Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali kuhusu Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Hesabu zilizokaguliwa za Serikali Kuu, Mashirika ya Umma na Kaguzi za Ufanisi kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Hesabu za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021, na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kuhusu Uwekezaji wa Mitaji ya Umma kwa Mwaka wa Fedha ulioishia Tarehe 30 Juni, 2021

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia jioni hii kwenye taarifa zilizopo mbele yetu kwa nia ya kutaka kulisaidia Bunge lakini pia kulisaidia Taifa letu.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee sana ninatoa pongezi kwa Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Chama cha Mapinduzi kikisimamiwa na Mheshimiwa Rais, Mama yetu Samia Suluhu Hassan ikiongozwa na Waziri wetu Mkuu, Mheshimiwa Majaliwa kwa kazi kubwa zinazofanyika Tanzania na maeneo mbalimbali kwenye Majimbo yetu na kila mtu anaona sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hii Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumepewa nafasi kubwa sana ya kuwasaidia Watanzania, kwa wale wapenzi wa mpira wa miguu wanafahamu kuna wakati wanafika wanasema the ball is on our court yaani ukifikia pale nusu ya pili ya kutaka kumaliza mpira na nyinyi ndiyo mnakwenda vizuri mnalazimika kumaliza vizuri. Nipongeze sana taarifa hii iliyoletwa hapa na CAG kwamba yeye ametimiza wajibu wake wote pasipo kuacha nafasi yeyote. Pia Kamati mbalimbali ambazo ripoti zake tunazijadili hapa leo na wenyewe wamefanya kazi yao nzuri sana, sisi wengine sio Wajumbe wa hizi Kamati ambapo ripoti zake tunajadili tunatoka kwenye kamati tofuti. Lakini tupo hapa na mimi nitatoa mchango wangu nikiegemea kwenye taarifa iliyoletwa na Kamati ya PAC.

Mheshimiwa Spika, bila kumung’unya maneno kabisa kwenye Kamati ya PAC kwenye ukurasa wake wa kwanza kwenye maneno yake ya utangulizi paragraph ya pili, wanasema hivi katika taarifa hii Kamati imebainisha maeneo kadhaa ambayo taarifa za CAG zimebainisha uwepo wa changamoto ya matumizi mabaya ya Fedha za Umma. Maeneo hayo ni pamoja na Serikali kupata hasara ya Shilingi ya Billion 68.73 ambayo ni riba zinazosababishwa na Wakala wa Barabara TANROADS, kwa hiyo hapa Kamati wameamua kuimulika wazi kabisa TANROADS na jambo hili lipo kwetu kama Wabunge na wewe ndiye kiongozi wetu.

Mheshimiwa Spika, tunao wajibu sasa wakumsaidia Mheshimiwa Rais, ripoti hii kuisaidia nchi hii pia, ripoti tunayoijadili tunategemea tuache yale mambo kama ambayo yalikuwa yanatokea labda tunaweza tukasema ya business as usual, tumepewa sasa nafasi yakusema wazi na ukweli na wewe kama Spika lazima uache historia ndani ya jengo hili, kwamba wakati wako uliitaka Serikali ilete taarifa ama za kuwawajibisha watu waliosababisha hasara hizi au wewe mwenyewe kuunda Tume Teule za kwenda kuchunguza maeneo haya yanayotajwa sana ndani ya ripoti ya CAG. Hii ndiyo namna pekee ya kuweza kulisaidia Bunge letu na kuweza kulisaidia Taifa letu pia lakuweza kumsaidia Mheshimiwa Rais, nikiangalia nia nzuri kabisa ya watu wa CAG wanataka kuona tunatoka hapa tulipokwama tunakwenda mbele.

Mheshimiwa Spika, kuna wakati fulani taarifa kama hizi zilizo wazi namna hii tulikuwa hatuzipati kila mara lakini leo taariafa inaeleza mapungufu makubwa haya tena tu kwenye baadhi ya maeneo ambayo yeye ameamua kuyataja na kuyakagua. Sasa kama hasara ya namna hii shilingi bilioni 68.73 inapatikana TANROADS peke yake, lakini TANROADS tunaamini wanayo Bodi, TANROADS ina viongozi wake wakiwemo Wakurugenzi Wakuu ambao bado mpaka sasa hivi wanatumikia nasi tuko hapa kama Wabunge, kwa niaba wa wananchi tunaona hasara hizi zinazoletwa na CAG amejaribu kufungua jicho lake na kutuelekeza mambo yanayotokea kwenye maeneo haya. Kwa hiyo, tusitoke hapa mikono mitupu. Hakikisha mambo haya yanakwenda kukomeshwa katika maamuzi yetu tutakayoyafanya ili siku moja tukumbukwe kwamba tulisaidia Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa SpikaNimetaja tu TANROADS peke yake lakini tunayo MSD, Mheshimiwa Tunza, jana wakati anachangia na yeye namshukuru kwa mchango wake mzuri, alieleza vizuri namna ambavyo MSD wameshindwa kutekeleza wajibu wao kwenye baadhi ya maeneo. Halmashauri yetu ya Wilaya ya Masasi DC peke yetu tuna karibia Shilingi Billion 180 ya dawa ambazo zinatakiwa zikateketezwe. Waliopeleka dawa hizi Masasi wanafahamika, waliokuwa wanazitunza kwenye bohari zetu wanafahamika. MSD bado ipo, Bodi ya MSD nayo bado ipo.

Mheshimiwa Spika, pia ukiangalia TPA kwenye taarifa ya CAG na pia kwenye taarifa hata hii ya Kamati na wenyewe wametaja, kuna ubadhirifu mkubwa uliofanyika kwenye Bandari ya Mwanza, kuna ubadhiru mkubwa uliofanyika kwenye Bandari ya Kigoma lakini pia na Bandari ya Mtwara kuna harufu za ubadhilifu. Sasa tuko hapa kusaidia kwa hiyo tunaomba wazi na tunaelekea mwishoni sasa kwa hiyo TPA nayo paundwe Tume au Kamati Maalum itayokwenda kufuatilia mambo haya ili tuweze Kwenda mbele kwa sababu kuna sehemu tumekwama. ATCL nayo imetajwa.

Mheshimiwa Spika, KADCO nayo Mheshimiwa Shangai, alichangia vizuri na ameeleza yeye anatoka eneo hili ni mtu anaefahamu vizuri historia nzima ya KADCO na mambo wanayoyafanya. Tuombe sana ili tuweze kusaidia nchi yetu tuondoke hapa tulipo simama.

Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine ambalo linasababisha labda wakati fulani hata inflation hii tunayoiyona tunaweza tukasema it’s a created inflation. Kuna suala la madai ya wakandarasi CAG nalo wameliangalia, mwaka 2017/2018 Wandarasi wa ndani walikuwa wanadai almost shilingi trilioni tatu. Mwaka 2018/2019 trilionI 2.7. Sasa hivi 2019/2020 wakandarasi wa ndani wanadai zaidi ya shilingi trilion 3.1. Tunaitaka Serikali ilipe madeni haya yatakwenda kusaidia kupunguza nakisi ya upandaji wa gharama huko nje kwa sababu maisha siyo marahisi tena kama ambavyo tulizoea.

Mheshimiwa Spika, vilevile tukumbuke Wakandarasi hawa na wenyewe wanakopa kwenye mabenki na kuna wanaofilisiwa huko kwenye mabenki wanapokopa ili kuendeleza hii miradi ya Serikli. Sasa kwa nini Serikali haitaki kulipa kwa wakati Wakandarasi wanapofanya kazi, hata kama wengine wameisha raise hizo certificate ili kuweza sasa namna ya kuona kuyafuta hayo madeni kwenye vitabu vya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mambo haya yanakwenda siyo hapo tu. Mpaka sasa CAG anao uwezo wa kukagua Taasisi nyingi za Serikali, lakini nitoe mfano mmoja ambao nasisi tunaona kuna haja au kuongeza wigo, kuna maeneo mengine yanakaguliwa na watu wa COASCO, kwa mfano niseme masuala ya ushirika wanaokagua kwenye hivi Vyama vya Ushirika ni COASCO. Hata hivyo mambo yakiwa mazito sana Serikali huwa inaweka mkono wake na ripoti za COASCO siyo kila mara na sikumbuki kama mara ya mwisho ni lini zililetwa hapa ndani kwa ajili ya kuzijadili.

Mheshimiwa Spika, hapa karibuni tumeona Serikali imekuwa na nia njema sana ikaunda Tume ya Kamati ya pamoja ya manunuzi ya pembejeo, kuna malalamiko makubwa kwamba pembejeo hizi kwa wakulima hasa nitoe mfano kwa wakulima wa korosho hazijawafikia ama kwa wakati lakini wakati mwengine haziwafikia kabisa au zimefika zikiwa chache kiasi wao wanaona ni bora tukarudi kwenye ule mfumo wa zamani Serikali ikitoa pesa basi waende kutumia kwenye ruzuku badala ya kutengeneza hiki kikundi ambacho wanasema ni Kamati maalumu, kumekuwa na ubadhirifu mkubwa sana, sasa tuombe badala ya ukaguzi wao kufanywa na CAG peke yake ikiwezekana ukaguzi maeneo haya ufanywe na Ofisi ya CAG badala ya kuachia hawa COASCO peke yao, ambao siku zote wamekuwa wanakaa na hawa watu wa vyama vya ushirika nakuona mambo wakati mwingine namna wanavyoweza kuyatengeneza ili yaweze kuwanufahisha wao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa namna hii ambavyo tunakwenda na Bunge tunakwenda sasa kuhitimisha nafikiri kesho tutakuwa tunahitimisha hoja zilizopo hapo hapa mbele yetu, niombe sana Kiti chako kiunde Kamati Teule kwenda kuchunguza maeneo haya ambayo Wabunge wote waliyosimama hapa wamechangia na wameyataja, ikiwemo MSD, TPA, TPDC, ATCL, KADCO pamoja na TANROADS tutakuwa tumetenda haki kwa ajili ya nchi yetu pia tutakuwa tumeweza kusaidia nchi yetu kuweza ku-move mbele.

Mheshimiwa Spika, kazi iliyofanywa na Kamati ya PAC, kazi iliyofanywa na LAAC vilevile na kazi iliyofanywa na CAG ni kazi nzuri sana kuacha zikaishia hapa katika sisi tu kuzijadili na hatua zake zisionekane. Aache historia katika Bunge hili na aache historia katika Nchi hii kwa kuelekeza Serikali katika kuhakikisha haya yanayotajwa, hasara zinazopatikana kwenye vyombo mbalimbali vya Serikali pia ubadhirifu unaotajwa waziwazi kwenye maeneo haya ushulikiwe, nasi tuweze kujisifia kwamba kuna wakati tuliweza kuisaidia nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, ninaunga mkono hoja ambazo zimeletwa hapa mbele yetu pia nisisitize kwa kifupi kwamba kuna haja ya kuunda Kamati Teule kuchunguza maeneo haya ili kuweza kusema ukweli yanayojili ndani kwenye vyombo hivyo.

Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa nafasi hii. (Makofi)