Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba nielekee moja kwa moja kwenye mchango wangu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote tunafahamu kwamba ili kupata umeme wa uhakika ni muhimu sana kuwekeza kwenye energy mixing. Mwenyezi Mungu ametubariki, kwamba tuna vyanzo vingi sana vya umeme ambavyo vinaweza vikatuwezesha tukapata umeme wa uhakiki ikiwa ni pamoja na umeme wa upepo ambao unapatikana Mkoani Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wote humu ndani tunafahamu kwamba kumekuwa na changamoto kubwa sana ya mwenendo wa hali ya umeme katika Taifa letu. Hata ile target ambayo Wizara wanayo, ya kufikia mwaka 2025 kuwa na megawatt 5,000 litakuwa ni jambo ambalo haliwezekani kwa sababu ya namna tunavyokwenda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme ni kivutio kikubwa sana kwa wawekezaji, lakini kwa namna tunavyokwenda tunapoteza wawekezaji wengi sana kwa sababu hakuna mwekezaji ambaye anaweza kuwekeza kwenye nchi ambayo umeme unakuwa ni wakusua sua na kukatikakatika na kuwaharibia mitambo yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu tunazopewa, kimsingi si sababu tunazotakiwa kuambiwa. Tunaambiwa kwamba mindombinu imechoka. Tuna engineers, tuna graduates wanazunguka wanatafuta ajira, kwa nini mitambo hii inashindwa kufanyiwa maintenance? Hata hivyo, swali lingine la kujiuliza, kama sasa hivi tuna megawatts 1,600 halatu tunashindwa kuifanyia maintenance, vipi lile dude la kule Rufiji la megawatts 2115 likikamilika? Si tutailipua nchi hii?
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa mitambo imezidiwa, kwamba unakuta transformer moja inahudumia watu zaidi ya 130; swali la kujiuliza, wakati vitu hivi vinaagizwa, hivi huko Wizarani hakuna zile specifications kwenye procurement? Kwa sababu kinachofanyika ni kama unachukua mgonjwa ambaye anahitaji oxygen anakuja mgonjwa mwingine unatoa kwa huyu uliyeweka kwanza unaweka kwa mwingine ili kuokoa maisha yake, huyo mwingine, lakini matokeo yake unaweza ukakuta unawapoteza wote kwa wakati mmoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, haya masuala ni muhimu yakafanyiwa kazi. Ni aibu sana; wakati wenzetu, kwa mfano China leo wanajadili, wanahangaika kupambana ili wapate jua ambalo ni artificial,l sisi bado leo tunazungumzia masuala ya transformer kulipuka, hili si sawa. Labda nafikiri hatuoni ukubwa wa tatizo kwa sababu tumekuwa hatufanyi tafiti za mara kwa mara ili kujua ukubwa wa tatizo hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nitakwenda kukuonesha ni kwa namna gani kukatikatika kwa umeme kunaathiri sana Taifa letu kiuchumi. Suala hili la kukatika kwa umeme, kwanza ni suala ambalo si la ajabu sana kwa sababu linatokea nchi nyingi sana na maeneo mbalimbali, tunatofautiana viwango. Kwa nchi za Afrika, nimesoma taarifa za Statistica za mwaka 2018 wamefanya tafiti kwenye nchi 15 wakagundua kwamba Tanzania imeshika nafasi ya tisa kwa mwaka huo, kwamba umeme umekatika mara 670. Nchi inayoongoza ni nchi ya Nigeria, umeme ulikatika mara 4,600, ikifuatiwa na nchi ya Niger 1,400 na nchi ya Congo mara 830. Nchini ambayo inafanya vizuri ni South Africa, ambapo kwa mwaka huo umeme ulikatika mara 50, ikifuatiwa na nchi ya Msumbiji, hapa jirani zetu, umeme ulikatika mara 80, na mwisho Nchi ya Senegal ambayo umeme ulikatika mara 130. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nikajaribu kufuatilia, ni kwa nini South Africa wanafanya vizuri, nilichokuja kugundua, na ninaomba hapo Wizara wanisikilize vizuri ili wajue ni nini cha kufanya. Kule South Africa kuna kitu kina ESKOM ambayo ni sawa na TANESCO ya hapa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ESKOM kwa kipindi kile cha mwaka 2019 waliangalia kwa takriban miaka 10 mfululizo, Nchi ya South Africa ilikuwa inakua kiuchumi chini ya asilimia moja na wakagundua kwamba sababu kubwa ilikuwa ni kukatikatika kwa umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma report ya Council for Scientific and Industrial Research, inaonesha South Africa kwa kipindi kile chote imepoteza takriban Rand bilioni 338. Sasa, kwa Taifa letu hili lazima tujifunze. Ni makosa makubwa sana kufanya makosa ambayo mwenzako alishayafanya nawe ukayarudia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba nijielekeze kukuonesha ni namna gani tunapoteza kama Taifa. Hapa mezani kwangu nina report ya EWURA ya mwaka 2018. Report hii inatoa taarifa za mwaka 2017. Inaonesha hivi: “kwa kipindi cha mwaka 2017 umeme wa Tanzania umekatika mara 2,844”.
Ukichukua takwimu hiyo hapo ni umeme ambao ni planned na unplanned kukatika. Kwa maana nyingine ni kwamba kuna wakati umeme unakatika TANESCO wamepanga na kuna wakati umeme unakatika hata wenyewe TANESCO hawajui. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tukichukua mara 2,844 kule kukatikatika kwa umeme maana yake ni siku 118 umeme ulikatika. Tukienda kwenye hesabu za kawaida kabisa kwenye uchumi unaweza ukaona kwamba ukimchukua mfanyabiashara wa kawaida tu ambaye labda anaingiza laki mbili na kitu kwa siku; yaani let us say kwamba umefanya annual turnover, labda anapata milioni mia moja, ukichukua siku hizi ambazo alikuwa hafanyi kazi maana yake amepoteza takriban milioni 32. Huyo ni mfanyabiashara mmoja. Chukua wafanyabiashara wa Tanzania 100,000 ambao kipato chao ni cha kawaida kabisa. Maana yake kwa mwaka 2017, umepoteza zaidi ya trilioni 3.2. Hii ni mara tatu ya fedha ambazo tumekopeshwa na IMF kwa ajili ya COVID, hiyo trilioni 1.3.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mambo kadhaa ya kushauri hapa. Jambo la kwanza, ni muhimu sasa Serikali itenge fedha ya kutosha kwa ajili ya kufanya maintenance kwenye mitambo ya umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwa sababu ya muda, nahitaji Serikali kupitia Wizara waweke specifications zinazoeleweka kwenye procurements zenu ili wanapokuwa mnaagiza vifaa vya mitambo ya umeme muwe mnaagiza kulingana na uhitaji uliopo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, wataalam wetu waliopo Wizarani wapelekeni wakajifunze. Wanakaa humu ndani wanafanya nini kama mambo haya kuna maeneo mengine wameshafanya makosa haya na wakajifunza? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa mwisho. Ni muda sasa Shirika hili la TANESCO likagawanywa mara tatu, ligawanywe liwe lina kitengo cha kuzalisha, kusafirisha na kitengo cha kusambaza…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. JESCA D. KISHOA: …na nakumbushia ile precaution aliyoitoa Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anajibu maswali, ya kwamba kama TANESCO itagawanywa mara tatu, kuna uwezekano wa kila kampuni kutofanya vizuri na ikasababishia wengine kuharibikiwa; lakini lazima hayo yote yazingatiwe kwa sababu tunaamini kwamba tuna wataalam wa kutosha kwenye nchi hii, watekeleze wajibu wao. Ahsante. (Makofi)