Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia katika hoja ya Kamati zetu hizi tatu za PIC, LAAC na PAC. Kwanza ninakushukuru sana kwa vile umerudisha heshima ya Bunge hili, umekumbusha Watanzania wote kwamba Bunge hili lina meno na kwamba kweli kipindi hiki hatuna mchezo, kwa hilo unamuunga Mama Samia Suluhu Hassan mkono, kwa vile nakumbuka tulivyokuwa Tanga kwenye semina ya Polisi wakifundishwa mambo ya maadili ambapo CAG alikuwepo alimsifia sana CAG kwa kazi yake kubwa anayoifanya, alikemea sana Polisi wanavyofanya ubadhilifu wa fedha za umma na akakagiza kwamba kwa kweli taarifa za CAG zifanyiwe kazi.
Mheshimiwa Spika, kwa kutupa muda wote mrefu huu wa kuchanganua ripoti ya CAG tunakushukuru sana, maana tumeweza kuongea na tutaweza kuongea mengi. Ninakuomba kwa muhtasari kidogo kabla sijachangia nieleze Bunge lako Tukufu wajue kwamba kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2022 CAG alifanya kaguzi kwa jumla taasisi 331 za Serikali Kuu. Pia kwa upande wa mashirika ya umma alifanya ukaguzi mashirika 200 na pia alifanya ukaguzi wa ufanisi kwa taasisi12, jumla alifanya kaguzi 543. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimewaeleza hilo kwa kuzingatia kwamba Kamati ya PAC kwa nafasi ambazo tunapewa kisheria, tumeweza kupitia chini ya asilimia 10 ya haya mashirika yote, kwa hiyo niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba kwa nini ripoti ya CAG imetawanywa kwa kila mtu? Ni kwamba tupitie, tuangalie, tuhoji, ndiyo kazi ya Bunge hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, isionekane ni hii PAC, LAAC au PIC yenye jukumu lile, maana kama ni kupitia kila mahali basi ingebidi iwe kazi ya kila siku kama ambavyo nchi nyingine wanafanya. Mimi ni Makamu Mwenyekiti wa SADCOPAC, PAC’s zilizoko Kusini mwa Afrika, kuna nchi ambazo wao throughout wanafanyakazi ya kupitia kaguzi za PACs zao na kuhakisha kwamba wanamaliza taarifa za CAG na kuhakikisha kwamba wanazimaliza ndipo wazipeleke Bungeni.
Mheshimiwa Spika, kwa taratibu zetu mashirika ni mengi na najua kwamba kwa hilo kwetu itakuwa shida kidogo, labda hapo baadae Bunge lako Tukufu linaeza kutoa muda zaidi tukaweza kupitia mashirika mengi yenye utata.
Mheshimiwa Spika, baada ya kutoa hiyo background niseme tu kwa kifupi kwamba, kwenye ripoti yetu tuliyoitoa kwa ukaguzi uliofanywa na CAG kwa mwaka wa 2019/2020 ripoti yetu tuliyoileta Bungeni hapa mapendekezo yote tuliyoyatoa ambayo Bunge lako Tukufu liliyachukulia kama maazimio mengi hayakufanyiwa kazi, na mengi yamejirudia katika taarifa yetu hii, ndiyo maana unaona kigezo chetu kikubwa tunachoweka ni kupitia yale mashirika ambayo tungeweza kusema au zile taasisi tunazoweza kusema wanashingo ngumu. Bunge lako Tukufu linatoa maagizo hawayafuati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikizungumzia kwa mfano mwaka jana ripoti yetu ya TRA ilikuwepo, TCB, TIB yapo, TANROADS ipo, NFRA ipo, hapa tunayarudia tena.
Mengine hatukuweza kuyapitia kwa sababu gani? Kama ni occurrence imefanyika mara moja ile ina utaratibu wake mwingine lakini zile ambazo zimejirudia tunaona hao watu siyo wasikivu na hawako tayari kufuata maamuzi ya Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano, ukiangalia TRA kwa mwaka huu Juni 2021 wameshindwa kushughulikia madeni ya trilioni 7.5, mwaka jana walishindwa kushughulikia madeni ya Trilioni Tatu. Tuliwapa maagizo kwamba washughulikie madeni hayo, kama wenzangu waliopita walivyosema waliona kwani tusiposhughulikia tutafanywa nini? Hili Bunge si litasema tu halafu basi yanaisha? Ndiyo maana unakuta asilimia 95 katika mwaka mmoja ya kodi zile madai hayakufanyiwa kazi. Sasa swali tunalojiuliza hivi Serikali yetu itapata wapi pesa za maendeleo kama tunadai fedha Trilioni Saba kwa mwaka huu tunaozungumza? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukiangalia mapungufu katika mfumo wa i-tax (Income Tax Management System), Bilioni 11 hazikuweza kuwa captured. Na unaambiwa mfumo una matatizo na hili tulishawambia hata ripoti iliyopita kwamba, huu mfumo unatengenezwa na binadamu kaushughulikieni msipoteze kodi zetu. Wamekuwa na shingo ngumu leo tena tunayaona haya haya. Kwa hiyo ninachosema ni kwamba umeturudishia heshima yetu na nimesikiliza Wabunge wote wakiongea na kuonesha jinsi ambavyo kipindi hiki hakuna msalia mtume. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, TANROADS, kwenye Bohari, dawa zinaharibika, wazee hawapati dawa wakienda dispensaries, wanaambiwa hakuna. Tumeona yaliyofanyika kwenye fake VISA huko. Tumeona ujenzi wa vihenge ambaye anapewa Mkandarasi wa nje kana kwamba sisi hatuwezi kujenga vihenge na ameondoka na hakuna anachofanyiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo ukianagalia kumekuwa ni kwamba kumekuwa na dharau kubwa sana kwa upande wa wale wenzetu ambao walipewa jukumu la kugawa au kutengeneza miradi mbalimbali kwa manufaa ya nchi hii. Kwa hiyo, tuseme hivi kama wakati ule aliposema Hayati Baba wa Taifa kwamba sababu tunayo, Bunge hili tuna sababu ya kuwawajibisha hao watu nia tunayo na uwezo tunao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukuombe kama itakupendeza italetwa labda kwenye mapendekezo, tuna Kamati yetu ya Maadili, yale yote ambayo Waheshimiwa Wabunge ambayo wanayasema, nafikiri itakuwa wakati muafaka. Waitwe hawa hawa watu kwenye maadili wajue Bunge lina meno ili Bunge lako tukufu liweze kupewa ripoti kamili ya jinsi ambavyo ubadhilifu huu mkubwa wa fedha za umma umefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, namshukuru Mungu kwamba mimi nipo kwenye Kamati ile na Makamu wangu Mheshimiwa Hasunga pia yupo kamati ile. Kwa hiyo, tutatoa yote, maana tumepitia ripoti yote ya CAG ni kwamba hatukuweza kuifanyia kazi yote, lakini wote tumeisoma na tunajua madhaifu yaliyofanyika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nikuombe, mengi yameshazungumzwa na kazi yetu kubwa ni kwamba tutajua tulete mapendekezo gani katika Bunge lako Tukufu ili yachukuliwa hatua. Nisisitize kwamba, Mama Samia Suluhu Hassan, ambaye wakati wa Hayati Rais Magufuli, alikuwa halali anaamshwa usiku wafanye kazi; leo anakuwa Rais anafanya kazi, watu wachache wanchukua hela wanatia mfukoni halafu wanajua Bunge litatufanya nini. Uzuri Rais mwana mama, Spika mwana mama, Wenyeviti wa Kamati ya PAC na LAAC wana mama. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hatukosei, kama tumeweza kuwafundisha wanaume kuvaa suruali, tumevalisha nepi, tumewanyonyesha, tukawalea, leo tunashindwa kuwawajibisha. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)