Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Biharamulo Magharibi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kukushukuru sana kwa kukubali hoja hii iwasilishwe hapa.
Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge. Wamechangia jumla ya wachangiaji 16, nadhani sitaweza kuwataja kwa majina kwa sababu ya muda, lakini niwashukuru sana kwa sababu mmeeleza kwa kina, Watanzania wamesikia kwa sababu Bunge hili ni la Watanzania na hii ndiyo sehemu yao wanapoweza kusikiliza maoni yenu kwa niaba yao.
Mheshimiwa Spika, lakini pia hata wale ambao wamekosa mikopo wamesikia, kwa hiyo sina haja ya kuyarudia yote ambayo Waheshimiwa Wabunge mmeongea kwa sababu ni dhahiri yameeleweka, kila mmoja ameyasikia. Ila sasa kwa sababu ya ku-save muda mimi ninaomba niende kwenye maazimio, kwa sababu tumesikia mengi hapa. Nina maazimio matatu ambayo nataka kuyawasilisha kwako. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, cha kwanza, kwa sababu tayari vyuo vimeshafunguliwa na watoto hawa wako majumbani wanahangaika, hawakupenda wawe nyumbani leo, ni kwa sababu wamekosa mikopo, tunaomba Serikali itoe tamko hapa la kuruhusu watoto hawa warudi vyuoni wakaungane na wenzao kipindi inatafutwa solution ili wasichelewe masomo kwa makosa ambayo siyo ya kwao. (Makofi)
Kwa hiyo, naomba tupitishe kama azimio ili wanafunzi hao, wale ambao wana vigezo na vinajulikana, lakini hawapo vyuoni kwa sababu pesa haijapatikana, kwa hiyo, Serikali itoe tamko na kama Bunge tuazimie ili sasa watoto hawa warudi shuleni, wakaungane na wenzao wakati solution inatafutwa.
Mheshimiwa Spika, azimio la pili,…
SPIKA: Kabla hujaenda kwenye azimio la pili; kwenye hilo la kwanza, ili Bunge lijue linahojiwa nini, kama umeliandika hebu ulisome maana umeenda na maelezo mengine ya ziada, kwa hiyo, hatutajua tunaazimia kwenye kitu gani? Kama unayo sentensi ya kuisema moja, mbili, tatu ili Bunge linapohojiwa, basi lijue linahojiwa nini? Kama unalo, lisome; kama huna, basi itabidi uandike.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, Azimio la kwanza; Kwa kuwa vyuo vimefunguliwa na baadhi ya watoto wameripoti vyuoni;
Na kwa kuwa wanafunzi hao wanavyo vigezo lakini wamekosa mikopo;
Hivyo Basi, waruhusiwe kuripoti vyuoni huku Serikali kwa kushirikiana na Bodi ya Mikopo wakitafuta fedha za haraka ili kukidhi uhitaji wa watoto hao. (Makofi)
SPIKA: Endelea na la pili.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, Azimio la pili; Kwa kuwa inaonekana shida kubwa hapa ni fedha;
Hivyo basi, Serikali ilete budget review hapa ili tuweze kujadili na hatimaye watoto hao ambao wamekosa fedha tuweze kupitisha kama Bunge ili fedha hiyo ipatikane kwa ajili ya kufanya nyongeza ya bajeti. (Makofi)
Sasa sijui ina….
SPIKA: Endelea tu, mimi nakusikiliza.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, Azimio la tatu; Kwa kuwa kutokana na michango ya Wabunge na hali iliyoko huko nje, malalamiko mengi yanailenga Bodi;
Na kwa kuwa tumeshindwa kupata majibu kwa muda mrefu;
Hivyo Basi, iundwe Tume Maalum ya Kibunge, ambacho ndicho chombo cha uwakilishi wa wananchi, ikapitie maoni ya Wabunge wote ambayo wameyataja hapa, pia iende Bodi ikachunguze nini kinaendelea huko kwa sababu inaonekana Serikali imeshindwa kuichunguza Bodi na hatimaye irudishe majibu ndani ya Bunge ili tuweze kufanya maamuzi kwa niaba ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mapendekezo ni hayo matatu.
SPIKA: Sawa. Azimio la kwanza na la tatu nimeyapata vizuri, hebu rejea la pili.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, la pili; Kwa kuwa inaonekana shida kubwa ni bajeti (fedha) ndiyo imefanya watoto wengi wasipate mikopo;
Hivyo Basi, Serikali ilete budget review ili kama Bunge tupitie na kutoa mapendekezo hatimaye tuweze ku-approve nyongeza ya bajeti kwa ajili ya Loan Board ili waweze kukopesha watoto wengi hao waliobaki huko bila fedha. (Makofi)
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hilo ni la tatu. Ulisema yapo matatu?
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ni matatu tu.
SPIKA: Haya hitimisha.
MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge likubali maazimio haya kwa ajili ya kuyapitisha.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)
(Hoja ilitolewa Iamuliwe)
MHE. CONDESTER M. SICHALWE: Mheshimiwa Spika, naafiki.