Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

Hon. Zahor Mohamed Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili nami niwe sehemu ya wachangiaji katika Muswada huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, naomba niseme kwamba amani tuliyonayo Watanzania ni mtaji, amani tuliyonayo ndiyo kivutio cha wawekezaji, na amani tuliyonayo ndiyo msalaba tulionao na tunatakiwa kuutunza kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu gani? Uhalifu na ugaidi ni vitu vinavyoendana. Tofauti yetu hapa ni maana ya neno ugaidi. Ila ugaidi ni uhalifu uliokithiri ambao unaweza kutoka nchi moja kwenda nyingine. Yuko mwenzetu amesema hapa kwamba vitendo vya kigaidi vinaweza vikapangwa katika nchi nyingine lakini vikatekelezwa katika nchi nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ni nini hapa? Ni kwamba amani tuliyonayo kama Watanzania haikuja kwa bahati mbaya. Amani tuliyonayo haikai hapa kwa bahati mbaya, ipo kwa sababu kama Taifa tumeamua; ipo kwa sababu Taifa linawekeza fedha nyingi kwa ajili ya kulinda amani ndani na nje ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili tuweze kuendelea na ili tuweze ku- maintain amani tuliyonayo, sisi kama Watanzania, majirani zetu na dunia yetu, ugaidi ni jambo linalosomewa. Huwezi ukaibuka tu leo ukawa gaidi. Kuna vitendo vya ku-recruit, ku-train na ku-equip. Lazima uwezeshwe uwe gaidi, huwezi ukaamka leo ukasema mimi nataka kuwa gaidi, haiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mambo haya hayaji kwa bahati mbaya. Sisi kama Watanzania tuna mtihani mkubwa kwa sababu amani tuliyonayo wenzetu inawapa matatizo na wako katika kutujaribu kila siku, kwamba kwa nini Tanzania iendelee kubaki kuwa na amani? Kwa nini wawekezaji waende Tanzania? Kwa nini tusiharibu image ya Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ombi langu kwa Waheshimiwa Wabunge, ni kwamba itifaki hii, pamoja na kuchelewa kwake, lakini sasa ni wakati mzuri kwa sababu tumeichakata kwa kipindi kirefu, tumeangalia pay turn ya matatizo. Maana yake, ugaidi, kama alivyosema mwenzangu, unaweza kupangwa eneo lingine lakini ukaja ukatekelezwa kwenye nchi nyingine. Sisi kama Watanzania kwa sababu Tanzania siyo kisiwa, na kwa sababu tunaweza kuondoa tatizo moja kulipeleka eneo lingine, Tanzania ni eneo ambalo kila mtu ametazama na angependa kutujaribu kuona kwamba kwa kweli tunataka tuvunje historia ya Tanzania kwamba ni eneo la amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenu; kwanza, turidhie itifaki hii kwa sababu Tanzania siyo kisiwa, Tanzania ni eneo ambalo tunaishi na wenzetu na walishafanya ratification, nasi kama sisi tunahitaji kuwa sehemu ya dunia. Kwa sababu matukio haya pamoja na kwamba yalitokea muda mrefu kwenye maeneo mengi, lakini bado yanaendelea kwenye nchi za wenzetu, nchi za jirani zinaendelea. Nasi tumekuwa tumo kwenye majaribio. Majaribio haya ni viashiria vya kwamba bado ugaidi unaendelea na sisi kama Taifa tunahitaji taaluma, nyenzo na kuendelea kuji-equip ili tuhakikishe kwamba tunaendelea kubaki kuwa salama. Kwa sababu wawekezaji kila siku wanatafuta wapi wataweka fedha zao ambapo pana amani? Bila ya hivyo tutaendelea kuwapoteza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo niwape mfano. Tanzania inasifika baada ya Royal Tour. Royal Tour hii haikuja kwa bahati mbaya, wala siyo bahati mbaya, ipo kwa sababu vyombo vyetu viko imara, havidharau taarifa na vinaendelea kutafuta taarifa kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwetu ni kwamba tusidhani kwamba tumechelewa, hatujachelewa, lakini ni wakati muafaka ili sasa tuweze kuingia kama Taifa kwenye mataifa mengine tuweze kupata kila ambacho kinastahili kupatikana ili tuweze kufanya zoezi hili lifanyike vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hiyo, hatuingii eti kwa sababu tu tumeingia. Tumejiridhisha vya kutosha kama Kamati, tumejiridhisha kama Taifa kwamba sasa ni kipindi muafaka kwa sababu matukio yanayoonesha ni ishara na viashiria kwamba bado tunawindwa kama Tanzania, bado tunayo nafasi ya kuungana na wenzetu. Vile vile hatusubiri tatizo litokee. Ndiyo maana sheria zetu zinasema kwamba tuna-prevent kwanza halafu ndiyo runa-combat.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenu ni kwamba turidhie itifaki hii ili tuweze kuendana na tuweze kutumia facilities zote zilizoko dunia nzima kuweza kupata taarifa na kuzitumia kwa ajili ya kushughuika na hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo hiyo, wanaokuwa-recruited ni vijana wetu, watoto wetu wadogo ambao wanaghilibiwa ili kuweza kuingia wakioneshwa kwamba hapa kuja jambo haliko sawa, kwa hiyo tuingie. Kwa hiyo, naomba; mwenzangu amesema hapa, na Mheshimiwa Waziri amesema, kwamba mara nyingi hili linatakiwa lianze ulinzi kwenye nyumba zetu, familia zetu, mitaa yetu, ili kila mmoja aweze kufahamika tabia zake na nyendo zake, itusaidie kuendelea kulinda heshima yetu kama Taifa, itusaidie kutulinda sisi na kuhakikisha kwamba na wenzetu wanaendelea kuwa na amani na imani kwamba Tanzania bado ni nchi iliyo salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile na watoto wetu, kwa sababu hili siyo kwamba tumelizungumza kama Kamati kwamba hatuna ushahidi. Kama mtakumbuka miaka michache nyuma, watoto waliotoka Uingereza na Mataifa mengine, wamevutika tu na neno ugaidi, wamekuwa recruited wamekwenda kufunzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba kwamba ili tuweze kuwazuia watoto wetu wasiingie katika mkumbo huu wa kughilibiwa na wakadhani kwamba hiki ni kitendo cha fahari, siyo fahari. Ugaidi ni tendo la kudhalilisha utu wa mtu na sisi kama Bunge tunayo nafasi na wajibu wa kuhakikisha kwamba tunazuia vitendo hivi visifundishwe kwa watoto wetu kwa kuwa-recruit lakini kuwapeleka halafu wakaja wakatudhuru sisi au wakadhuru binadamu wengine wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge, nawaomba sana kwamba hili tulichukue, turidhie ili tuendelee kuwa Taifa lenye salama na amani ili tuendelee kubaki kama Tanzania ambayo tumeirithi na sisi tuwarithishe vizazi vyetu ikiwa bado ni Taifa lililo salama. Ninawaomba sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudie kusema kwamba amani tuliyonayo ndiyo mtaji, amani tuliyonayo ndiyo fahari tuliyonayo ambayo dunia nzima inaihitaji na tungependa kama Kamati, kama Bunge, tuendelee kuwa Taifa lenye utulivu na kila mtu akiliheshimu akijua kwamba hapa ndipo eneo la kukimbilia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuliko hayo, nimezungumza hapa nyuma kidogo kwamba Royal Tour haikuja kwa bahati mbaya. Royal Tour imetufungulia mambo mengi sana lakini moja kubwa zaidi ni kuongeza imani ya watalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwape kisa kimoja. Watalii ni kama njiwa. Kama wapo wenzangu hapa waliowahi kufuga njiwa; njiwa kwa kawaida hata ukimwaga mchele anakuja mmoja mmoja, wa pili, wa tatu, wanakuwa wengi; lakini ukidondosha jiwe, wanaondoka wote kwa wakati mmoja. Kwa hiyo, ombi langu, tusidhani kwamba jambo hili linawafurahisha wote. Hili linatufurahisha sisi kama Watanzania lakini tumepeleka au linaonekana ni tatizo kwa competitors wetu kwenye mambo ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana litusaidie kuhakikisha kwamba tunalinda Royal Tour yetu ya kwanza na ya pili na ya tatu itakayokuja kwa kuhakikisha kwamba tunaendeleza amani, na dunia iendelee kuamini kwamba bado Tanzania ni eneo salama, utalii uendelee na sisi tuweze kupata yale ambayo Taifa limejipangia ili kufikia malengo yake kwenye suala la utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa heshima sana, naomba niunge mkono hoja, lakini naomba turidhie kwa faida yetu kama Bunge, kama Taifa, kama East Africa, Afrika na jumuiya za Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)