Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

Hon. Paschal Katambi Patrobas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Shinyanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021 na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2021

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA, AJIRA NA WENYE ULEMAVU): Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwanza nikupongeze kwa sababu baada ya wewe kuchaguliwa kwa kishindo na Chama cha Mapinduzi, lakini pia kwa kuidhinishwa na Bunge hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja katika eneo la hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge. Nizungumzie kuhusu suala la Kiwanda cha Mbigiri, niwaambie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba katika uwekezaji ambao unafanywa na Serikali katika mifuko hii kuna sera ambayo inaongoza uwekezaji wa Mifuko lakini pia tunayo sera ya uwekezaji ambayo ndiyo msimamizi mkuu wa Mifuko hii. Miongozo kabla ya uwekezaji ni lazima ipitishwe na Benki Kuu ya Tanzania na taratibu zinaelezwa na nini kinafanyika kabla ya uwekezaji. Mwongozo unaeleza lazima ufanyike utafiti na upembuzi ili kubaini au kugundua kama kuna economic viability yaani kuangalia faida katika uwekezaji huo.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili linaangaliwa ni katika sasa kufanya uamuzi wa kwamba uwekezaji ufanyike au usifanyike na kwa kuzingatia required rate of return ambayo inaelezwa kwenye mwongozo huo na kwa mujibu wa maelekezo mazuri yanayofanyika na Benki Kuu ya Tanzania na kigezo cha kufanya hivyo kama itaonekana kutakuwa na tija ndipo uwekezaji unaweza ukaendelea kwa kuzingatia pia miongozo ambayo inatolewa na Social Security Investment Guidelines.

Mheshimiwa Spika, sasa Social Security Investment Guidelines ndiyo zingatio la usimamizi wa Serikali katika kuhakikisha chochote kinachowekezwa kinachotoka katika Mifuko hii kiende kuleta tija. Kwa kweli niishukuru sana Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, ya Awamu ya Sita, amekuwa akitupa miongozo kwa wakati wote kuweza kuhakikisha kwamba, tunayatekeleza majukumu kama jinsi ambavyo ilikusudiwa. Nini kilitokea katika kiwanda hiki cha Mbigiri? Changamoto zilizojitokeza baada ya tafiti hizo na kuruhusiwa kuanza, kiwanda hiki ndani ya miezi 16 kilikuwa tayari kilishaanza kufanyakazi by mwaka jana mwezi Agosti kingekuwa kimekamilika.

Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu sote ni jambo la janga la dunia nzima, baada ya kuanza procurement procedures zilifika zikachelewa kwa sababu ya uwepo wa janga la Covid mashine zikachelewa kuingia na kufikia mwezi Agosti na sasa hivi tunavyozungumza tayari mashine zimekwisha kuingia. Kwa hiyo tunasubiri by mwezi Agosti mwaka huu pengine tayari waende kwenye hatua ya mobilization na installation kwenye eneo hilo la kiwanda.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo mkataba huu tumeendelea kuhakikisha kwamba tunasimamia ili uweze kutekelezwa kwa kadri agizo na ni siku tatu zilizopita Mheshimiwa Waziri wangu Profesa Ndalichako alikuwa kwenye kiwanda hicho na kuangalia tija namna gani Serikali itaenda kupata faida zaidi. Kwa hiyo tunalisimamia kwa karibu zaidi.

Mheshimiwa Spika, hoja ya pili ilikuwa ni kuhusiana na hasara ambayo wakulima waliipata katika kilimo walichokifanya cha miwa. Sambamba na hilo tukumbuke Serikali pia nayo ililima mashamba, miwa hii yote kwa pamoja kwa maelekezo mazuri ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan na uongozi wetu katika Wizara na usimamizi wa Mheshimiwa Waziri Mkuu, ilibidi Serikali ifanye uamuzi wa kutafuta soko na kwenda kuuza katika viwanda vingine na miwa hii ilinunuliwa na faida ilipatikana zaidi ya bilioni moja. Kwa hiyo ilikuwa ni katika hatua ya kupunguza hasara ambayo ilijitokeza kutokana na changamoto tulizozipata.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni kuhusu madeni ya Serikali katika Mifuko. Katika hili turudi katika hoja za CAG, tulizichukua hoja 12 za Ofisi ya CAG na tayari Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri Mkuu wamekwisha kuanza utekelezaji wake na moja ya utekelezaji wa hoja hizo 12 za CAG, tayari zaidi ya shilingi trilioni mbili zimelipwa kwenye Mfuko wa PSSSF na Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan katika kupitia hiyo cash bond.

Mheshimiwa Spika, pia kulikuwa kuna hoja nyingine kwa kadri ya maelekezo ambayo umetupa kwamba tujielekeze katika hoja. Suala la fedha ambazo Ofisi ya Waziri Mkuu zinazosemekana bilioni 56 zinazodaiwa kwa kile alichokisema Mheshimiwa Mbunge kwamba zinadaiwa. Ni kweli fedha hizo zilichukuliwa kwa utaratibu wa kuokoa hasara ambayo kubwa walikuwa wanaenda kuipata wakulima. Ndipo Serikali ikalazimika kuchukua hatua za makusudi kuweza kuhakikisha wakulima hawa mazao yao hasa yale mahindi yananunuliwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika, utaratibu kama jinsi ambavyo mikopo mingine inalipwa, Serikali inaendelea kulipa deni hili na Mheshimiwa Aida Khenani atakuwa shahidi hata yeye mwenyewe kuna maeneo ambayo pengine atakuwa na mkopo na mkopo unategemeana na masharti na vigezo. Kwa hiyo huwezi ukalipa kwa mkupuo, kwa hiyo hili suala tayari Serikali inalipa na niwaondoe shaka Serikali ya Awamu ya Sita katika kila hoja zinazotolewa na Wabunge na hoja zinazotolewa na Kamati za Bunge, tunazitekeleza usiku na mchana kuhakikisha kwamba maagizo ya Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan yanatimizwa. Ahsante sana. (Makofi)