Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi kuwa mchangiaji wa mwisho kwa siku ya leo katika Wizara hii ya Afya. Kwanza nipende kutoa pongezi nyingi kwa waliopata nafasi hii, Mawaziri hawa, Mheshimiwa Ummy pamoja na Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla. Hongereni sana maana tunatambua jitihada zenu mnazofanya kuhakikisha kwamba Taifa linasonga mbele hasa kwenye sekta ya afya na afya ni uhai. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napenda kuchangia kwenye sekta hii ya afya hasa kwenye eneo la CHF. CHF ilipokuwa inaanza mwanzo mfano katika Wilaya ya Igunga ilikuwa ni sehemu mojawapo ya majaribio na ilifanya vizuri sana kiasi kwamba Wilaya zingine zilikuwa zinakuja kuangalia namna gani imefanya vizuri katika Wilaya ya Igunga. Matokeo yake sasa hivi si tu wilaya zilikuwa zinakuja kujifunza Igunga lakini sasa CHF Igunga inafanya vibaya kama ambavyo inavyofanya vibaya katika maeneo mengine.
Mheshimiwa Spika, mwanzo CHF ilikuwa na Mfuko wake, akaunti yake ambapo zile fedha zilizokuwa zinakusanywa zinahifadhiwa sehemu moja, lakini baada ya Waraka uliotolewa na Wizara ya TAMISEMI kuhakikisha kwamba kila Halmashauri iwe na akaunti zisizozidi sita ikapelekea fedha za CHF kwenda kwenye akaunti za halmashauri na fedha zile zikawa zinabadilishiwa matumizi. Kutokana na kubadilishiwa matumizi kunakuwa na upungufu wa fedha za kununulia dawa.
Mheshimiwa Spika, hivyo tunaomba Wizara hizi mbili zikae chini ziangalie upya ili Mfuko huu wa CHF urudi kama ilivyokuwa awali, iwepo akaunti special ya CHF. Ikiwepo akaunti special ya CHF itapelekea kurudisha ubora, lakini pia itapunguza uhaba wa dawa katika hospitali zetu. Maana tunawahamasisha wananchi wajiunge katika CHF, lakini mwisho wa siku akienda kwenye vituo vya afya hakuna dawa. Kwa hiyo, tuombe Wizara ya Afya katika hili waliangalie upya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nipende kuzungumzia suala ambalo limezungumzwa na ndugu yangu hapa, kaka yangu Mheshimiwa Hussein Bashe la ADB. ADB wamekuwa wanafadhili katika nchi yetu katika eneo la afya. Katika Wilaya yetu ya Igunga na wilaya nyingine Tanzania ADB wameweza kujenga majengo mazuri katika vituo vya afya na hospitali zetu. Wamejenga majengo mazuri pale Choma, Nanga katika Jimbo la Mheshimiwa Kafumu, Igurubi, Hospitali ya Wilaya ya Igunga na katika hospitali mbalimbali ndani ya nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, napata wasiwasi jinsi hii miradi inavyotekelezwa kwa sababu sehemu nyingine wanajenga wanafika mpaka mwisho na vifaa vinapelekwa, lakini sehemu nyingine wanajenga jengo linaishia katikati, kwa mfano, katika Tarafa ya Simbo, Kata ya Simbo, jengo limejengwa limeishia katikati na hakuna vifaa vilivyopelekwa. Unajiuliza hizi fedha za wafadhili zinasimamiwa na watu gani? Haiwezekani kwingine zijengwe zifike mwisho na vifaa viletwe, tena vya gharama kubwa, sehemu nyingine jengo tu lisimalizike. Kwa hiyo, naomba Wizara ipitie upya, waangalie hii miradi inayofadhiliwa na wafadhili isimamiwe vizuri ili kuweza kuleta tija.
Mheshimiwa Spika, siyo tu kusimamiwa maana tumeona pamoja na majengo kwisha na vifaa kuletwa, kwa mfano pale Choma Chankola, Igurubi, Itumba na maeneo mengine ambayo kaka yangu Mheshimiwa Bashe ameyazungumza na mengine yako kwa Naibu Waziri Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla kwake kule, wamejenga wameweka na vifaa lakini vituo hivi havijafunguliwa, vinakaa muda mrefu bila kufanya kazi. Wameweka vifaa yenye thamani kubwa ukiangalia unaona kabisa vinatakiwa vianze kutumika.
Mheshimiwa Spika, pia Theater zinajengwa vizuri wanaleta na vifaa safi lakini zinachelewa kufunguliwa, tunajiuliza kuna tatizo gani? Hakuna wasimamizi wanaofuatilia kila siku kuona hivi vitu ambavyo vinawekezwa na wafadhili havipotei ama haviharibiki maana vinatelekezwa mpaka watu waanze kulalamika au watu waanze kupiga kelele majukwani huko mitaani ndiyo tuanze kujua kwamba kumbe kuna miradi ya wafadhili ambayo haitiliwi maanani.
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, katika Wilaya ya Igunga katika Jimbo la Manonga pale Simbo, mradi umeishia katikati unakabidhiwa kwenye halmashauri halafu wanasema eti halmashauri imalizie. Halmashauri inatoa wapi fedha ya kumalizia miradi mikubwa ambayo imeanzishwa na wafadhili hawa? Kwa hiyo, tuiombe Wizara, hii tabia ya wafadhili wanakuja wanafadhili halafu wasimamizi wale wanafikia katikati eti wanawaambia halmashauri wamalizie wanamaliziaje? Hata vifaa vinavyotakiwa viwekwe wanavitoa wapi na fedha ziko wapi?
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niombe Wizara ipitie upya suala hili, warudi waangalie katika wilaya hizo nilizotolea mfano za Igunga, kwa kaka Mheshimiwa Kafumu, kwangu mie, ukienda kwa Mheshimiwa Zedi tatizo lipo, ukienda kwa Mama Sitta kule najua litakuwepo na kwa Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla lipo na kwa Mheshimiwa Bashe lipo.
Mheshimiwa Spika, naomba hii miradi inayofadhiliwa na wafadhili waisimamie ili tufike mwisho, isiwe inafika katikati inatelekezwa, baadaye inakuwa kero na kero hii inakuwa moja ya changamoto ndani ya chama na Taifa. Kwa hiyo, niombe Wizara iangalie na kuhakikisha inaboresha katika maeneo hayo niliyozungumzia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini Wabunge wenzangu wamezungumza kuhusu masuala ya Basket Funds zinavyokuwa haziendi kwa wakati katika hospitali zetu. Niombe Wizara kwa sababu wanasema hizi Wizara zimeungana au zinafanya kazi pamoja na TAMISEMI wahakikishe wanafuatilia kujua hizi Basket Funds zinakwenda kwa wakati kwenye halmashauri ili kupunguza uhaba wa dawa katika hospitali zetu.
Mheshimiwa Spika, hospitali hazifanyi kazi wanakwambia Basket Funds haijaja matokeo yake kunakuwa na mlundikano wa wagonjwa ambao wanakosa dawa hatima yake wanapoteza maisha hawa ambao wanatakiwa wapate tiba. Kwa hiyo, niombe Wizara iangalie hili zoezi na walipitie upya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo nataka kuchangia ni kwenye hizi zonal hospital. Tumeona kuna Hospitali ya Bugando, tumeona Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Kusini lakini sijaona hospitali ya Kanda ya Magharibi. Kwa hiyo, niiombe Wizara iangalie upya ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kuwapeleka katika kanda hizi nyingine. Mkiiboresha Hospitali ya Kitete mkaipa hadhi ya kuwa Hospitali ya Zonal, basi hata kama siyo Hospitali ya Kitete mnaweza mkaipa hata Nkinga Hospitali kuwa hospitali ya zonal ili kupunguza msongamano wa wagonjwa kwenda katika hizi hospitali zinginezo. Hizi hospitali zilizo ndani ya Mkoa wa Tabora geografically zilivyokaa zinaweza kuhudumia watu kutoka Kigoma, Shinyanga, Singida na wengine kutoka Katavi pamoja na Rukwa. Kwa hiyo, niombe sana Wizara iangalie zonal hospital katika Mkoa wa Tabora. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia hii Hospitali ya Mkoa wetu wa Tabora ya Kitete, toka tumeifahamu ina X-ray ya miaka nenda rudi, inakufa, kila siku wanafanya marekebisho. Hii Wizara iangalie namna gani italeta X-ray mpya ili kuboresha huduma za watu wa maeneo yale lakini iendane na kasi ya ongezeko la watu katika eneo lile. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia hospitali zetu za wilaya, japo mmesema kwamba hospitali hizi zipo TAMISEMI na Wizara ya Afya iko kwa mbali sana, naomba sana hospitali hizi ziangaliwe.
Mheshimiwa Spika, mwisho, napenda niunge mkono hoja. Ahsante kwa kunipa nafasi.