Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KHADIJA HASSAN ABOUD: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza napenda kuwapongeza Kamati zote tatu zilizotuletea ripoti zao hizi pamoja na ripoti ya CAG. Kwa kweli wamekaa na kuchambua na wametulea vitu ambavyo tunaweza kujadili asubuhi hii ya leo. Naunga mkono hoja za kamati zote tatu.
Mheshimiwa Spika, mimi nitajielekeza kwenye kipengele ambacho kinahusu fedha za dharura ambazo zinatumiwa na halmashauri pale ambapo kunatokea majanga, maafa na maradhi ya mlipuko.
Mheshimiwa Spika, inapotokea maradhi ya mlipuko hayana dakika wala saa; lakini wanapoomba vibali halmashauri Wizara husika inachelewa sana kutoa majibu ya vibali vile na hapo inasababisha wavunje sheria kwa kutumia fedha ambazo hazikuidhinishwa.
Mheshimiwa Spika, hoja yangu hapa, ili kuepusha isiwe kichaka cha upotevu wa fedha nyingi cha kutumia kipengele cha kwamba maradhi ya mlipuko au majanga na maafa Wizara iandae aidha, kitengo maalum au wahusika maalum ambao watapokea barua na watafanyia kazi kwa haraka kwa dharura iliyojitokeza ili kuepusha matumizi ambayo hayakuidhinishwa na au kuwa, kama nilivyosema mwanzo, kuwa kichaka cha utumiaji wa fedha za umma bila matarajio yaliyokusudiwa.
Mheshimiwa Spika, hapa inakuja hoja, je tusubiri kibali cha matumizi au tuachie watu wafe? Sasa inapokuja hoja kwamba tuwaachie watu wafe ndipo halmashauri na wahusika kutumia fedha bila kupata kibali. Hili suala lina hoja nzito kwa sababu huwezi kuwaacha watu wakafa wakati fedha unazo lakini fedha hizo ni madhumuni ya watu walewale ambao unatakiwa kuwaoongoza lakini wakifa wote unaomuongoza nani? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikijielekeza kwenye mchango wangu kuna ripoti ya CAG kuna hasara ya shilingi takriban milioni 56 ambazo wamelipwa watumishi hewa, watumishi waliostaafu, watumishi waliokufa na watumishi ambao hawapo kazini kabisa. Hapa ni upotevu mkubwa wa fedha za umma ambazo zinahitaji fedha zile zielekezwe katika kutumia fedha hizi katika mambo mengine ambayo yanahusu maendeleo ya nchi, ya wananchi na watumishi wengine.
Mheshimiwa Spika, nikiunganisha hapo hapo kwenye suala la watumishi, kwenye ripoti ya CAG kuna madeni ambayo yanahusu bilioni 160 ambayo hawajalipwa watumishi, pamoja na milioni 96 ambazo ni posho na mengine haya kwa ajili ya watumishi ikiwemo uhamisho, likizo na vitu vingine. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, watumishi hawa ndio tunawategemea wasimamie fedha zetu, watumishi hawa ndio tunategemea wakakwamue maendeleo ya wananchi na wasimamie fedha na maendeleo ya wananchi. Lakini tunapowavunja moyo na kuwakatisha tamaa, malimbikizo mengine yanafika miaka kumi, mitano, sita mpaka mtumishi anakufa mrithi wake anakufa fedha hizi anapewa nani? Anakuja kupokea mtu ambaye hausiki kabisa hajamsaidia lolote yule mtumishi aliyetumia nguvu zake.
Mheshimiwa Spika, ukiwahoja halmashauri ni mkakati gani ambao wameweka kulipa watumishi hao mabilioni haya wanatenga fedha kidogo sana ambazo kwa kutenga fedha hizo inaweza ikachukua muda mrefu, takriban miaka kumi hajamaliza madeni.
Mheshimiwa Spika, tutafute hatua za haraka na dharura ili kuhakikisha tunapunguza angalau nusu ya madeni ya watumishi wetu ili watumishi hawa wasitumie fursa hii ya kuhujumu kwa sababu hawalipwi likizo, uhamisho, mishahara, na matibabu. Sasa ili wasihujumu, wasifiche mapato wafanya kazi zao kwa weledi na kwa uaminifu na wao stahiki zao zinatakiwa zilipwe kwa wakati. Wajibu unaendana na haki. Sasa, sasa, ili atekeleze wajibu wake mtumishi apate haki zake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naendelea. Kuna uvujaji mkubwa wa mapato katika halmashauri ambako hawakusanyi mapato kutoka kwenye vyanzo vingi, na hapa kuna upotevu mkubwa wa fedha za Serikali na fedha za umma. Kwa mfano kuna ushuru wa mazao, chanjo na machinjio ambako zaidi ya bilioni 14 hazikukusanywa kwenye baadhi ya halmashauri; tumeikuta katika ripoti ya CAG.
Mheshimiwa Spika, huu uvujaji wa mapato au kutokukusanya mapato kunaitia hasara kubwa Serikali, kwa sababu haya mapato tunayotaka kuyakusanya ndiyo tunatakiwa tuwalipe watumishi, tulipe vikundi, kufanyia shughuli nyingine za maendeleo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikiongezea hapo hapo kwenye ukusanyaji wa mapato, mfano ukusanyaji unaohusiana na kilimo, mifugo na uvuvi ndani ya halmashauri watenge percent ambayo itasaidia kuendeleza zile sekta, tuziziachie Wizara peke yake. Kule kuna uvuvi, kilimo, ufugaji, zitengwe fedha kwaajili ya kuongeza majosho, kusaidia uboreshaji wa kilimo na mabwawa. Hii ni kwa sababu ndio ushuru wa kilimo chenyewe au uvuvi na mifugo yenyewe. Kuonekane basi kuna faida kuendeleza kile kilimo katika ile halmashauri kwa sababu wanachukua fedha kutoka kwao hayo ni maoni kwa sekta zinazohusika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niendelea, kuhusu mfuko wa wanawake, vijana na wenye ulemavu, hili ni takwa la kisheria kupeleka 4:4:2, lakini baadhi ya halmashauri hawafikishi hiyo asilimia kwa hivyo vikundi, na inasababisha sasa kuzorota kwa ile azma ya Serikali ya kumkomboa mwananchi kiuchumi na kupunguza umaskini wa kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika hii mifuko kuna takriban bilioni 47.01 hazijakusanywa kwenye mamlaka 155, bilioni 47 hazijakusanywa kwenye mamlaka 155.
Mheshimiwa Spika, hapa inabidi tutafakari na tujiulize; kweli fedha hizi zitapatikana? Waliohusika na kupewa hiyo mikopo wapo? Hivyo vikundi viko? Uhakiki umefanyika ili kuhakikisha vikundi hivi viko hai na vinafanya uzalishaji? Kama vinafanya uzalishaji na havirejeshi mikopo basi ni suala letu sisi wahusika kufuatilia hiyo mikopo. Lakini kama baadhi ya vikundi havipo ni kwamba tuna haja sasa ya kuhakikisha fedha hizi zinakwenda kwa walengwa husika ambao wana miradi mahususi ya uzalishaji ili fedha hizi zirudi zikasaidie wengine katika kujikwamua na umaskini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa mfano halmashauri badala ya kuwapa fedha wahakikishe vile vikundi wanavipa ujuzi kwanza ndipo baadaye wanavipa vifaa na vitendea kazi. Wavisimamie ili kuhakikisha wao wenyewe wananufaika lakini na Serikali fedha zake zinarudi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hapo kuna baadhi ya halmashauri hawapeleki ile asilimia 40 na asilimia 60 kwenye miradi ya maendeleo. Hili ni takwa la kisheria, inatakiwa fedha ziende kama ilivyotakiwa ili kuimarisha miradi ya kiuchumi na miradi mingine ya kijamii katika halmashauri zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nikimalizia la mwisho nakuja kwenye uhaba wa watumishi, uhaba wa watumishi umejitokeza katika sehemu nyingi za halmashauri zetu. Hapa nitoe rai. Halmashauri itenge fedha za kusomesha na kuwajengea uwezo wale watumishi waliopo, wasisubiri tu uajiriwe na Serikali kuu ilete kwa sababu wao wana fedha na wana watumishi. Kwa mfano, kwenye sekta ya hesabu na sekta ya mambo ya kimtandao (TEHAMA). (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sekta hizi mbili ndiyo zinachangia sana kwenye uvujaji na upotevu wa mapato katika halmashauri, tukiweka wataalam, halmashauri ikiwa na mpango mkakati wa kusomesha watu wake wale wale walio ndani ofisini kuwajengea uwezo watu wa hesabu na TEHAMA hakutakuwa na upotevu na ubadhirifu mkubwa wa fedha wataweza kuweka hesabu zao sawa na kujua wanafanya nini.
Mheshimiwa Spika, naipongeza sana Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi, nampongeza Mheshimiwa Rais, anajitahidi sana kuhangaika huku na kule kutafuta fedha kwa ajili ya wananchi wetu. Ni wajibu wetu sisi tumuunge mkono kuhakikisha fedha hizi zinatumika ipasavyo ili kuwaletea wananchi wetu maendeleo, na kuwapunguzia upungufu na umaskini wa kipato. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata nyumbani kama unahangaika kuomba, kukopa, unachuna uso unakwenda kwa ajili ya watoto wako, lakini watoto wakawa wanaharibu, hawatumii ipasavyo roho yako inanyonga, inaumia na inachukia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuwaunge mkono viongozi wetu wote waliopo madarakani kwa kuhakikisha kwamba tunawasaidia katika kuokoa fedha na katika kuwasaidia wananchi kuwaletea maendeleo.
Mheshimiwa Spika, ahsante, nakushukuru na naunga mkono hoja zote. (Makofi)