Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kyela
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ALLY A. J. M. JUMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 30 Septemba, 2020, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alikwenda kuomba kura pale Mbeya; na alisema maneno makuu matatu ambayo Wanambeya wanayakumbuka. Jambo la kwanza alisema naomba wanambeya mnichagulie Wabunge wote wa Mkoa wa Mbeya waingie Bungeni, Wanambeya wakafanya, ahsante Wanambeya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili alisema, naomba Wanambeya nichagulieni Tulia, roho yangu itulie. Sasa kama huko alipo anatusikia tunamwambia roho yake itulie sana, Tulia alichaguliwa na sasa ndiyo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia tunataka tumwambie aliyemuachia kazi Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kazi yake anaiendeleza na anaupiga mwingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la tatu alilolisema, alisema nataka niifanye Mbeya iwe ni kitovu cha biashara kwa Nchi za Kusini mwa Afrika na SADC kwa ujumla. Ili mambo haya yatimie, kuna mambo muhimu ni lazima yawepo hasa ya miundombinu; na jambo la kwanza ni uwanja wa Mbeya ambao tayari unaendelea vizuri. tunaishukuru sana Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni barabara; barabara ya TANZAM, barabara muhimu kuliko zote na nataka niseme katika barabara ambazo kwa sasa zimesuswa ni hii barabara. Sasa naiomba Serikali kama kweli lengo lipo vilevile halijabadilika, ni lazima sasa Serikali yetu ihakikishe inakwenda kuijenga barabara hii kwa viwango sahihi. Sasa hivi ajali za magari zinatokea kila sehemu, ukitoka Mbeya kilomita 70 ni kila siku kuna ajali, barabara imeharibika na hii barabara ndiyo inayounganisha SADC, ndiyo inayounganisha magari yote na mizigo yote inayokwenda Malawi, Zambia, Congo mpaka Zimbambwe. Kuisusia barabara hii ni kuisusa Tanzania kiuchumi na kuharibu bandari zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapofika Mbeya, ukifika pale katikati hapapitiki, barabara haipitiki, pamejaa vibajaji, daladala na kadhalika. Tunaomba Serikali sasa ichukue hatua za haraka ijenge barabara ile kwa njia mbili nina uhakika itatusaidia wakati huo tunafikiria kujenga bypass. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, ili kuhakikisha ile ndogo ya Mheshimiwa Rais inatimia ni lazima TAZARA ifanye kazi. Naomba katika jambo la TAZARA Bunge hili livae meno ya chuma, tuache kuvaa meno ya plastiki kwa sasa. Naomba hili suala siyo la mchezo, safari hii tumekubaliana na Zambia tubadilishe mikataba, mkataba uwe mzuri, lakini tutunge sheria ya maana. Upande wa Tanzania mambo yamekwenda vizuri, leo naambiwa eti Zambia hawana Bodi ya Wakurugenzi mpaka watakapounda Bodi ya Wakurugenzi ndipo hizo Kanuni na Sheria zipitishwe, tunakwenda wapi? Ni lazima sasa tutoe tamko lenye maana. Naiomba Serikali; katika hili Serikali tuwe wakali, mkataba huu unaiangusha nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, ili lengo hili litimie ni lazima Mbeya kuwe na Bandari ya Nchi kavu pale Inyala. Vyombo vyote vya usafiri vikiishia pale Inyala na nchi za SADC kule Kusini zikachukua mizigo pale uchumi huu utakwenda na Serikali itaona bandari yetu itakavyofanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi)