Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwanza kwakunipa nafasi niweze kuchangia hoja iliyopo mezani kwanza nianze kwa kuunga hoja zote tatu mkono.
Mheshimiwa Spika, vilevile nimshukuru na kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa namna ambavyo anaendelea kututumikia Watanzania na tunaridhika na kazi nzuri anayoifanya. Vilevile nitakuwa mchoyo wa fadhira nisipokushukuru na kukupongeza wewe kwa umakini, unaona kabisa kwamba kazi ya kuisimania Serikali kwa siku hizi mbili, tatu ukitoka nje ya Bunge lako hili wananchi wanaifurahia ni kwa sababu unatuelekeza vyema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba sasa nichangie kwenye hoja Mahsusi ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Mimi ni Mjumbe wa Kamati. Taarifa ya CAG inaonyesha dhahiri kwamba dosari zote za matumizi mabaya ya fedha za Serikali yanatokana na mambo matatu:
(i) Kutokuzingatiwa kwa Sheria ya Fedha za Umma;
(ii) Kutokuzingatiwa kwa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa; tunaijua wote Sheria Na. 9 Sura ya 283 ya Mwaka 1982 na marekebisho yake;
(iii) Kutokuzingatiwa kwa Sheria ya Manunuzi ya Umma. Hapo ndiyo msingi wa mambo yote ambayo Wabunge wako hapa wamekuwa wakiyachangia katika nyakati tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nilikuwa najiuliza, hivyo sasa kama Bunge lako linakaa hapa tunatunga Sheria nikawa najiuliza inawezekana kwa sababu siyo Mwanasheria lakini wewe ni mbobevu kwenye hili eneo, hizo Sheria tunazozitunga kwenye Bunge lako Tukufu hili hazitoi adhabu? Sheria zinapaswa kusimamiwa na tunajua asiyetekeleza jambo lolote kwa mujibu wa Sheria husika, kwa maana anayevunja hiyo Sheria anapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa maeneo ambayo yanaonekana hayaridhishi naomba tu niseme mifano michache. Kwenye taarifa ya CAG imeonekana matumizi ya fedha mbichi, fedha ambazo hazikupelekwa benki kiasi cha Shilingi Billion 17 ambazo hizo ni kwa Mamlaka 147 tu, kwa maana POS zimekusanya lakini hizi fedha zimetumika mbichi. Jambo la kusikitisha siyo kwamba zimetumika kwa shughuli za maendeleo, hazijulikani!
Mheshimiwa Spika, hiyo imethibishwa na baadhi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa zilizotokea mbele ya Kamati. Eneo lingine ni Matumizi ya Fedha za akaunti ya Amana. Akaunti ya Amana siyo akaunti ya matumizi kwa Halmashauri za Wilaya lakini inaonekana Jumla ya Shilingi Billion 9.74 kwa Halmashauri 81 haya matumizi yake hayakusimamiwa. Inasikitisha, Mkurugenzi mmoja wapo kwenye Kamati alipoulizwa kwa nini ulitumia fedha zilizopo kwenye akaunti ya Amana zaidi ya Million 95? Alijibu kwa jibu ambalo linasikitisha bila kuogopa akasema hizo fedha za Akaunti ya Amana hazina rangi kwani fedha zina rangi? Maana yake nini? Maana yake Maafisa Masuuli hawana uwoga na fedha za umma. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo lingine limetajwa sana, hivyo wakati Watanzania wengi wanalalamika kwamba hakuna dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya. Ukiangaria ripoti ya CAG kwa miaka mitatu mfulilizo jumla yake ni Billion 12.362, dawa ambazo zimekwisha muda wake kwa kipindi cha Miezi Mitatu mpaka miaka 20, madhara yake dawa hizi pia zikiingia kwa watumishi wasio waadilifu Watanzania tutapata madhara. Hata hivyo taarifa ya CAG inasema anaona mapendekezo yake aliyotoa kwa miaka mitatu mfululizo hayajafanyiwa kazi. Je, Bunge napo linapofanya kazi yake ya kuisimamia Serikali bado yasifanyiwe kazi? Hayo ndiyo maswali ya kujiuliza.(Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika ile Sheria ya Manunuzi malipo ya bidhaa za huduma ambazo hazikupokelewa Billion 8.44 kwa Halmashauri 61. Ununuzi wa bidhaa zenye thamani ya Shilingi Billion 7.93 kwa Halmashauri 42, pamoja na hasara zinazopelekewa kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka kwa baadhi ya Taasisi za Serikali kama vile Mfuko wa Bima ya Afya, MSD, GPSA, TEMESA na zinginezo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Tanzania kwenye maeneo mbalimbali kwa sasa wanalitegemea Bunge lako Tukufu. Wabunge wanafanya kazi yao ya kuisimamia Serikali, hivyo ninaungana na mapendekezo yaliyotolewa kwenye Kamati lakini na Wabunge kwamba ni wakati sasa wa kuhakikisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya wale wote wanavunja Sheria. Haiwezekani, kwanini tukae hapa Bunge litunge Sheria, lakini Sheria zinapaswa kusimamiwa, lakini ziwe zinavunjwa halafu hakuna hatua zinazochukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, zile Halmashauri chache tu ambazo zilitokea mbele ya Kamati inaonyesha kwamba ukiharibu Halmashauri ‘A’ unahamishiwa Halmashauri ‘B’. Ukiharibu Halmashauri ‘B’ unahamishiwa Halmashauri ‘D’, sasa huo utaratibu huo ndiyo unazozifanya Mamlaka za Serikali za Mitaa kuendelea kutokufanya vizuri, ni kwanini? Kwa sababu hawana woga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa je, tutaendelea kwa utaratibu huu halafu tutasema tunamsaidia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Hapana, inatosha! Kwa sababu, CAG ameonesha mapungufu hayo yote, na sisi tunayatambua hayo maeneo; jukumu letu hapa kwa kamati hizi na kwa taarifa hizi kwa kipindi hiki ni kuisimamia Serikali. Kwa hiyo, mimi nadhani naomba nisisitizwe, kwamba hoja za Wabunge walizosema, kwamba sasa Bunge liazimie katika eneo lolote ambapo sheria ilivunjwa hatua stahiki zichukuliwe. Kwa utaratibu gani, Bunge liielekeze Serikali kwa sababu, lina wajibu wa kuisimamia. Hiyo itatuepusha sisi kurudi hapa kuja kusema kila mwaka tunarejea kwenye hoja zilezile ambazo kimsingi hazionekani kurekebishika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ukiangalia kwa mifano hiyo unaona namna ambavyo Serikali inapata hasara. Sasa kumbe kwenye maeneo hayo yote iwapo usimamizi huo ungekuwa thabiti ina maana tungeweza kuikoa fedha ya Watanzania. Fedha hizi zingeweza kutoa huduma katika maeneo yetu mbalimbali tunayotoka na hivyo Watanzania pia wangeweza kuwa na amani.
Mheshimiwa Spika, lakini ukiangalia haya mapungufu ndiyo yanayowagonganisha wananchi na Serikali. Sasa mtu mmoja anapoamua kufanya hili huyo yeye achukuliwe hatua stahiki ili Serikali iwe salama kwa wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, na sasa ukiangalia mapendekezo ya CAG, ambapo kwenye maeneo mengi sana wajumbe wamesema, anashauri, anashauri; lakini kwenye maeneo mengine amebainisha kwamba mapendekezo anayatoa hayafanyiwi kazi. Tujiulize kuna nini? Hivi si kweli kwamba kuna eneo labda wale wanaofanya pengine kuna, mimi sijajua, lakini pengine kama Bunge tutafakari, kuna nini? Kwamba CAG anapotoa pendekezo, anaposhauri halifanyiwi kazi, mtu anahamishwa kutoka Point A kwenda Point B akaendelee kuharibu; kuna nini? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa wengine wanaweza wakatoa majibu ya haraka tu, hayo hayahitaji chuo kikuu. Mwingine atasema labda kuna kulindana, mwingine atasema labda sijui ni nini, labda ni mtoto wa fulani.
Mheshimiwa Spika, sasa sisi hapa Wabunge ni wawakilishi wa wananchi. Sisi hatuna cha mtoto wa shangazi, hatuna cha mtoto wa mjomba, sheria ifuate mkondo wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaunga mkono hoja nikiamini kwamba hayo yote yatafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Spika, lakini kabla sijamaliza, yale mapungufu yote kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuna Sekretarieti ya Mkoa pale. Mimi ninaomba niwashawishi Wabunge moja ya azimio liwe Serikali ifanye tathmini ya kina nini kazi inafanywa na Sekretarieti za Mikoa? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu, wakuu wa section wapo hapo, inakuwaje mpaka mwaka unaisha ndipo kunaonekana madudu mpaka CAG anaenda kufuatilia, wakuu wa section wapo? Wanasubiri Mkuu wa Mkoa aende kwenye ziara? Wanasubiri Waziri aende kwenye ziara? Wana jukumu gani pale? hilo ni suala la kufanyiwa tathmini ya kina. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.