Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi. Ninapenda kutumia nafasi hii kuipongeza Serikali pamoja na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Masauni Naibu wake na timu yake nzima ambao tumekutana kwenye Kamati kwa takriban wiki nzima kupitia Azimio hili la Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi za Afrika kuzuia na kupambana na ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekitti, lakini pia nitumie nafasi hii kuwapongeza wajumbe wenzangu wa Kamati, kama alivyosema Mheshimiwa Mwenyekiti wetu Vita Kawawa, kwa utulivu na umakini wa hali ya juu katika kuhakikisha kwamba tunafikia siku hii ya leo kuwasilisha hili azimio humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ilivyo kwenye masuala mengi mbalimbali kimataifa, jambo la kupambana na ugaidi ni jambo ambalo sisi kama Taifa na kama nchi ambayo hatuishi katika kisiwa tunapaswa kushirikiana katika kukabiliana na uhalifu mbalimbali ukiwemo vitendo hivi vya kigaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Taifa na kwa jinsi ambavyo vitendo vya ugaidi vyenyewe jinsi vilivyo; kwanza mpambano wa kigaidi si kama vita ya kawaida ambayo pengine nchi A inaweza ikawa inapambana na nchi B, au kikundi cha mataifa kadhaa kikawa kinapambana na kikundi cha mataifa kadhaa, kwamba kitu ambacho kinaonekana. Tatizo la ugaidi ni vita ambayo adui kwanza humuoni na wala hujui yuko wapi na wala hujui anaishi wapi. Kwa hiyo, kwa ugumu huo maana yake ni muhimu sana kufanya jambo hili ili kukabiliana nalo katika namna ya kushirikiana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Taifa tumekuwa tukishiriki katika shughuli za ulinzi wa amani chini ya uratibu wa Umoja wa Mataifa na wakati mwingine chini ya utaratibu wa Jumuiya zetu za kikanda kama vile SADC. Kwa hiyo hata katika jambo hili ni muhimu sana kuhakikisha kwamba tunaendeleza utamaduni wetu wa kushirikiana na wengine duniani na kikanda katika muktadha mzima wa kuhakikisha kwamba tunakabiliana ipasavyo si tu na vitendo lakini ikibidi hata na viashiria vya masuala ya kigaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika maeneo mbalimbali chini ya utaratibu wa Umoja wa Mataifa au Umoja wa Kikanda kama nilivyosema tumeshiriki katika masuala ya ulinzi wa amani, ama katika eneo letu hili la maziwa yetu makuu ama hata katika nchi mbalimbali kama huko Lebanon nchi za Afrika za Kati, kote huko kuna majeshi yetu ambayo yanashiriki katika ulinzi wa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi zote ni taratibu ambazo tunaziweka kimataifa ili kukabiliana na matukio au na vitendo mbalimbali ambavyo vinaweza vikahatarisha usalama si wa nchi yetu tu bali usalama wa eneo la kikanda na usalama wa dunia katika ujumla wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuridhia azimio hili la Bunge na Itifaki hii, sisi sasa pia tunaweza tukanufaika. Kama nilivyosema, suala lenyewe hili ni gumu kwa sababu napambana na adui ambaye kwanza umuoni na hujui yuko wapi. Kwa hiyo miongoni mwa faida ambazo tutanufaika nazo ni pamoja na ku-share taarifa. Kwa mfano tunacho hiki kituo cha kanzidata ambacho kipo pale Algeria, maana yake tukiwa sehemu ya hii Itifaki, sehemu ya hili azimio kuna taarifa sisi kama taifa tunaweza tukapewa ambazo tukazitumia katika kuhakikisha kwamba tunakabiliana si tu na vitendo lakini hata na viashiria vya ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia, kwa wanasheria wanaweza wakanisaidia; katika sheria, hasa sheria za kimataifa, kuna kitu kinaitwa extradition ambapo ni makubaliano baina ya nchi na nchi kubadilishana wafungwa. Lakini kupitia suala hili na azimio hili bado tunaweza kubadilishana wahalifu, tukawa na utaratibu maalum ambao unaweza kutuwezesha sisi kama taifa kubadilishana na wahalifu ambao kwa namna moja ama nyingine wanashiriki katika vitendo au kwa namna moja au nyingine kuna viashiria kutokana na watu wao na masuala ya kigaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia taifa letu tumekuwa tukifanya juhudi kubwa za kujenga uchumi wa nchi yetu, tunajenga miundombinu kama vile viwanja vya ndege; na kwa mfano sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa SGR. Hii ni miundombinu ambayo kwa namna moja au nyingine inasaidia katika kuvutia wawekezaji, inasaidia katika katika kuhakikisha kwamba tunapanua shughuli zetu za kiuchumi na kukuza biashara baina yetu na mataifa mengine, pia na baina yetu na majirani. Sasa, ili uweze kuwavutia wawekezaji, pamoja na miundombinu hii kama ya ujenzi wa barababara, kama nilivyosema ujenzi wa SGR, miundombinu ya nishati kama vile bwawa la umeme; lakini pia mwekezaji ili aje anataka awe na uhakika na usalama katika ile nchi au taifa analoenda kujiwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa moja wapo ya mambo ambayo ni muhimu kama taifa ni pamoja na kuhakikisha tuishi kama kisiwa, tunashiriki katika itifaki hizi ambazo ni za kimataifa au taratibu mbalimbali za kikanda. Kwa hiyo wanaangalia katika list na kuona kwamba hawa kumbe ni washirki katika jumuiya ya kimataifa na ni washiriki katika kikanda kuhakikisha kwamba kama taifa lao wanakuwa salama. Si wao tu lakini pia na majirani zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika suala la utalii, kama nilivyosema tunaendelea na ujenzi wa miundombinu ya viwanja vya ndege. Kama sisi kule Iringa tunaendelea na ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Iringa. Pia hivi karibuni tutaanza ujenzi wa barabara kutoka Iringa kwenda Ruaha National Park. Hivi vyote kwa namna moja au nyingine vitavutia watalii, pamoja na kutumia fursa ya kutangaza ile filamu ya Royal Tour ambayo inavutia watalii. Sasa, ili nao, watalii, waweze kuja katika nchi yetu yapo mambo ambayo ni ya msingi ambayo wanatazama. Wanaangalia, je, Tanzania kama Taifa inashirikiana kimataifa kwa kiwango gani na kikanda kwa kiwango gani katika kuhakikisha kwamba inakuwa tu si yenyewe salama lakini salama na watu na majirani wanaotuzunguka?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo mtu anapoangalia katika check list anaona kama taifa tumeridhia azimio kama hili, kama taifa tunashirikiana na jumuiya za kimataifa katika kuhakikisha usalama wa taifa letu na majirani kwa hiyo inampa yule mtu confidence ya kuja kutembelea kama mtalii, lakini pia nakuja Tanzania kama mwekezaji. Kwa hiyo, itoshe kusema kwamba, jambo hili ni muhimu na limeletwa wakati ambao ni sahihi, na kama kamati ambavyo imeshauri, na ile sheria yetu ya kukabiliana na ugaidi pia tuifanyie mabadiliko ili iweze kuendana na suala hili kama ambavyo tumesema iwe combat and abrogation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, nawashukuru sana. (Makofi)