Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niwe sehemu ya kuchangia taarifa hizi tatu za Kamati zetu. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa fursa ya kuwa mzima na kuweza kusimama ndani ya Bunge lako Tukufu. Nizipongeze Kamati zote pamoja na Wenyeviti wa Kamati kwa kuwasilisha taarifa zao vizuri ndani ya Bunge letu hili.
Mheshimiwa Spika, kipekee nikupongeze Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kuweka rekodi mpya ya namna Bunge lako linavyojadili ripoti hizi ni mwaka huu tarehe 16 Februari, 2022 siku moja tu ilitumika kujadili ripoti zote hizi tatu, lakini mwezi huu Novemba kwa maboresho kidogo na kwa ridhaa yako Bunge lako linatumia siku nne kujadili ripoti hizi tatu inaonesha ni namna gani tunakwenda kuweka Bunge la Kumi na Mbili, pengine Mungu atajalia litaweka historia ya kuisimamia Serikali kwenye mapato na matumizi ya fedha ambazo zinaidhinishwa na Bunge hili.
Mheshimiwa Spika, nimpongeze pia Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla kwa kazi nzuri inayofanyika ambayo inaonekana waziwazi kwa taarifa ya utekelezaji wa bajeti iliyoishia Juni, 2022. Taarifa ile ilionesha Serikali ilikusanya zaidi ya 95% ya mapato ya ndani trilioni 24.3, taarifa ile ilionesha kuna ongezeko la zaidi ya trilioni 3.8 kwa bajeti iliyopita iliyoishia Juni, 2021, lakini taarifa hii ilionesha kwamba pesa nyingi zimepelekwa kwenye miradi kutokana na mapato ya ndani zaidi ya tirioni 11.55, 99.7% na ni kwa mara ya kwanza imevuka lengo hilo na ukilinganisha na trilioni 8.34 zilizopelekwa mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2021.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri hii ndio maana naifurahia hatua yako hii, tusipoweka msingi imara wa kuisimamia Serikali tutakwenda kushuhudia upungufu unaoendelea kujitokeza kwenye Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na hapa nimpongeze kwa dhati kwa kazi yake nzuri. Mwezi Agosti mwishoni uliruhusu Kamati zako nne ya PAC, PIC, LAAC na Bajeti kupewa semina na Taasisi ya Wajibu ambayo ilihusu ripoti ya uwajibikaji. Katika ripoti hiyo ilifanya kazi ripoti zote za CAG na taarifa yake ni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hoja zote za CAG, ziwe za mapato, ziwe za matumizi, ziwe za manunuzi na yote, zote zile ukizisoma zina viashiria vya rushwa, udanganyifu na ubadhirifu na ndio maana taasisi hii inayoongozwa na CAG mstaafu Ndugu Ludovick Uttoh ilifanya tathmini ifuatayo: -
Mheshimiwa Spika, kwa viashiria vya rushwa, udaganyifu na ubadhirifu ambao taarifa hii ni kwa ajili ya CAG kwa mwaka 2018/2019 ilikuwa jumla ya bilioni 232.5. Kwa mwaka 2019/2020, ilikuwa jumla ya tirioni 1.77. Kwa mwaka 2020/2021 viashiria hivyo kwa ripoti ya CAG ni trilioni 4.5, zaidi ya 15% ya matumizi yote ya trilioni 31.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo ni ongezeko la 159% kutoka mwaka wa fedha 2019/2020 ambao kiuhasibu tunaita yote hayo ni nugatory expenditure na ni viashiria gani? Ni mapato kutopelekwa benki, kukosekana kwa hati za malipo, kutumia hundi za malipo zilizoghushiwa, kufanya malipo kinyume na matakwa ya Sheria Kanuni na Taratibu za Manunuzi, malipo ya huduma au bidhaa ambazo hazijapokelewa, malipo kwa watumishi hewa, malipo kwa Wakandarasi ambao hawajulikani.
Mheshimiwa Spika, hakuna taarifa yoyote ambayo itapelekea matumizi haya au hoja hizi ni rushwa, ubadhirifu na udanganyifu. Katika vigezo vyake alivyotumia katika hiyo taarifa ya wajibu ambayo imesambazwa katika taasisi mbalimbali za ndani na za nje na Mabalozi mbalimbali inaonesha kwa mwaka 2020/2021, kati ya viashiria vya trilioni 4.9, viashiria vya upotevu wa mapato ni trilioni 1.8. Viashiria vya matumizi ya kawaida, usimamizi wa mishahara, mafao na rasilimali watu trilioni 1.1, viashiria vya matumizi ya Mikataba kinyume cha taratibu na kanuni ni trilioni 1.6. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika mapendekezo ya Kamati na maazimio ya Bunge naomba mimi binafsi nishauri azimio lingine mojawapo. Ikikupendeza, kwa kuwa tunataka tuweke rekodi na kwa kweli inaonekana ni dhamira ya Serikali yenyewe tupendekeze kuundwa kwa Kamati Teule ya kuangalia kwa nini kunakuwa na ongezeko la hoja za ukaguzi. Sitaki kuamini wataalam ndani ya Serikali ni wengi, Wahasibu waliosoma, wenye CPA, wenye MDA, Maafisa Masuuli lakini ongezeko la 159% la mapungufu ya usimamizi wa fedha ya mapato na matumizi kutoka trilioni 1.7 mpaka trilioni 4.9, inataka Kamati Maalum ya kuyapitia hayo na kujua kulikoni.
Mheshimiwa Spika, haiyumkiniki, ukaguzi siyo kuviziana, mimi nilikuwa Mkaguzi wa Hesabu, unaingia, unaitisha kikao, unawambia utaenda maeneo gani, utatumia sampling ya aina gani. Unamaliza, unaitisha kikao unawaambia haya niliyoyaona, unarudi ofisini, unaandika management letter, unawapelekea, wanapewa siku 21 wajibu, unapoona kimya hizi zilizowasilishwa hapa hawakuwa na majibu. Iweje inapowasilishwa kwa Mheshimiwa Rais anaiwasilisha Bungeni, zinavyoanza Kamati ndio majibu yanapatikana, huo wote ni ufisadi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa naomba niende kwenye Kamati ya PAC, pamoja na mapendekezo ya maazimio ya Bunge, naomba niongeze azimio mojawapo namba
3.3 kuhusu ukaguzi maalum. Kwa kuwa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali upande wa Mashirika ya Umma umebainisha ubadhirifu mkubwa wa pesa za umma kwenye kaguzi maalum na kaguzi za uchunguzi, naomba tuweke waziwazi ukaguzi maalum katika Mamlaka ya Bandari, wizi wa zaidi ya bilioni 22.64, wizi wa zaidi ya bilioni 24.29, wizi wa bilioni 2.9, wizi wa bilioni 8.38 cash yaani cheque zinaandikwa zitoe cash hazina kiambatanisho chochote, lakini katika hilo wizi wa bilioni 64 Mamlaka ya Bandari Tanga. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tarehe 3/8/2019 Mkandarasi wa kufanya kazi ya kutengeneza sehemu ya kugeuzia meli Bandari ya Tanga alipata mkataba wa bilioni 172, ndani yake zaidi ya bilioni 104 ni kwa kazi mbili tu ya kuongeza hilo lango la kugeuza meli. Tarehe 1/8/2019 hata kabla hajasaini mkataba alifaulisha hiyo kazi kwa kiasi cha bilioni 40. Huyu mtu alichukua cha juu bilioni 60. Lazima Bunge lako liweke azimio waziwazi na hawa ndio wa kuweka kwenye orodha hiyo.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Bandari imezoea ubadhirifu, ripoti ya kwanza aliyopokea Mheshimiwa Rais ya mwaka 2020 iliyoishia Juni, 2020, walikwapua bilioni 3.5, lakini ukaguzi maalum wameendelea kuonesha kwamba ni mamlaka inayokwapua pesa na bandari tunaitegemea kuchangia pato la Taifa.
Mheshimiwa Spika, kwenye ripoti ya PAC, naomba niongeze kuhusu kaguzi maalum wamezitaja pale kama moja ya azimio la Bunge, lakini naomba iwekwe wazi pia ukaguzi maalum juu ya tuhuma za ubadhirifu wa noti Benki Kuu, bilioni 3.9. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia tuongeze ukaguzi wa kuchunguza malipo ya dawa za Kimarekeni kutoka akaunti ya Benki ya Mradi wa Kuongeza Tija ya Uzalishaji Mpunga wa Benki Kuu ya Tanzania zaidi ya dola za Kimarekani 298,500. Naunga mkono taarifa hizi, lakini kwa kweli Serikali na jitihada za Mheshimiwa Rais kuzunguka nchi mbalimbali hata za ndani mapato yake yanavyoongezeka na rekodi mbalimbali, lakini hazitakuwa natija kama tunawaacha na Serikali iboreshe Sheria ya Manunuzi ya Umma, Serikali iboreshe Sheria ya Fedha za Umma ya mwaka 2001, iweke adhabu, yeyote anayeendelea na hoja za ukaguzi aadhibiwe kama kukatwa mshahara, kushushwa cheo…
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, taarifa.
T A A R I F A
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Spika, nataka tu nimpe mzungumzaji taarifa kwamba jana tumepata msamaha kwa nchi ya China shilingi bilioni 31. Kwa hiyo ukiangalia bilioni 60 tena zinapigwa pale Tanga kimchezo mchezo, ndio unaweza ukaona ni namna gani tupo kwenye dilemma ambayo huwezi kuielewa.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
SPIKA: Mheshimiwa Subira Mgalu, dakika moja malizia mchango wako, unapokea taarifa hiyo?
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, naipokea hiyo taarifa na ni kweli kwamba nchi yetu ukiangalia namna ambavyo ubadhirifu katika ripoti ya CAG tuna uwezo wa kuongeza mapato zaidi lakini hata hiyo misaada sasa ikaleta tija zaidi. Niwaombe sana watumishi wa umma, niwaombe kuwa wazalendo, haipendezi.
Mheshimiwa Spika, niwaombe pia Watanzania, ubadhirifu hauna awamu, hata sasa tunajadili miaka ya fedha iliyopita, lakini hauna awamu kwa sababu si mamlaka ndio inayotuma ubadhirifu na tunaona Wabunge tunaendelea kupongezwa kwamba mnafanya hivi na kwamba Rais awe mkali. Nataka niseme tu ni ubadhirifu wa miaka mbalimbali iliyopita, lakini tunaweka tahadhari na kwa kadri miaka ya fedha inayopita kwa kweli niwaombe sana Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali majibu yanayokwenda Ofisini kwake baada ya taarifa kufika Bungeni naomba ayahakiki vizuri, walikuwa wapi hawa wakaguliwa, wayalete sasa, kwa kweli siyo sawa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)