Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi kuweza kuchangia taarifa za Kamati zetu ambazo zimewasilishwa hapo mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipongeze Kamati ya Nishati na Madini inayoongozwa na Mwenyekiti kwa taarifa yao, na ninaunga mkono hoja. Katika kuongezea tu – Taarifa ya Kamati imejitosheleza – ninataka kuzungumzia juu ya usambazaji wa umeme vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, REA imetoa kwa wakandarasi miezi 18 wakamilishe kazi ya kusambaza umeme vijiji vyote Tanzania. Na wakandarasi wamepewa kusambaza ndani ya vijiji vyetu kilometa moja. Sasa wakati mwingine zile kilometa moja kutokana na umbali wa wananchi wetu imesababisha kukuta wananchi wanaunganishiwa watu watano mpaka kumi na inakosa tija kwa ukubwa wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa sababu tunaye Waziri, Mheshimiwa January Makamba, na tunampongeza kwa kazi nzuri na amekuwa mtu wa kufunguka kutoka nje, nimuombe aangalie uwezekano kwenye bajeti inayokuja tuongeze fedha kwa hawa wakandarasi ambao tunao site, waongezewe kilometa nyingine moja ili kuhakikisha kwamba wanasogeza umeme unakuwa eneo kubwa la wananchi kwenye kijiji waweze kupata, kuliko sasa hivi ambapo tunafikisha miundombinu lakini wananchi wengi bado hawapati umeme ambao wanautarajia. Na tunatumia gharama kubwa sana kutengeneza transmission line kupeleka kwenye vijiji. Tunataka tuone impact, wananchi wengi wakipata umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niwaombe sana TANESCO, REA na wadau wote wajipange kuhakikisha kwamba ujazilizi kwenye vile vijiji vyetu unakuwa mkubwa. Hatutarajii kuona wakandarasi wakifanya kazi chini ya kilometa moja walizokuwa nazo, waende zaidi ya kilometa moja. Kwa hiyo niwaombe sana Wizara walisimamie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo ninapenda kuchangia ni bei. Bei ambazo zimetangazwa na TANESCO ni bei ambazo kwa kweli siyo zile ambazo zilikuwa hapo awali. Kwa mfano tunaweza kuzungumza bei ilikuwa kuvuta umeme kwa mjini inawezekana ikawa 170,000 kama umbali wa labda mita 30, lakini sasa hivi imekwenda mpaka 300,000 na ushehe. Tuombe waliangalie hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bei za mijini ibaki ile 170,000, kwa bei za vijiji vyote irudi 27,000. Vijiji vyote. Labda kwenye ile wanaita halmashauri za miji midogo ndiyo unaweza kuongeza bei, lakini kwa vijiji kama vijiji na kata turudishe bei ya shilingi 27,000 kama ilivyokuwa. Na hii itaongeza na itasababisha wananchi wengi waweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uchakavu wa miundombinu yetu; tumeona umeme unakuwa ukikatwa kwa sababu ya kufanya maboresho kwenye miundombinu yetu. Niombe Wizara na TANESCO waangalie. Kwa sababu ziko transmission ambazo zenyewe ni ndefu sana, zinatembea zaidi ya kilometa 200 mpaka 300 pasipo kuwa na substation na hii imekuwa ni sehemu moja wapo ya kusababisha umeme kukatika maeneo mbalimbali ya nchi, achilia mbali huu umeme unaokatwa kwa ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano mdogo naweza nikatoa Wilaya ya Igunga umeme wanachukulia Nzega. Kutoka Nzega mpaka ije Igunga ni zaidi ya kilometa 150 inatembea ndani ya wilaya. Halafu inatoka Igunga inakwenda Wilaya nyingine ya Iyui pasi na kuwepo na substation ndani ya Wilaya ya Igunga, ndani ya Wilaya ya Uyui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe Wizara waangalie ujenzi wa substation ndani ya Wilaya ya Igunga kupunguza umbali ambao umbali huu ukikatika sehemu yoyote miongoni mwa eneo hilo, wilaya zote mbili zinaingia gizani na wanaweza kukaa zaidia ya wiki moja au siku tano wakati wataalam wa TANESCO wakitafuta wapi kumetokea tatizo la kukatika kwa umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hili limekuwa ni tatizo kubwa sana, huo ni mfano tu kwa Wilaya yetu ya Igunga, lakini naamini iko maeneo mengi katika nchi yetu na wilaya mbalimbali. Niombe Wizara waliangalie hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Wizara yetu waendelee kusimamia kwa karibu ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Lakini pia ujenzi wa Rusumo Hydro Power kule Ngara, Mheshimiwa Waziri simamia kwa karibu, tunahitaji kupata umeme kutoka Ngara usaidie Mikoa ya Kagera, Rukwa na Kigoma.

MWENYEKITI: Ahsante.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)