Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nianze kwa kuungana na waliotangulia kuchangia kumshukuru Mheshimiwa Rais hasa kwa kazi kubwa anayofanya ya kutuletea miradi mingi kwenye majimbo yetu.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kujieleza kwenye chimbuko halisi, chimbuko lenyewe la Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Mamlaka ya Serikali za Mitaa chimbuko lake tutakumbuka wote wakati wa Ukoloni Serikali za Kikoloni zilianzisha mamlaka hizi na waliziita Local Authorities, lakini walizigawanya kwenye makundi takribani matatu na zinazotuhusu Waafrika waliziita Native Authorities.

Mheshimiwa Spika, hapa nchini Tanzania, Hayati Baba wa Taifa mwaka 1997 aliamua kuziondoa Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Baadaye miaka ya 1982 aliona umuhimu wa kurudisha Mamlaka za Serikali za Mitaa na zikatungwa sheria mbili za Bunge; Sheria za Serikali za Mitaa Mamlaka ya Wilaya (Sura Na. 287) na Sheria za Serikali za Mitaa Mamlaka ya Miji (Sura Na. 288).

Mheshimiwa Spika, hali kadhalika mwaka 1998 tukawa na Sera ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa. Dhana ilikuwa ni kutengeneza mazingira wezeshi kwa wananchi na ugatuaji wa mamlaka ulikuwa unakusudia kwamba wananchi washirikishwe moja kwa moja kupitia mamlaka zao pale kuanzia ngazi ya Kijiji, Kata halikadhalika mpaka ngazi ya Wilaya.

Mheshimiwa Spika, baada ya kupitia taarifa ya CAG ukurasa wa tisa, taarifa inaeleza kwa habari ya udhaifu katika uwekaji wa mitaji wa Mamlaka za Serikali za Mitaa. Taarifa nimeitolea mfano, Manispaa Jiji la Dar es Salaam wamewekeza hisa takribani 24,036,348 kwenye Benki ya DCB zenye thamani ya Shilingi bilioni 5.77, lakini taarifa inaendelea kusema kwamba Benki hii utendaji kazi wake hauridhishi. Sasa udhaifu huu chanzo ni nini? Naomba nianze hapo.

Mheshimiwa Spika, leo hii hakuna mwongozo, sheria hata kanuni inayoweza kutoa mwelekeo au kuelekeza halmashauri namna gani zinaweza kufanya uwekezaji. Tuanze hapo. Hatuna mwongozo, sheria, au kanuni inayoelekeza namna gani halmashauri zetu nchini zinaweza zikawekeza mitaji. Ameendelea mbele zaidi akatolea mfano Jiji la Dodoma kwamba hapo awali ndani ya Jiji la Dodoma; ukisoma ule ukurasa wa tisa kuna mfano bora, mzuri wa Jiji la Dodoma kwamba limejenga Hoteli ya nyota tano pale Mji wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, nianze hapo. Jiji la Dodoma sisi tilijiongeza tu wakati huo na nitangaze maslahi, nikiwa nahudumu kama Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma. Nianze bajeti sasa, nitoe mifano ya namna gani mlolongo wa namna gani mapato ya ndani yalikuwa yakikua mwaka hadi mwaka hadi mwaka. Mwaka 2015/2016 bajeti ya Jiji la Dodoma ya Manispaa ya Dodoma bilioni 4.5 na makusanyo yalikuwa bilioni 3.6. Mwaka wa Fedha 2016/2017, makisio yalikuwa bilioni 3.9 na makusanyo yalikuwa bilioni 4.8 wakati huo, tukatumia bilioni 1.8 kupeleka kwenye miradi ya maendeleo, hapo awali ilikuwa ni ngumu hata kujenga choo cha shule ya msingi kupitia mapato ya ndani, tulianzia hapo. Mwaka wa fedha 2017/2018, makisio yalikuwa bilioni 20 kutoka bilioni 3.9, tukakisia bilioni 20 na tukafanikiwa kukusanya bilioni 25, tuka break even. Kwa nini tulikisia bilioni 20 kutoka bilioni 4.8?

Mheshimiwa Spika, tulikisia hivyo kwa sababu, mtakumbuka mwaka 2017 Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliondoa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Makuu (CDA) na yenyewe ilikuwa na bajeti yake. Sasa mwezi Disemba tukafanya mapitio ya bajeti, wao bajeti yao tukaingiza kama bilioni 13 ambayo inatokana na viwanja na ya kwetu ikawa bilioni saba ikawa bilioni 20, lakini viwanja vile havikuwepo, ilikuwa ni bajeti tu kama bajeti. Tukavipima, ndio vikapatikana na tukapata hiyo bilioni 13 na tuka-break even kwa bilioni 25. Halikadhalika sasa mamlaka ya upangaji ikawa jiji kwa maana ya manispaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka wa fedha 2018/2019, tukakisia bilioni 67, kutoka makusanyo ya bilioni 25, tukakisia bilioni 67, tuka-break even, tukakusanya bilioni
71. Tukasema viwanja muda unavyokwenda maana yake itafika mahali soko litapungua na sisi karibu asilimia 70 ya mapato tunategemea viwanja na ndio ilikuwa fursa kwetu Dodoma. Badaye nitarejea namna gani halmashauri nyingine zinaweza kufanya hivyo kwa fursa ambazo zipo huko.

Mheshimiwa Spika, tukasema hapana, Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi, sasa haya mapato ya bilioni 71 yatakuwa sustainable? Jibu likawa hapana, sustainability, yaani uendelevu wa mapato hayo utafika mahali utashuka kwa sababu chanzo cha ardhi kikipungua hatuwezi kufikia hayo malengo. Tukakaa na management team yetu tukakubaliana tutafute uwekezaji ndani ya Jiji la Dodoma. Tukaona fursa pekee Dodoma, watumishi wanahamia, watu mbalimbali wanahamia, tukasema tuanzishe hoteli. Tujenge hoteli na hii miradi ni ya kimkakati, lakini pia tujenge nyumba za kupangisha watumishi, tulikuwa tunafikiria hivyo ili hii fursa tuitumie kama Makao Makuu ya Nchi.

Mheshimiwa Spika, tukaanza na hoteli. Pale Mji wa Serikali ule mradi uliitwa Government City Complex na lengo lilikuwa ni kujenga miradi mbalimbali hadi shopping mall pale. Kwa phase one tumefanikiwa kujenga hoteli ya bilioni 18. Naomba niweke sawasawa hapo, phase one ni bilioni 18, ile hoteli inayoonekana pale Mji wa Serikali na ni hoteli yenye hadhi ya nyota tano. Kama haitoshi tukatumia tena bilioni tisa kwa mapato ya ndani, sio mkopo wa benki wala fedha kutoka Serikali Kuu, tukajenga hoteli nyingine mkabala na White House, ukumbi wa pale Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi ya bilioni tisa.

Mheshimiwa Spika, hii yote ilikuwa ni mikakati ya kuhakikisha kwamba, mapato yetu, demand ya viwanja ikipungua maana yake sasa hii inakwenda kuwa mbadala wake. Leo hii hoteli hizo nadhani wanatafuta operators ili zianze kuleta fedha.

Mheshimiwa Spika, nataka kusema nini? Ni kweli kuna udhaifu mkubwa kwenye namna ya miradi inayoanzishwa kwenye halmashauri, kwa nini? Hoja ileile, hatuna sheria, mwongozo wala kanuni inayoelekeza namna gani halmashauri zinaweza kuwekeza au kufanya uwekezaji. Niseme tu dhana hii ya sera yenyewe huko duniani, nitoe mfano mathalani Jiji la Pretoria, South Africa; ukienda pale Tshwane Metropolitan City Council wale wana-deal hadi na kampuni, wana idadi ya kampuni zaidi ya sita, wanatoa dividends to central Government, Tshwane Metropolitan City Council.

Mheshimiwa Spika, sasa huko nchi nyingine, ukienda vilevile Nigeria, majiji mengi duniani yanajitegemea yenyewe bila kutegemea Serikali Kuu. Sasa nchini kwetu ni tofauti kidogo, mathalani Jiji la Dar-es-Salaam. Nilikuwa naangalia hapa Jiji la Dar-es-Salaam, lenyewe kwa mwaka wa fedha 2021/2022 limekusanya bilioni 75, lakini leo hii recurrent ya Serikali Kuu inapeleka, mishahara ya watumishi inalipa Serikali Kuu. Bilioni 75 wanakusanya, lakini hata kamradi tu, hata kujenga tu zahanati, Hospitali ya Wilaya bado tunasema central government.

Mheshimiwa Spika, nataka kueleza hapo kwa hiyo, namna gani naweza kusema, lakini halikadhalika Kinondoni 49 bilioni, Arusha 23 bilioni, Mwanza bilioni 17. Nikirudi kwa maana ya fursa za halmashauri huko zilizoko, natoa mfano kule niliko kwa sasa Jimbo la Mlimba. Sisi bajeti yetu kwa mwaka ni bilioni 3.7. Tumetengeneza mpango wa kujenga kila mwaka kituo cha afya kimoja na mpaka sasa ninavyozungumza tunajenga vituo vya afya vitatu, Serikali kuu imetupa kimoja tu. Tunajenga Kituo cha Afya Chita, OPD imekamilika na tumefungua, Kituo cha Afya Kata ya Igima kinajengwa, lakini na vilevile Kituo cha Afya Kata ya Mofu kwa mapato ya ndani, 1.5 billion.

Mheshimiwa Spika, sasa kama Halmashauri ya Mlimba ndogo, yenye bajeti ya 3.7 billion inajenga vituo vya afya, hivi kweli na Dar-es-Salaam wanapiga magoti Serikali kuu? Majiji? Arusha Jiji? Ndio maana sasa matumizi mabaya ya fedha yanatokea kwa sababu, pesa haina matumizi. Wizara ijipange kutengeneza mpango kwenye majiji haya. Niliwahi kushauri huko nyuma watengeneze clusters kwa majiji na manispaa na ruzuku inavyokwenda waangalie, halikadhalika Wilaya. Kwa sababu, kwa mfano, nilikuwa naangalia pia halmashauri nyingine; kuna halmashauri zinakusanya chini ya bilioni moja, lakini fedha ya ruzuku ya maendeleo inaenda sawa na nyingine ambazo zinakusanya zaidi ya bilioni 10. Sasa Mheshimiwa Waziri kwa sababu yupo hapa hebu aliangalie hili ili tusiwe na uneven distribution of national income. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hatuwezi kupeleka fedha kwenye halmashauri zote ambazo zina uwezo wa kukusanya fedha kwa hiyo, lazima tuangalie, tutengeneze clusters. Cluster A, Cluster B, Cluster C, ili sasa tupeleke fedha za miradi ya maendeleo na recurrent kwa maana ya matumizi mengineyo ziende kulingana na mahitaji yao.

Mheshimiwa Spika, baada ya kumaliza hayo, niende eneo lingine. Mfano nilisema Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, sisi tumekubaliana sasa, tumeanza, tumeshalima shamba la miti lenye ekari takribani 1,386, fursa tumeona ni miti. Nilivyokuwa Dodoma niliona hoteli ni fursa, kule tumeona fursa ni miti ya mbao, halmashauri zote zinaweza kufanya haya, Mungu alivyoiumba Tanzania ina fursa za kila aina kwa sehemu yao. Halikadhalika kule Songea wanaweza kulima hata mahindi, huku Rukwa wanaweza kulima hata mahindi ambayo ni miezi minne mitano unavuna.

Mheshimiwa Spika, sasa tukiendelea kusubiri kodi za wananchi, kama haitoshi tunalima pia na korosho na tumepanda ekari takribani 135 mpaka sasa. Nilikuwa nimesema Mlimba baada ya five years, huko nyuma nilisema Dodoma kwa sababu ndio Makao Makuu ya Nchi, kule actually tumeanza from the scratch, inawezekana.

Mheshimiwa Spika, changamoto tuliyonayo, narudia kusema, ni mindset, fikra. Wakati mwingine unaweza ukazungumza hapa kuwa kama uko sayari nyingine kumbe uko sayari hii hii.

Mheshimiwa Spika, changamoto ni fikra (mindset), utayari wa kuamua kufanya jambo (commitment), lakini mwisho uzalendo. Unakuta Mkurugenzi wa Halmashauri tangu ameteuliwa hata kubadilisha kiti hawezi, hata kiti tu. Hata kubadilisha mkao wa kiti tu. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, kule South Africa nafasi hizi nyeti zinatangazwa watu wanaomba na wanamwita Municipal Manager, hawaiti Director, wanaita Municipal Manager, City Manager, wanatangaza kazi na watu wanaomba Professionals, sasa sisi mfumo wetu ni wa uteuzi. Sasa mimi najaribu kueleza hali halisi.

Mheshimiwa Spika, nijielekeze eneo lingine ambalo ni muhimu sana, eneo la Ofisi ya Mkaguzi wa Ndani Halmashauri. Ofisi hii ni muhimu sana, lakini tunaitazama kana kwamba, haina kazi, haisaidii chochote na ndio maana mianya ya wizi wa fedha ya Serikali unatokea. Leo hii uliza Halmashauri ngapi zina Mkaguzi wa Ndani ana gari? Anakaguaje miradi ya maendeleo wakati hana gari wala facility yoyote? Kwa hiyo nadhani Mheshimiwa Waziri aliangalie hilo. Lazima Ofisi za Mkaguzi wa Ndani ziwezeshwe zifanye kazi zao vizuri. Huyu ndio watch dog wa kwanza kwenye level ya halmashauri kule.

Mheshimiwa Spika, mwisho, nijielekeze kwenye eneo hili la Mfuko wa Mikopo kwa Vikundi. Tuna sheria nzuri kabisa na niwaambie fedha hizi zinazokwenda kwenye vikundi zina tija sana kwa wananchi wetu na sisi Mlimba, nataka nitoe mfano Mlimba, nataka kusema kwa sababu tunayafanya hayo; Mlimba sisi kila mwaka hatudai chochote, wananchi wanarejesha fedha zote, tumefanyaje? Naomba ku-share experience.

Mheshimiwa Spika, tumetengeneza utaratibu wa kugawana majukumu, kwa hiyo, Madiwani wao kwenye vikundi vya kata fulani anasimamia kurejesha fedha. Kama kata hiyo kuna kikundi chochote hakijarudisha fedha mikopo ijayo hakipati, kata hiyo haipewi kwenye mgawo. Kwa hiyo, inakuwa ni jukumu la Diwani kuwa mlezi wa kikundi na kuhakikisha fedha inarejeshwa kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo kwa kuwa kengele imelia, naomba kusema tu kwamba, nahitimisha mchango wangu hapo, lakini nakushukuru sana. (Makofi)