Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mwera
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ZAHOR MOHAMMED HAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi. Pia naomba kuwashukuru wenzetu wa Kamati zote tatu kwa taarifa nzuri zilizo chambuliwa kutoka kwenye taarifa ya CAG ambayo imewafanya Wabunge waweze kuzisoma na kuzielewa taarifa hizi vizuri kabisa. Kwa sababu volume ni kubwa lakini wamefanya kazi kubwa sana wenzetu wa Kamati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pia nataka kuishukuru Serikali, mwenzangu mmoja amezungumza hapa kwamba kwa kawaida taarifa hizi huwa hatuzipati mapema, halafu tukazipitia, kuzichambua na kuzichangia. Hii inaonesha ni jinsi gani Serikali yetu imeamua kwa makusudi kuheshimu misingi ya sheria.
Mheshimiwa Spika, naomba nichangie katika maeneo mawili; eneo la kwanza ni la PAC, lakini eneo la pili ni LAAC.
Mheshimiwa Spika, wamezungumza wenzetu wengi sana hapa juu ya upotevu wa fedha za Serikali. Wenzetu wamezungumza hapa kwamba TANROAD imetutia hasara ya Shilingi bilioni 68.7. Vile vile kwenye ujenzi wa vihenge, NFRA tumepoteza Dola milioni 33. Kwanza naomba hapa tuelewane. Unapozungumza Dola milioni
33 unaweza ukaona kama ni kitu kidogo hivi, lakini ukizigeuza Dola milioni 33, tunakaribia kwenye Shilingi bilioni 72 na kitu. Kwa hiyo, tusichukulie kama ni fedha ndogo, ni nyingi sana ambazo zingeweza kusaidia kwenye majimbo yetu.
Mheshimiwa Spika, kuna fedha nyingine hapa, amesema kaka yangu Mheshimiwa Maganga, kuhusu upotevu wa Dola milioni 153.4. Hizi ni fedha nyingi. Tunazungumzia karibu Shilingi bilioni 300 na kitu zimepotea na hazina maelezo. Vilevile wako wajanja hapa wengine, mwaka 2021 lilipoungua soko la Kariakoo, tumeambiwa kwamba shilingi bilioni 3.56 hazijulikani zilipo na hazina maelezo. Halafu, taarifa itoshe hivyo, haiwezekani.
Mheshimiwa Spika, pia tumeambiwa kwenye DART kuna malipo ya usumbufu. Haiwezekani kwenye Taifa hili lenye Wabunge walioteuliwa wakachaguliwa na wananchi halafu mambo yakaenda kawaida tu. Siyo Bunge hili. Bunge hili limekuja kwa asilimia kubwa na wengi hapa na wengi wetu tunasimamia Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi. Moja katika ahadi zake CCM ni kupambana na mambo ya ubadhirifu wa fedha za Umma. Bunge hili ni lazima tuchukue hatua na lazima Chama chetu kilichotutuma kijue kwamba tumekuwa wakali kwenye hili. Kwa hiyo, asiondoke mtu kama ni business as usual. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukiangalia kidogo kwenye LAAC, wenzetu wa Kamati wanasema wametuletea taarifa hii ili kutushawishi. Naomba ninukuu: “Lengo la taarifa hii ni kulishawishi Bunge liafiki ushauri wa Kamati wa kuitaka Serikali ichukue hatua.”
Mheshimiwa Spika, jana ulisema hapa, ulitupa moyo sana, kwamba kuna wakati wa kushauri na wakati wa kusimamia. Sasa hivi tunataka kusimamia kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza maelekezo na maamuzi ya Bunge hili. Kwa sababu hii ni mihimili mitatu; mhimili huu ndiyo unasimamia Serikali. Kwenye hili, wenzetu wa Kamati wala msipate taabu, siyo kazi yenu kutushawishi. Mmeweka facts kwenye meza, zimeonekana, na hizi mmezitoa kwenye taarifa ya CAG, tunawashukuru na tunakubaliana na ninyi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa sababu wenzetu wamesema, naomba kidogo niipongeze Serikali kwamba angalau imefanya kazi kubwa; ukilinganisha miaka ya nyuma na ya sasa, wanasema kwamba, katika maeneo ya halmashauri zilizofanyiwa utafiti, zilizokaguliwa ni halmashauri 178 ambazo ni sawa na asilimia 96.2, hii ni hatua kubwa sana. Naomba niipongeze Serikali lakini tuendelee, kwa sababu tunahitaji mia kwa mia, kila aliyepewa pesa zetu ni lazima akaguliwe, kwa sababu hii siyo option, ni lazima. Kama kuna upungufu wa watenda kazi, tunaomba wenzetu Serikali ahakikishe kwamba wataalam wa ukaguzi wanafanya kazi yao, kwa sababu hao wenzetu wameona upungufu kwenye maeneo kumi.
Mheshimiwa Spika, nitataja machache tu, kwanza, anasema, ni upungufu kwenye mifumo. Mifumo inatengenezwa na kudhibitiwa na binadamu. Mifumo hii inakuwaje? Maana yake huu ni mkakati wa makusudi kuhakikisha kwamba fedha zinapita lakini katikati wako wajanja wanazichezea. Mifumo ni ya kwetu na wataalam tunao inakuwaje kuna kuchezewa kwenye mifumo?
Mheshimiwa Spika, vile vile wanasema kwamba kuna dosari kwenye matumizi na makusanyo. Tunaweza kufanya dosari ndogo kwenye makusanyo lakini kwenye matumizi hatuwezi kusema ni dosari bali ni makusudi. Kwa sababu tunapotumia tunazo Sheria za Fedha ambazo ndizo zinazotuongoza. Tuna Sheria za appropriation ndizo zinazotuongoza, tunakoseakoseaje? Wenzetu wamesema hapa kwamba ni mkakati wa makusudi kwa sababu sheria zimeonekana zina upungufu, wataalaam wanazijua, wanazichezea. Kwa hiyo, ningeomba hili kwa Wabunge wenzangu tukubaliane na mapendekezo ya Kamati kwa sababu Kamati ilifanya kazi kwa niaba yetu. Sasa sisi ni wajibu wetu kama Bunge kufanya maamuzi.
Mheshimiwa Spika, anasema kuna matumizi mabaya ya shilingi bilioni 9.74, amana za halmashauri. Sasa kwenye akaunti za amana bilioni 9.74 zinapoteapoteaje? Mbona hapa Kiswahili hakieleweki? Tokea tarehe Mosi Julai mpaka tarehe 30 Juni ya kila mwaka tunapoteza kwenye akaunti hii tu bilioni 9.74 kwenye akaunti nyingine ambazo hatuna taarifa nazo inakuwaje? Kwenye hili, pamoja na kwamba wenzetu tunawakubali wanafanya kazi, lakini waongeze kasi kwenye hili. Wenzetu wanafanya kazi kwa sababu wameona kuna upungufu kwenye sheria zetu.
Mheshimiwa Spika, naomba nielekee kwenye ruzuku za miradi ya maendeleo. Ukiangalia pale kwenye pesa za ruzuku zinazokuja kwenye halmashauri utagundua mambo yafuatayo na Kamati imetusaidia. Kuna halmashauri ambazo zimepewa zaidi ya asilimia 52 ya fedha ambazo zimeidhinishwa na Bunge. Ukiangalia kwenye mtiririko wa jedwali lile namba moja, utakuta kwamba kuanzia mwaka 2017 hadi mwaka 2021 kuna halmashauri zimeongezewa 52% ziada.
Mheshimiwa Spika, suala langu liko hapa, Bunge hili tunakaa miezi mitatu kwa ajili ya kupanga bajeti, kuangalia maeneo gani tupeleke, maeneo gani tupunguze, tukimaliza tunaidhinisha ziende. Kama kuna dharura ni wajibu wa Serikali kutuita Bunge hili kwamba kuna fedha za ziada. Sasa naomba wenzetu watusaidie, unawezaje kuongeza mahali 52% ziada tena sio Sh.2000/=. Kwa mfano, kwenye jedwali namba moja, utakuta ziada ni Shilingi 41.787 bilioni, nani katoa kibali hiki? Mwingine amepewa ziada ya 30% Shilingi bilioni 20, nani katoa mamlaka ya hili? Kwa sababu mamlaka inayoidhinisha fedha ni Bunge hili. Sasa nadhani wenzetu waje watusaidie hapa, kwa sababu kwa kawaida kama kuna bajeti ya ziada ni Bunge hili ndilo linaloombwa.
Mheshimiwa Spika, naomba nirudi pale, nilisema kama Mabunge mawili yaliyopita hivi, kwamba tunalo tatizo kwenye sheria zetu na nilishauri na naomba niendelee kushauri kwamba, Bunge hili bado halijafanya kazi yake. Kuna kitu kinaitwa Appropriation Committee, Kamati hii ndio inatakiwa ifanye kazi mkono kwa mkono na Serikali ili kile kinachokusanywa kipelekwe kwa maelekezo ya Bunge hili si vinginevyo. Hatuwezi tunakutana hapa tunapanga, tunaamua, halafu mwingine kwa matashi yake tu anaamua wakati Bunge lipo na linaweza kuitwa wakati wote kama kuna dharura likafanya maaamuzi. Halafu mmoja anamua kwa sababu sheria zina nafasi, zinamruhusu au sisi kama Wabunge hatujaamua kufanya kazi kama wabunge?
Mheshimiwa Spika, ukienda kwenye ukurasa wa 11 kuna vitu vidogo sana, ukivisoma unaviona ni vyepesi sana. Anasema, ununuzi bila idhini ya bodi zinazohusika. Bodi za zabuni, watu wametumia shilingi bilioni 7.9, tuko wapi? Bunge liko wapi? Hao wenzetu wa Serikali wako wapi? Fedha hizi zinapotea mpaka tunakuja kuletewa taaarifa na CAG sisi kazi yetu nini?
Mheshimiwa Spika, ununuzi usiozingatia mpango wa manunuzi. Tumepoteza shilingi bilioni 3.84 kwenye halmashauri 24. Hii ni aibu kwetu. Narudia ni sisi kama Bunge hatujafanya wajibu wetu, ndio maana watu wanaona Bunge liko legelege, kwa hiyo wanaweza wakalichezea tu. Hili sio Bunge legelege. Hili ni Bunge ambalo likiamua kufanya maamuzi linafanya. Kwa hiyo ningeomba tufanye maamuzi ili kila mtu akae kwenye mstari wake.
Mheshimiwa Spika, naomba sana, kuna mtu mmoja anasema amelipa malipo ya ununuzi bila ya kuzingatia taarifa za mapokezi. Huyu amepoteza shilingi bilioni 2.02.
Mheshimiwa Spika, naona tabu hata kutaja hizi namba kwa sababu ni kama vile unajichoma kisu. Maana yake ni dhambi yetu sisi kama Wabunge. Sasa ningeomba niseme haya kwa sababu ni mengi sana. Kule kwetu Waswahili husema mchelea mwana kulia, hulia mwenyewe. Sisi hapa wengi wetu tumeletwa kwa heshima na kibali cha Chama Cha Mapinduzi lazima tukithibitishie Chama chetu kwa sababu Serikali ina wenyewe. Wenye Serikali hii naomba niseme kwa sasa ni Chama Cha Mapinduzi. Haitozidi mwezi mmoja tutakwenda kuulizwa pale mlitusaidiaje kama Chama cha Mapinduzi kuisimamia Serikali? Kwa sababu Serikali ni ya kwetu na chama kimetuingiza kwenye Bunge hili ili tuisimamie Serikali. Sasa ningeomba kushauri haya yafuatayo; pamoja na mengine waliyoshauri wenzangu nakubaliana nayo.
Mheshimiwa Spika, jambo la kwanza, kwenye PAC na LAAC; ningeomba tuhakikishe kwamba uchunguzi wa kina unafanyika ili kila aliyehusika abebe msalaba wake.
Mheshimiwa Spika, kwenye manunuzi, waliohusika sheria zitumike kwa sababu hawa ni watendaji wetu. Sheria zipo wanazijua, kanuni zipo wanazijua lakini kwa sababu wanajua loophole za sheria, wanafanya wanavyotaka. Kwenye hili naomba sheria, kanuni na taratibu kwa watumishi hawa zifanye kazi wala tusioneane huruma.
Mheshimiwa Spika, mwisho, ningeomba tupitie upya Sheria ya Manunuzi inayoonekana ni dudu lisilowezekana. Sheria ya Manunuzi inatuumiza sana. Kama mtakumbuka miaka michache nyuma, alikuwepo Rais wetu aliyetangulia, Mheshimiwa Jakaya Kikwete alisema Sheria za Manunuzi zina mapungufu mengi, mtu anaweza akafanya mazuri lakini sheria ikamkamata kwa sababu hakufuata taratibu na mtu anaweza akafanya madudu lakini kafuata sheria, huyo anaweza akawa free. Naomba tupitie sheria zetu za manunuzi.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)