Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hoja ya Dharura kuhusu Mikopo ya Elimu ya Juu Nchini

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Rais ametusaidia sana katika kutuletea fedha za elimu, hasa katika Majimbo yetu, kwenye shule za Msingi, shule za Sekondari na sasa ndiyo hili tatizo linajitokeza hapa.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuunga mkono mara moja hoja hii ya Mheshimiwa Ezra. Kwa sisi ambao tunaabudu katika Biblia, maneno ya Mungu yanasema hivi kwenye Mithali 4 Mstari wa 13, “Mkamateni sana elimu msimuache aende zake, mshike maana yeye ni uzima.” Kama haitoshi Biblia inasema tena kwenye Kitabu cha Hosea, “Watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa”. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimenukuu tena kwenye neno…

SPIKA: Sasa ngoja nikusaidie kidogo, ni watu wangu wanaangamizwa, sio wanaangamia, watu wangu wanaangamizwa.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, sawasawa. Kwa kukosa maarifa na maarifa yanaletwa na elimu. Kwenye misahafu, amenisaidia hapa Mheshimiwa Nahodha, Mtume anasema hivi, tafuteni elimu mpaka China. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sasa hapa nimejaribu kuangalia na kwenye Biblia yangu hapa nimefungua neno elimu limeandikwa mara 300 kwa umuhimu wake, neno tu elimu. Nimesoma kitabu cha Mheshimiwa Hayati Benjamin Mkapa, Mheshimiwa Rais wetu cha ‘‘Maisha Yangu Malengo yangu au Maisha Yangu Dhamira Yangu’’ amendika, yeye mwenyewe nanukuu: “Mimi leo ni Rais nisingefika hapa bila elimu” Mwisho wa kunukuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nia yangu ni kuonesha jinsi ambavyo elimu imepewa kipaumbele kwenye Biblia na Misahafu pia kwa viongozi wetu wa nchi. Tumeona sisi hapa leo hii, mimi kule Jimboni wanafunzi wengi wa vyuo wamerudi sasa kwa sababu kwa kweli hawana mikopo na hawawezi kuendelea bila mikopo. Ukiangalia bajeti ya mwaka jana, amesema Mbunge mmoja hapa na nimesoma ni zaidi ya Bilioni 427, tena mwaka huu Bilioni 570. Ni lazima sasa Serikali ije na projection tunapokwenda kwenye miaka ya bajeti tuhakikishe kwamba tatizo hili halijirudii tena, kwa sababu hili ni bomu na bomu hili linakuja pale ambapo sasa tunaendelea kukatishana tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika familia zetu maskini watu wengi kwa kweli kwa sasa wameshauza mashamba, wameuza ardhi, wamefanya mambo mengi kufikisha watoto katika level hii ya University. Sasa inapofika mtoto anakosa fedha ya mkopo ili kuendelea na masomo yake, hasa akiwa mwaka wa pili au mwaka wa tatu na kurudi nyumbani, hii ni hatari sana.

Mheshimiwa Spika, siyo hilo tu, ukiangalia sasa hivi katika zile sifa za kupata mkopo, awe yatima, awe fukara, asiwe na wazazi, haya yote Serikali haina uwezo wa kujua moja kwa moja na kama inao basi maana yake ni kwamba, hali yetu imeshakuwa mbaya sana.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba hii Bodi ya Mikopo ivunjwe mara moja kwa sababu inaonekana sasa haina namna ya kutusaidia, lakini pili utaratibu huu wa kuona namna gani ya kupata mkopo kutoka mtoto wa fukara au masikini utaratibu huu uangaliwe upya kwa sababu, inaonesha kabisa hali ni mbaya kule kwenye maeneo yetu na wananchi wanapata shida.

Mheshimiwa Spika, pia tuone tutafute hela ya dharura ili watoto hawa waweze kwenda shule, tusipofanya hivyo tutakuwa tumezalisha watoto ambao baadae hawawezi kuwa viongozi. Kwa mfano, ametoa mfano mtu mmoja hapa, Rais wetu wa Kwanza, Baba wa Taifa, ameenda shule na wakati ule bahati nzuri shule ilikuwa bure na ametoka kwenye familia tunayoijua. Rais wa Pili, Rais wa Tatu, Rais wa Nne na Rais wa Tano, bila ya elimu asingeweza kuwa Rais na huyu wa Sita kaenda sana, unajua leo hii bila elimu kwa nafasi hii ya Urais watoto wetu wale fukara hawawezi kuwa viongozi.

Mheshimiwa Spika, ombi langu ni kwamba Wabunge leo hii tusimame, tuungane kwa jambo hili, Serikali ije na fedha ya dharura kuwasaidia watoto hawa ambao wako nyumbani wanaotakiwa kwenda vyuo sasa. (Makofi)

SPIKA: Haya ahsante sana, muda wako umekwisha.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naunga hoja hii mkono. (Makofi)