Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Lupa
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi ya kuchangia; na nitajielekeza sana kwenye miundombinu. Nitapenda nianze na barabara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa barabara zetu hizi kila mwaka Serikali imekuwa na mipango na imekuwa inatenga fedha kwa ajili ya kuwezesha barabara hizi kuweza kujengwa, lakini kiasi cha fedha kinachotengwa ni kidogo sana ukilinganisha na kazi ambayo inatakiwa kufanywa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, takribani barabara ya kilometa 100, lakini unakuta inatengewa shilingi bilioni mbili kwa mwaka. Sasa hapo tunakaa tunajiuliza: Je, itatuchukua muda gani mpaka barabara hii kukamilika? Mwaka wa fedha uliopita ambao tunaendelea nao, kuna barabara ambazo zimetengewa fedha, lakini ni kiasi kidogo sana na nyingine nyingi hazijaanza kujengwa na ndiyo tunaelekea kumaliza mwaka wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuiombe Serikali iweze kuona namna gani ya kuzikamilisha hizi barabara na kuzitengea fedha za kutosha. Zikitengwa fedha za kutosha walau sasa wananchi wetu nao wataweza kunufaika na kwa muda mfupi wataona barabara zao zinajengwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili, kwenye upande wa barabara, tuishauri Serikali iweze kutenga, kuwa na mipango ya muda mrefu kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Leo hii kila mzungumzaji hapa ni kuhusu habari ya mradi kukwama kwa sababu ya fidia. Sasa inakwama kwa sababu hatuna mipango ya muda mrefu. Sisi mipango yetu ni ya muda mfupi. Tunaishauri Serikali hasa kwenye upande wa miundombinu iweze kuwa na mipango ya muda mrefu; miaka 50 mpaka miaka 100 mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tunazungumza barabara za mzunguko. Tumeona juzi tukisaini hapa Dodoma barabara za mzunguko. Hizi barabara za mzunguko tunataka mipango yake iende kwenye miji na majiji karibu nchi nzima. Kila mkoa huwe na mipango ya miaka 50 au 100 mbele ndiyo tutaweza kutoka hapa tulipo tuweze kwenda mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano, leo kwenye Jiji la Mbeya kuna changamoto ya barabara. Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kutengeneza barabara ya bypass. Sasa badala ya kujenga barabara ya bypass kwanini isiweke mpango kujenga sasa barabara za mzunguko ambazo zitakaa kwa muda mrefu zaidi? Hata kama ujenzi wake hautaanza sasa hivi, lakini tuna imani ndani ya miaka 10, 15, 20 hizi barabara zitaanza kujengwa; na kwa kuwa tayari kunakuwa na hiyo mipango ya muda mrefu ambapo tunakuwa tumeshirikisha majiji kwenye masterplan zao, fedha itakayokuwa inapatikana tutaendelea na ujenzi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ile bypass ya Uyole kwenda kutokezea Songwe, fedha yake imeshatengwa tayari. Sasa badala ya kuanza kujenga bypass, plan iwekwe barabara ya mzunguko ili hii fedha iingie sasa kuanza kujenga barabara ya mzunguko badala ya kujenga barabara ya bypass. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuzungumze sasa pia kwenye upande wa mizani zetu. Leo tunaona magari yanayotoka kuanzia Dar es Salaam kwenda mikoani mpaka nchi jirani, kila kwenye mizani inapopita inatakiwa isimame. Sasa unajiuliza leo, tenki la mafuta linaloondoka Dar es Salaam linaenda Mwanza, Bukoba au nje ya nchi, lina sababu gani ya kupita kila mzani na kupima uzito? Wakati tenki la mafuta likishajazwa kutoka Dar es Salaam likapimwa, lina lita labda 30, haliwezi kupungua njiani mpaka linafika Bukoba au Mwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tuone namna iliyo bora zaidi, hii mizani yetu, baadhi ya magari mengine kama ya matenki yanaweza yasipite kwenye mizani. Hii itaweza kusaidia sana kupunguza foleni. Haya matenki mengi yameshafunga vehicle tracking system, hata ule mfuniko tu ukiugusa, tayari unapiga kelele kule. Maana yake hawezi kufanya chochote njiani hapa. Kwa hiyo, magari kama ya matenki ya mafuta yapime yanapoanza kuondoka na mwisho wa safari ili kurahisisha na kupunguza msongamano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata kwa upande wa mabasi hasa ya safari ndefu; basi linatoka Kigoma, Mbeya au Mwanza; kila kituo ikipita inapima uzito. Inapita Mwanza, inapima uzito; inafika Morogoro, inapima uzito; inafika Mikese, inapima uzito. Sasa akifika Mikese akapima uzito, hana sababu tena ya kupima uzito pale Vigwaza, tunaongeza foleni isiyokuwa na sababu. Kwa hiyo, tuone namna ambavyo Wizara na Serikali itayachukua haya iweze kuyafanyia kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kusema hayo, naunga mkono hoja na ninaomba sana Wizara iyachukulie haya na iweze kuyafanyia kazi. Ahsante sana. (Makofi)