Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia jambo hili muhimu sana ambalo linajenga mustakabali wa kuijenga nchi yetu miaka inayokwenda mbele na miaka ya sasa. Naomba nianze kwa kuunga mkono kabisa hoja nzuri ambayo Mheshimiwa Ezra ameileta, hoja ya kukomboa kizazi chetu.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu sasa ni nchi ambayo inajiunga na forum mbalimbali ikiwepo East Africa na nchi zinazidi kuongezeka ndani ya East Africa na wenzetu wanasomesha watoto wao kwa nguvu kabisa. Katika nchi yetu mkombozi pekee aliyebaki katika suala la ajira ni kujiajiri. Sasa tunataka vijana wetu wajiajiri lakini tunataka kuepuka kuwasomesha, sasa sijui watajiari kwenye ajira gani? Nasema hivi kwa sababu wanashindana na wenzao katika East Africa ambao wamesoma sana na mipango ya kujiajiri lazima watu wawe wamesoma, kwa hiyo hiki ambacho kinatokea sasa tunakokwenda vijana watakuwa ni wafanyakazi sijui wafanya kazi za ndani sijui za mashambani? Maana yake tutakuwa hatuna wasomi ambao wamesoma ili waweze kujiajiri na kuajiri wenzao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo suala hili, naomba kabisa Bunge lako tuje na solution ya haraka ili vijana wetu ambao wamefaulu vizuri waende wakasome. Huu utaratibu jinsi gani wanapata mikopo ya asilimia mbili, asilimia tatu pengine umefeli. Baada ya hao kuondoka, naomba Bodi ya Mikopo waje hapa watueleze formula hizi wanazitumia vipi, wanachagua vipi watu hawa. Tuwasaidie mawazo ikiwezekana, kwa sababu inaonekenana wamelemewa na huu mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kama alivyosema mwenzangu Mheshimiwa Kanyasu, huu ni mkopo wa aina gani? Mbona ni kama hisani. Wapo watoto wana division one mwaka jana hawakupata mikopo, wamekaa mwaka huu ndio wamebahatisha asilimia ndogo, wengine ndio wamefaulu na division one mwaka huu, hawajapata kabisa, afadhali hata yule aliyetolewa mfano ana viasilimia kidogo, wako wengi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo niombe suala hili kwa kweli tutoke na muafaka hapa jinsi gani watoto wetu hawa ambao wamefaulu vizuri wanakwenda shule. Vinginevyo nchi yetu hii tuna idadi kubwa ya watu ndani ya East Africa, ukiacha Congo, lakini sasa sijui ndio tutaanza ku-provide wafanyakazi wa ndani kwa wenzetu. Kwa kweli inabidi sasa tuliangalie jambo hili kwa makini sana. Bajeti imeongezeka tulisikia hapa, bado marejesho yanafanyika, lakini sijui kitu gani kinatokea katika jambo hili. Jambo hili ni serious sana, hatuna urithi mwingine wa kuwarithisha vijana wetu na watoto wetu zaidi ya elimu, tukishampa elimu tunamwambia ardhi ile pale, mifugo hiyo hapo, nenda kajiajiri, lakini elimu wanayo, hivyo, atajua ata-convert vipi hiyo ardhi ili iweze kumpatia maslahi. Sasa hili atalifanya vipi kama hana elimu kichwani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ningeomba niunge hoja suala hili na tulichukulie kwa makini, kwa u-serious mkubwa, hawa waende lakini Bodi ije hapa itueleweshe vizuri formula wanayotumia, tuwasaidie mawazo ili usawa upatikane. Watoto wengine wakishasoma private ndio kibali cha kunyimwa mkopo tayari. Pengine amesaidiwa huko wengine na compassion, wengine wamesaidiwa na Mbunge na wengine wamesaidiwa na mjomba. Mjomba ameshafariki, eti kwa sababu kasoma privatae tayari anaambiwa wewe huna sifa ya kuwa na mkopo. Kwa hiyo ningeomba hii formula iangaliwe upya kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hayo machache kwa uchungu sana naunga mkono hoja. Nakushukuru sana. (Makofi)