameeleza vizuri kwenye eneo hili lakini ni vizuri tukaiomba Serikali izingatie na kutekeleza mpango kazi mpango mkakati ambao unao wa miaka mitano ambapo Serikali imekubali kutenga bilioni 550 ambapo kila mwaka itatoa bilioni 102 kwa ajili ya vijana 681,000 kuwawezesha katika sekta ya ajira. Tunadhani hili ni jambo muhimu sana Serikali ikalizingatia na hili litakuwa limeboresha sana sana huduma kwa vijana kwa sababu kabla yake tulikuwa tunawahudumia vijana 20,000 tu kwa mwaka lakini sasa tutaweza kuwafikia vijana 136,000 kwa mwaka ni mapinduzi makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pili, kwa kibali chako eneo lingine ambalo limejadiliwa sana na Wabunge humu ndani ni eneo hili la OSHA. Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani amelisema, Mheshimiwa Tadayo lakini Mheshimiwa Asha Abdullah.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Taasisi hii ya OSHA, kwa ridhaa yako niiombe Serikali iichukulie kama miongoni mwa taasisi za mfano, ikibidi taasisi nyingine za Serikali zikajifunze kwenye taasisi hii. OSHA imeweza kuitambulisha Tanzania SADC na sasa ina dawati, kwa sababu inafanya kazi vizuri, lakini pia wana matumizi bora ya fedha wakati wa ujenzi wa jengo lao hapa Dodoma, imefanya vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo haya tumeiomba OSHA ijaribu kuji-align na blue print ili kuona namna gani inaweza kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini. Tulitaka tutambue mchango mkubwa sana wa Mtendaji Mkuu wa taasisi hii. Nirekebishe hoja ya mjumbe wangu mmoja, alisema kwamba Mtendaji Mkuu hajathibitishwa; Mtendaji Mkuu amethibitishwa na anafanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la tatu lilikuwa ni kuhusu Kiwanda cha Viatu na Bidhaa za Ngozi (Kilimanjaro International Leather Industry Company Limited) na hapa pia kumekuwa na mchango wa Mheshimiwa Waziri. Sisi tunaamini kiwanda hiki, kwanza, kina fedha nyingi sana za wananchi kwa kupitia Mfuko wa PSSSF asilimia 86 ziko hapo, lakini kina tija kubwa sana kwa Watanzania wote wanaozunguka Mikoa ya Kilimanjaro, hasa wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iwapo kiwanda hiki kitafanya vizuri kitatoa ajira kubwa sana kwa Watanzania. Zaidi ya Watanzania 3,000 wanategemea kupata ajira ya moja kwa moja na Watanzania 7,000 watapata ajira zisizo za moja kwa moja. Haya ni mapinduzi makubwa sana na ni mchango mkubwa sana kwa maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi letu kama Kamati, waangalie teknolojia tunayotumia kutengeneza viatu hivi ili tuweze kupata teknolojia bora na shindani zaidi katika masoko ya ndani na ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la nne, ukipenda, ni mfumo wa utoaji haki nchini. Miongoni mwa maeneo ambayo tungependa tu-draw attention ya Wabunge ni namna ambavyo Serikali ya awamu ya sita imekusudia kwa dhati kabisa kusimika miguu Dodoma kama Makao Makuu. Ujenzi wa Jengo la Mahakama Kuu ambalo sisi kama Kamati tumetembelea leo ambalo lina three courts katika campus moja, maana yake kuna High Court, Supreme Court na Court of Appeal, ni kielelezo kwamba sasa mihimili yote mitatu ipo Dodoma, Serikali imesimika miguu Dodoma. Hilo tulidhani ni muhimu kulisema. Hili sasa linajibu hoja za wachangiaji walioonesha kwamba tuna changamoto kidogo kuhusu mfumo wa utoaji haki nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa jengo hili na upatikanaji wa watumishi kwenye eneo hili utaongeza kasi ya utekelezaji wa jukumu hili. Niiombe Wizara sasa, tuna upungufu wa watendaji, Wizara ilifanyie kazi hili. Vile vile kuna eneo muhimu la kukamilisha Sera ya Taifa ya Mashtaka, ilitakiwa iwe imekamilika by December, 2021, lakini mpaka sasa bado, pamoja na uharakishaji wa kanuni baada ya sheria kutungwa. Tunaomba Mheshimiwa Waziri ayachukue haya na ayafanyie kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema haya, kwanza niiombe Serikali iyafanyie kazi maoni na mapendekezo yote ya Kamati ya Katiba na Sheria kama yalivyowasilishwa mezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja sasa kwamba Bunge lako lipokee Taarifa ya Kamati na likubali maoni na mapendekezo yote ya Kamati kama yalivyowasilishwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. ELIBARIKI I. KINGU Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.