Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza kabisa, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi ya kuchangia. Pia namshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuwakilisha vyema nje ya nchi na kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kwa Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Mheshimiwa Waziri wa Madini, kwa kweli wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kwa moja niende kuchangia kwenye sekta ya madini. Tumeona, na ninawapongeza sana Wizara kwa kuhuisha Shirika letu la STAMICO. STAMICO wanafanya kazi kubwa sana. Ukilinganisha STAMICO ilipokuwa na sasa, unaona maendeleo makubwa sana; na tunaona uendelezaji wa ununuzi wa mitambo kwa ajili ya kusaidia wachimbaji wadogo wadogo umeshika kasi kubwa sana kwa sasa. Niendelee kuwaomba STAMICO pia waendelee kuondoka sasa kwenye maeneo ya uwekezaji mkubwa, waje sasa moja kwa moja kwenye uwekezaji wachimbaji wadogo wadogo katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona sekta ya madini wachimbaji wengi katika nchi hii hawana lesseni. Naomba Wizara, sisi tunaishi katika maeneo ambayo yana wachimbaji, maeneo mengi yamekamatwa na wachimbaji wenye PL na leseni kubwa. Leseni hizi ukiziangalia, bado watu hawazifanyii kazi. Kwa hiyo, naiomba Wizara kwamba wahakikishe wanaenda kuzipitia upya leseni hizi zote na ikiwezekana waweze kuzifuta wazirejeshe kwa wachimbaji wadogo wadogo ili wachimbaji wadogo wadogo waweze kupata leseni za uchimbaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sitarudia aliyosema Mheshimiwa Musukuma kwenye Nishati; sisi tunaotoka kwenye majimbo ya vijijini tumeona kata zetu nyingi na vijiji vyetu vingi bado havina umeme na mabadiliko ya bei yaliyotoka ya shilingi 27; katika maeneo yetu huko kwenye ngazi za mkoa kuna maelekezo yametoka ambapo yanataka maeneo ya vijijini ambapo kuna vituo vya afya, sekondari na shule, basi bei ile ya shilingi 27 inaenda kuondolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kazi anayoifanya Mama Samia Suluhu Hassan katika maeneo yetu haya ni kuweka miundombinu ya vituo vya afya hasa vijijini. Sasa unapochukua kituo cha afya kama kigezo cha kubadilisha bei ya shilingi 27,000/= kwa wananchi wale, maana yake ni kwamba unaenda kuwaumiza wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri yuko hapa, naomba alichukue hili, aende akapitie upya maelekezo hayo, aondoe; kwa sababu vijiji vyetu ukiangalia, center zake zina umbali mrefu wa kilometa moja. Unapochukua kigezo cha pekee kuwa na kituo cha afya ndiyo kigezo cha kuchajiwa 320 siyo sawa. Wananchi wetu bado wanahitaji umeme. Namwomba Mheshimiwa Waziri afute kauli hii, wananchi wetu waweze kupata haki ya umeme katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho niende kwenye suala nzima la barabara na sisi wanashinyanga hasa Mkoa wa Shinyanga tunahitaji huduma ya usafiri wa ndege. Tuna kiwanja chetu Mkoa wa Shinyanga, tumepata ufadhili kati ya Serikali na Benki ya European Investment Bank ya European Investment ambayo imetoa kiasi cha shilingi bilioni tatu na Serikali imetoa shilingi milioni 600 kwa ajili ya ujenzi wa kiwanja cha ndege Mkoa wa Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka ninavyozungumza hivi, Wizara imeshindwa kutoa shilingi milioni 500 tu kwa ajili ya kulipa fidia ili ujenzi uanze. Naomba Wizara, toeni fedha hii shilingi milioni 500 iende ikalipe fidia kwenye eneo lile ili uwanja wa ndege uanze kujengwa na wananchi wa Shinyanga nao wapate huduma ya ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)