Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Umoja wa Nchi Huru za Afrika wa Kuzuia na Kupambana na Ugaidi ya Mwaka 2004

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichukue nafasi hii kwa dhati niipongeze Serikali kwa kuja na Azimio la Kuridhia Itifaki ya Mkataba wa Kupambana na Ugaidi. Zaidi jambo hili linatoka kwa pendekezo na muktadha kutoka Umoja wa Mataifa kwamba nchi katika Kanda mbalimbali na dunia kwa pamoja tuweze kushirikiana kupambana na ugaidi. Bahati mbaya, dhima na dhana hasa ya ugaidi bado inatofautiana kutoka eneo moja kwenda eneo lingine. Vilevile bado kuna ulegevu mkubwa wa Umoja wa Mataifa wenyewe kutoa definition kamili ya nini maana ya ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ugaidi umekuwa unafadhiliwa na baadhi ya mataifa makubwa waziwazi na UN ipo. Ugaidi umekuwa kama unataka kuua mbwa mpe jina baya, baadhi ya nchi zimejaribu kutengeneza ugaidi kwenda kudhuru nchi zingine. Siwezi kuzitaja nchi hizo lakini ipo sponsored terror groups na jambo hili linatokana na mtofautiano wa kiitikadi kwamba huyu ni gaidi, kwa hiyo anaweza kuwa gaidi kwa mtizamo wa mwenzangu lakini kwangu vilevile asiwe gaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona katika historia wakati wa mapambano ya Kusini mwa Afrika, kikundi cha Nelson Mandela na Wapigania Uhuru wote wa South Africa waliitwa magaidi. Jambo hili bado linaendelea hata duniani, Mwalimu Nyerere alikwenda ziara Iraq mwaka 1979, wakati wanatoa ile inaitwa International Communiqué sasa maazimio ya pamoja na Iraq; Rais Sadam Hussein akataka waweke na kipengele kwamba kwa pamoja wamekubaliana kupinga uonevu unaofanyika kwa Wamarekani Weusi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere alikataa akasema we don’t subscribe to that conflict; japo kuwa sisi ni PAN Africanism. Kwa hiyo na sisi tunapoingia katika muktadha huu wa kupambana na ugaidi lazima kuwa na maeneo tusi-subscribe; lazima tuseme sawa lakini hili bado haturidhii kama ule ni ugaidi. Tukienda hivyo, tutaondoa ile dhana ya sisi kutumiwa, kwa maana ya kwamba mataifa makubwa na mengine yanayotufadhili katika mambo mbalimbali yanaweza yakatumia mwanya huu sisi kuingizwa kwenye migogoro ambayo haituhusu na kwa sababu tumeingia katika Itifaki hii, basi tutaonekana kwamba na sisi tuweze kuwa pamoja katika migogoro ambayo wanayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wamesema kwa maana ya kanzidata ambayo ipo Algeria kwenye security na kwa maana ya ku-share information ni jambo la msingi; lakini siyo kila information utataka uitumie. Kwa hiyo, naiomba Serikali katika jambo hilo kwamba ni lazima tuseme kuna maeneo tunakubaliana kwamba huu ni ugaidi na kuna maeneo mengine lazima tukatae tuseme huu siyo ugaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashindwa kutaja baadhi ya nchi na baadhi ya vikundi, lakini jambo hili linaendelea. Ukienda nchi kama Qatar kuna vikundi vipo pale lakini nchi zingine wanasema wale ni magaidi; lakini wamewa-host wanakaa pale. Ukienda Palestine inachukuliwa ni magaidi, lakini kuna nchi hata sisi wenyewe tunasema Wapalestine siyo magaidi. Kwa hiyo, muktadha huu usitupeleke moja kwa moja katika Azimio hili, sasa katika context ya Afrika na sisi hata Kikanda bado kuna maeneo tunakubaliana hatukubaliani. Serikali zetu lazima tuchukue wajibu kwamba tusitumie mabavu ya Serikali kunyanyasa vikundi vingine na tukavipa nembo ya ugaidi. Jambo hili katika SADC na Afrika kwa ujumla ni lazima tuliangalie, kupitia hili Azimio tuwe na model nzuri ya kusema ugaidi ni nini na namna gani tuna-combat nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu hapa yalitokea pale Rufiji ilikuwa ni ugaidi, lakini tumeona Msumbiji imekuwa ni ugaidi, wenzetu wa West Africa wanasumbuliwa sasa na ugaidi nchi karibu tatu zote zile. Kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba lengo letu tuwe katika nyanja zaidi ya kiusalama badala ya kushabikia ugaidi hasa kwa maana ya context ya dunia ambapo bado hatujakubaliana gaidi ni nani katika mtazamo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nchi zetu na Serikali zetu ni lazima ziangalie mipasuko katika jamii kwa kuwapelekea rasilimali, mgawanyo wa rasilimali uwe unakwenda sawasawa; moja ya maeneo yanayozalisha ugaidi ni baadhi ya jamii kutengwa, ni baadhi ya jamii kuona sasa hawafaidiki. Vilevile nchi zetu zina utajiri wa madini, baadhi ya maeneo ugawaji wa rasilimali haujakaa sawasawa; kwa hiyo, Tanzania kama kioo na kama kiranja wa ugawaji sawa wa rasilimali, ni lazima tuzikumbushe nchi zingine za Afrika ambazo tunaingia nazo katika Itifaki hii kwamba, lazima kuwe na usawa wa kugawanya rasilimali ili kuondoa minong’ono katika vikundi vingine katika jamii na hasa kuzalisha ugaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa, ni lazima sote tukubaliane kwamba mitazamo ya kidini imetumika katika ugaidi na kwa bahati mbaya yapo maeneo ambayo wamepata indoctrination hasa katika watoto wadogo na baadaye kuingia katika stage kubwa ya ugaidi. Pamoja na hilo lazima na Tanzania iendelee kuwa mfano katika hizi nchi nyingine za Afrika kwamba sisi tumewezaje kukaa na dini mbalimbali, tumewezaje kuishi pamoja na tumewezaje kuvumiliana katika kuwa makabila zaidi ya 127. Kwa hiyo, tunavyoingia kwenye Itifaki hii tuna kazi ya kuwaonesha wenzetu, tuna kazi vilevile ya kutoa somo kwamba ni namna gani katika jamii nyingi kwa ujumla na namna gani una in grace zile differences ili uweze kuwa na jamii ambayo haina mikwaruzano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya hivyo kama nilivyosema pamoja na kuingia katika itifaki hii sisi tuwe kiranja katika kuonesha wenzetu ni namna gani wanaweza wakakumbatia zile tofauti zilizopo, tumefanya hivyo katika miaka mingi, tumekuwa wasuluhishi migogoro ya Maziwa Makuu. Kwa hiyo, kama nilivyosema tuna jukumu kubwa lakini kikubwa zaidi tusitumie ugaidi katika context ambayo baadhi wanazo tofauti zao za kisiasa na baadhi ya vikundi vinafadhiliwa na Serikali za nchi mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana. (Makofi)