Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, nami niungane na wachangiaji wengine kukupongeza kwa kuchaguliwa kwa kura nyingi sana. Naipongeza sana Kamati ya PAC na LAAC kwa taarifa ambayo wametuletea hapa inayoleta taswira kwa nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo ninaomba niishauri Serikali jambo moja. Serikali inapotaka kuingia kwenye uanzishwaji wa mifumo kwa ajili ya ukusanyaji wa fedha, naomba ifanye upembuzi yakinifu ili mifumo inayotengenezwa ije kuwa na tija kwa ajili ya Watanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Bandari mwaka 2010 iliingia mkataba wa miaka minne na Softech, mpaka 2014, kwa ajili ya kutengeneza mfumo wa ukusanyaji wa fedha. Mfumo huu ulikuwa unachukua gharama ya shilingi milioni 694, lakini mpaka kufikia mwaka 2014 mfumo haufanyi kazi na tayari Mkandarasi alikuwa amelipwa shilingi milioni 600 sawa na 87%. Inasikitisha kwa sababu fedha hizi ni za Watanzania, lakini mradi ule haukufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa Softech waliongezwa mkataba wa thamani ya shilingi milioni 55 kwa ajili ya kufundisha watumishi wa TPA ambapo mfumo haukufanya kazi. Pamoja na hayo, walilipwa shilngi milioni 55 zote na katika zile shilingi milioni 55 zilitakiwa kulipwa kwenye mkataba wa awali wa shilingi milioni 694. Serikali ikaingia hasara ya shilingi milioni 600 ya kwanza na ikaingia hasara ya shilingi milioni 55 ya pili. Hizi fedha ni za walipa kodi.

Mheshimiwa Spika, bado haitoshi, mwaka 2015/2016 kampuni ya 23rd Century System iliingia mkataba na Serikali ya kutengeneza mfumo pale TPA ambao ungegharimu shilingi bilioni 14, lakini mpaka mwaka 2019 mfumo huu haufanyi kazi, Serikali imelipa shilingi bilioni tisa; hasara kwa Serikali na hizi ni fedha za walipa kodi. Bado haitoshi fedha zililipwa shilingi bilioni tisa, lakini Mkandarasi hakulipa kodi ya zuio (Withholding Tax), akatoroka na fedha za wananchi sawa na shilingi milioni 874. Ni lazima Serikali ichukue tahadhari inapoanzisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bado haikutosha kampuni ya SAP mwaka 2020 ikaajiriwa; kazi yake ni kuangalia kama huyu 23rd Century System Limited alifanya kazi ambayo ilistahili kulipwa zile fedha. Naye akalipwa dola za Kimarekani 433,000 sawa na shilingi milioni 874. Hizi ni fedha za walipa kodi na bado mifumo haikufanya kazi. Tunavyozungumza sasa hivi, ule mfumo haukufanya kazi tena pale TPA na fedha za walipa kodi zililipwa. Katika mifumo hii ni shilingi bilioni 17 zilitumika na mfumo haukufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, siyo TPA peke yake, ukienda pale GPSA wamenunua mfumo wa shilingi bilioni 1,087, sasa wamekuja kugundua ule mfumo hautoi yale mahitaji ambayo walikuwa wanayahitaji. Wamekuja kugundua ule mfumo hautawasaidia tena. Sasa wameshindwa kuutumia ule mfumo na fedha za Serikali zililipwa shilingi bilioni 1,087. Wameandika kibali kwenda Wizara ya Fedha, wabadilishe watumie mfumo mwingine na Wizara ya Fedha imewakubalia na hasara tayari imepatikana katika fedha za walipa kodi. (Makofi)

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. HUMPHREY H. POLEPOLE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mzungumzaji anateremsha taarifa muhimu sana, nilitaka kumpa taarifa kwamba TANESCO mwaka jana 2021 mwishoni wameingia mkataba na kampuni ya kutoka India kwa zaidi ya shilingi bilioni 69 kwa ajili ya mifumo ya TEHAMA na watu wengi tunajiuliza kama uwezo huo wa kampuni kutoka India haupo nchini Tanzania licha ya kwamba mifumo mingine ya Kiserikali inatengenezwa hapa Tanzania?

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Simon Lusengekile unapokea taarifa hiyo.

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, ninapokea taarifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tuone ni namna gani Serikali inaingia hasara katika mifumo ambayo haina tija na haileti matokeo chanya kwa Taifa. Wahasibu wanaita this is nugatory expenditure. The Government incur some expense that cannot generate economic benefit. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali kuchukua hatua za haraka kwa wale wote ambao wamesababisha hasara kwa Taifa. Watumishi ambao wapo ofisini wamesababisha hasara kwa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, tayari ameshaanza kuchukua hatua na kumwelekeza DG wa Bandari kuhakikisha kwamba wafanyakazi waliopo pale waliosababisha hasara hii wanachukuliwa hatua za haraka.

Mheshimiwa Spika, ninaishauri Serikali ichukue hatua kwa makampuni haya ambayo yalilipwa fedha nyingi na Serikali shilingi bilioni 17 na mfumo haukuleta tija ikiwepo na hii 23rd Century System Limited iweze kulipa fedha za TRA ambayo ilikuwa ni Withholding Tax, shilingi milioni 877. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo naomba pia nichangie kidogo kuhusu kiwanda cha sukari pale Mbigiri. Serikali iliingia mkataba wa kusimika kiwanda cha sukari cha kisasa pale Mbigiri, lakini mpaka sasa tunapozungumza, kiwanda kile hakijawahi kusimikwa na Serikali imepata hasara ya fedha kwa sababu walilima miwa wakijua kwamba kiwanda kitawahi kuja, miwa ile imeharibika, tayari Serikali imepata hasara ya zaidi ya shilingi milioni 300. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haitoshi…

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nampa taarifa jirani yangu wa Busega kwa mchango wake mzuri. Siyo Serikali tu, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imelazimishwa kuwekezwa hapo, PSSSF miaka mitatu imetengeneza hasara ya shilingi bilioni 11; na ukiuliza sababu, Serikali haijapeleka mashine.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Simon Lusengekile, unapokea taarifa hiyo?

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Spika, pale Mbigiri NSSF ina 96% na Magereza wana 4%, tunazidi kudidimiza taasisi zetu. Waliingia mkataba wa kununua miwa ya outgrowers; wakulima wa mazingira ya pale. Wakulima wamekopa fedha benki kwa ajili ya kuwekeza kwenye kilimo cha miwa wakijua kwamba baada ya kiwanda kuja watauza ile miwa. Kiwanda hakijasimikwa mpaka sasa hivi, wananchi wanateseka, wanashindwa kulipa mikopo kwa sababu kiwanda hakijapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba Wizara husika sasa iharakishe kusimika kiwanda hiki ili kiweze kuleta tija kwa Watanzania. Ninaamini kitaleta ajira nyingi kwa Watanzania.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, naunga mkono hoja. (Makofi)