Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii kwanza kukushukuru kwa kunipa nami nafasi ya kuchangia katika hoja zetu tatu hizi ambazo zinaendelea mezani, hoja ya Kamati ya PIC, PAC na Kamati ya LAAC. Nitajikita kwenye mambo mawili.

Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza nitajikita kwenye Kamati hii yetu ya PAC juu ya ukaguzi na hasara ambayo tumeipata kutokana na matumizi mabaya ya fedha za umma ninayo ripoti hapa ya Kamati kuanzia ukurasa wa 10 mpaka ukurasa wa 11 kipengele 2, 5, 1 kuhusu riba kuchelesha malipo inayotokana na kuchelewa kulipa wakandarasi katika Wakala wa Barabara TANROADs Billion 68.7.

Mheshimiwa Spika, nataka nijikite hapa, kutokana na taarifa ya Kamati inasema sharti la Kifungu cha 54 ya jumla ya mkataba wa ujenzi GCC kinatamkwa kwamba Mwajiri atamlipa Mkandarasi kiasi kilichothibitishwa na Meneja wa Mradi ndani ya siku 28 tangu tarehe ya kila hati ya malipo (Mikata ya Kimataifa ni siku Hamsini na Sita (56) kwa msingi huo Mwajiri akichelewesha malipo Mkandarasi atalipwa riba ya kuchelewa malipo katika hati ya malipo inayofuata.

Mheshimiwa Spika, sasa nikipitia hapa tunaona kwamba TANROADS wanetusababishia matumizi mabaya ya Fedha ya Umma kwa takribani billion 68.73 katika Mwaka huu wa Fedha 2021. Nimejaribu kupitia baadhi ya miradi nikawa najaribu kuangalia nikaona kwamba yapo matatizo na hususan ambao tumetokea kwenye ukandarasi huko tunajua. Kumekuwa na shida kubwa sana ya kupoteza fedha za umma lakini fedha hizi zinapotea kwa mipangilio mibaya tu. Sasa kama wanakubaliana au wanakosea kwa kutokujua sasa ndiyo nataka leo tuangalie hapa.

Mheshimiwa Spika, pesa zote hizi ambazo tunaziongelea hapa tunao uzoefu kwamba hakuna Mkandarasi wa ndani ambaye huwa analipwa hizi pesa, mara nyingi Mkandarasi wa ndani ukidai tu penalty kwamba umecheleweshewa malipo mradi unaofuata sehemu hiyo hutopewa mradi hata siku moja, experience tunayo lakini pesa zote hizi wanapewa watu wa nje, kwa sababu kwenye mkataba kuna sehemu ya kulipa riba lakini kuna sehemu ya kukata liquidated damage.

Mheshimiwa Spika, haiwezekani ripoti ya CAG inatuonesha kwamba TANROADs wamesababisha hasara hii kwakulipa riba lakini nowhere tunaoneshwa kwamba hata wao liquidated damage walikata wapi? Serikali peke yake ndiyo wanaokosea, lakini Mkandarasi katika Wakandarasi wote waliowalipa kwa sababu kulikuwa na miradi ya takribani zaidi ya Billion 600 ambazo walikuwa wanadaiwa lakini there is nowhere tunapooneshwa kwamba na upande wa Mkandarasi napo huwa kuna makosa. Kwa sababu kipengele cha kumtoza faini Mkandarasi kama liquidated damage kipo, kwamba na yeye anapochelewesha mradi unaanza kumkata baada ya siku kadhaa mpaka pale mradi utakapoisha au amount ile ya security ambayo ameiweka, lakini we don’t see that ila tunachokiona ni sehemu ile tu ambayo upande wa Serikali wanakosea.

Mheshimiwa Spika, kwa nini inafikia hatua hii? Kwanza iko tabia na mazoea yale ambayo tunayo sisi hapa, hakuna Mkandarasi anayefanya makosa. Mkandarasi akishaona tu muda wake wa ku-expire umefika kwamba mkataba unafika mwisho Mkandarasi anaandika barua ya kuomba extension, lakini upande wa Serikali hata humu ndani kuna Waheshimiwa Wabunge mnafanya biashara mnajua. Ukishampelekea certificate ya malipo wewe tena ndiyo unayetakiwa kugeukwa kuwa mtumwa kila siku kwenda kumbembeleza kama vile ile hela ni ya kwakwe mfukoni anakupa wewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa wenzetu wa nje hawafanyi hivyo. Wenzetu wa nje kwa sababu sisi tunapenda nchi yetu, tunapata kazi hapa lakini tunapenda nchi yetu hatutaki ugomvi wa kugombana na Serikali. Wakati wenzetu wa nje wakishapeleka certificate hatakupigia simu wala hakufuati yeye anakaa siku 56 zimeisha anasubiri, sasa mambo mengi tumeyaona ikitokea ziara ya Kiongozi wa Kitaifa hapo ndipo utakaposhangaa Mkandarasi anatafutwa kwa nguvu zote maana wanaona hela inaelekea huku, hata ile hela ambayo ulikuwa umeomba certificate haijaja mtu yuko tayari kukutumia hela leo halafu Kiongozi anaingia keshokutwa, matokeo yake akifika pale Wakandarasi wazawa tunaonekana kwamba tunalipwa pesa na hatufanyi kazi! lakini jiulize ile pesa imelipwa lini?

Mheshimiwa Spika, ndio maana mimi kuna rafiki yangu mmoja nakumbuka aliwahi kuwaambia hata pesa wasimuwekee kwenye akaunti maana aliogopa, unaletewe hela leo halafu Kiongozi anaingia keshokutwa, akiingia keshokutwa wewe ukikubali kwamba hela umeipokea kwenye akaunti kinachotokea ni nini? Anayesoma ripoti atasema Mkandarasi tumemlipa mpaka hapa lakini kazi haionekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa naongea hii generally tujaribu kuangalia jinsi ya kuondokana na haya. Tukikumbuka TANROADS wamekuwa na na tabia ya kutangaza miradi yao yote mwezi wa Julai, tunapoanza tu mwaka mpya wa fedha wanatangaza miradi yao yote, lakini tujiulize chanzo cha pesa za TANROADS ni nini? Tunazo pesa za Road Fund, tuna pesa za Hazina - Mfuko Mkuu wa Serikali na tunazo pesa za donors saa nyingine. Sasa unapotangaza miradi yote mwezi Julai kwa pamoja, miradi ya mwaka mzima, kinachokuja kutokea ni nini? Cash flow haiji kwa pamoja!

Mheshimiwa Spika, wale watu ukishawapeleka site kila mmoja anafanyakazi bila kumuuliza mwenzake umefikia wapi? Sasa unajikuta certificate zinafika mwisho kila mmoja ana madai na pesa ile haijapatikana au haijaonekana. Kwa hiyo the proper planning ambayo inabidi tufanye kama Bunge kuielekeza ni kwamba ili tuondokane na hizo hasara, kwa sababu Billion 68 siyo hela ndogo, hapo ungejenga kilometa 68 zingine. Unaongelea vituo vya afya zaidi ya 120, hii si pesa ndogo wanaenda kulipwa watu interest!

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi ukijaribu kuangalia pesa ya nje huwezi kuilipia interest tutalipa kwa kutumia pesa ya ndani, maana yake ni nini? Pesa yetu ile ambayo tumeikusanya kwa kodi na kwa taabu badala ingetusaidia hapa tunachukua kama penalty tunapeleka nje tena kwa Wakandarasi ambao wametoka huko nje waonatudai hizi penalty. Kwa hiyo, niombe Bunge tutoe maelekezo mahsusi, ni bora wakagawanya in quarterly basis, miradi wakaigawanya kama wana miradi mia mbili, ukafanya miradi hamsini ianze Mwezi wa Saba na miradi 50 ianze Mwezi wa Tisa, miradi hii iendane, iwe inapishana utakapoanza kupokea pesa, kwa sababu una uhakika hakuna Mkandarasi wa barabara ambae atafanya mobilizations afanye vitu vyote hivyo ndani ya mwezi mmoja au miezi miwili awe ameanza kudai certificate. Kwa hiyo, tukifanya hivi itatusaidia ku-save hizi pesa. Hivyo, mipango mibovu ya TANROADS imetufikisha hapa leo kutusababishia hasara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapoendelea kuyasema haya mipango mibovu ni pamoja na management nzuri. Tumeangalia hapa kwenye ripoti ya Kamati yako hii ya PAC ukurasa wa 22 inasema hivi, Taasisi kutokuwa na Bodi za Wakurugenzi. Tunajua TANROADS hawana Bodi ya Wakurugenzi leo ni takribani mwaka wa pili. Sasa jiulize taasisi hii tunaiendeshaje na haina Bodi ya Wakurugenzi? Imesemwa hapa kwamba complains hizi tunazozitoa hapa, ushauri tunautoa hapa unampelekea nani? Bado TANROADS huyu amerundikiwa majukumu mengi, tumesikikia jana hapa Waziri Mambo ya Viwanja vya Ndege baada ya watu kuongea hapa tangu juzi, akasema ooh! tutafanya adjustment! Unajiuliza kasema uwanja wa Msalato utaendelea kubaki chini ya TANROADS, nilikuwa najiuliza jambo moja hapa, Shule ya Msingi tukiwa tunasoma, tulikuwa tunafundishwa Wakala wa Barabara TANROADS, kazi yake nini? Kujenga barabara. Wakala wa Viwanja wa Ndege? TAA, Wakala sijui wa mambo ya Reli? TRL. Sasa tukianza kuchanganya haya mambo leo mtoto kesho na kesho kutwa miaka imepita, kwa sababu hivi vitu haviondoki.

Mheshimiwa Spika, nimeingia tu kwenye website uki- type pale Bajeti ya Mwaka gani unapata. Leo tuko na mtoto mmoja pendwa katika Wizara hii ambapo wote wapo chini ya Wizara moja. Lakini kuna mtoto mmoja ana mapenzi makubwa mpaka anapewa kazi za wenzake, bado tupo humu ndani ya Bunge tunaambiwa kwamba ataendelea na Kiwanja cha Msalato, sasa unajiuliza huyu mtoto mzuri namna hii kama Baba ni huyohuyo mmoja, kwa nini asiwaelekeze na wenzake wazuri wakafanya kazi zao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwangu mimi ninachokiona tusichanganye mambo haya. Hili Bunge limejaa wasomi, wewe mwenyewe ni msomi wa Degree Tatu za Sheria, hebu tuende sawa tunapofanya maamuzi kama Bunge tuweke legacy na heshima ya Bunge hili. Tuelekeze TANROADS waachie miradi ya Viwanja vya Ndege, iende chini ya TAA, kama kuna matatizo ya management Waziri ni yuleyule. Hata hivyo, kwa kukumbuka hapa Bodi ya TANROADS ninavyojua na ambavyo jinsi nilivyofuatilia hii ni advisory board siyo executive board, ndiyo maana wanaweza hata kupeleka vitu huko wakaingilia fanya kazi ya fulani, ikakubali fanya kazi ya fulani ikakubali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, unapoongelea Uwanja wa Ndege, unapokuwa unajenga uwanja wa ndege huongelei runway, runway ndiyo barabara. Uwanja wa ndege una vitu vingi, una majengo pale, ina watu wa umeme na nini, sasa unajiuliza TANROADS ni Mkandarasi ndani ya ile Wizara anayetakiwa afanye kazi za wenzake au TANROADS ni nani ndani ya ile Wizara?

Mheshimiwa Spika, hivyo ninaomba kama TANROADS ana cheti cha ukandarasi tukakutane naye site tushindane naye, lakini kama hana cheti cha ukandarasi, miradi ya viwanja vya ndege irudishwe TAA, kwa sababu hii Miradi inafanywa kwa standard. International Civil Aviation Organization wametoa standard za kujenga viwanja vya ndege. Sasa sielewi TANROADS ya Tanzania yenyewe mpaka inajua, kesho tutawakuta na kwenye reli hawa kama hatutangalia hapa, tutakuja kuambiwa TRL hawafanyi vizuri SGR ipelekwe TANROADS tena. Kwa hiyo, ninachoomba tusimame kwenye standard. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili ni Bunge la Wananchi wa Tanzania, kama ni Bunge la Wananchi wa Tanzania kila mmoja afanye kazi zake kwa mujibu wa Sheria maana hizi Organizations au hizi Taasisi zimetundwa kwa Sheria ya Bunge, tusizibadilishie matumizi kwa mtu mmoja kukaa na kuamua anavyotaka wakati vitu hivi vimetungiwa na Sheria na Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba juu ya hayo tuyaangalie ili yaweze kutusaidia, kesho na keshokutwa tutakapokuwa tunakimbizana na hasara kama hizi, huyu unayempelekea mpaka na viwanja vya ndege ametusababishia hasara namna hii na bado tunazidi kumrundikia kazi. Kwa hiyo, ningeomba tuliangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia najaribu kupitia hapa tena kwenye suala la miradi ambayo baadhi ya Wakandarasi wamepewa. Kuna Wakandarasi wametutoza penalty huko kwenye ile Billion 68, yet tumeenda na tumewapa na kazi nyingine kubwa tu wamesaini hivi karibuni na wanaendelea nazo. Sasa unajiuliza hawa Wakandarasi wa nje wana mapenzi gani na sisi? Wanatutoza penalty tunawalipa na bado tunawapa kazi nyingine wanaendelea nazo. Naomba tutoe kauli kwamba miradi hii ikae chini ya taasisi na hatimae iweze kufanyika, hata Watanzania wanapokosea au wanapocheleweshewa malipo na wenyewe pia walipe penalty kama hizi. Kwa sababu haiwezekani mtu anayetoka nje ya nchi tunampa pesa halafu wa ndani ya nchi tunamnyima.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana naunga mkono hoja. (Makofi)