Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kojani
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Awali ya yote nami nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Rahim ambaye ametuwezesha kukutana katika Bunge hili na kujadili taarifa hizi tatu za Kamati zetu na bado anatupa thamani ya ubinadamu. Thamani ya ubinadamu ni uhai tu, ukiondoka uhai, basi tumekosa thamani ya ubinadamu na ndiyo maana tunaondolewa katika makazi ya watu na kupelekwa katika makazi maalum. Jambo la pili, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan, kwa namna anavyo pambana na kupigania kwa kujitoa kabisa kwa maslahi ya Taifa na wananchi wake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba pia nikushukuru wewe kwa kunipa fursa hii na mimi kutoa mchango wangu katika mjadala huu, Mungu akubariki sana. Naomba niwashukuru Wenyeviti wa Kamati hizi tatu lakini na Wenyeviti wa Kamati zote, niwashukuru na niwapongeze sana Wabunge wenzangu ambao mmechangia na kwa kweli mchango unalenga kujenga Taifa letu. Michango yenu ni mizuri sana na kila mmoja ambaye amesimama hapa nilikuwa namuona anaongea, anatoa hoja kwa hisia kali sana, kwa uchungu wa nchi yake, nawashukuru na ninawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba moja kwa moja nijielekeze katika hoja ambazo zimeletwa na Waheshimiwa Wabunge. Nikianza na hoja ya mwenendo wa utoaji fedha kwenda LGS siyo mzuri, ametoa mfano Mheshimiwa Mbunge, Halmashauri ya Mwanga.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2021/2022 bajeti yao ilikuwa ni bilioni 2.31 kwa ajili ya kujenga miradi ya maendeleo ya Halmashauri hiyo ya Mwanga. Serikali ilitoa shilingi bilioni 5.07 sawa na asilimia 219 kupeleka ndani ya Halmashauri hiyo. Mwaka 2022/2023 bajeti yao ilikuwa Bilioni 5.55 hadi kufikia Oktoba tayari Serikali imeshatoa Bilioni 1.85 sawa na asilimia 33.74. Ofisi ya Msajili wa Hazina ipo katika mchakato wa kuboresha sheria ili kuonesha baadhi ya vipengele vyenye upungufu hususan utaratibu wa kutoa adhabu kwa baadhi ya viongozi wa Taasisi za Umma ambao wanakiuka taratibu na sheria.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni ya GPSA. Kwanza naomba nikiri kwamba GPSA imechelewa au imechelewesha kutoa huduma hiyo ya magari. Kwa kweli, suala hili limechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo UVIKO–19 pia vita vya Ukraine, hii imechangia sana ucheleweshaji wa ununuzi wa magari hayo. Serikali imelipokea hili nikuhakikishie na nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba tutalichukulia hatua haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Spika, ipo hoja ambayo inasema Wizara ya Fedha na Mipango iboreshe mazingira ya Internal Auditors katika Serikali za Mitaa. Wizara ya Fedha na Mipango, tayari imepitia muundo wa Idara ya Internal Auditors na Mamlaka za Serikali za Mitaa…
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika taarifa!
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jerry William Silaa.
T A A R I F A
MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Spika, nimemsikiliza mchangiaji kwa makini na nimechelea kidogo. Nimemsikia akisema ziko hoja zimetolewa na Wabunge na anataka kutoa majibu, lakini hoja iliyoko mezani ni hoja ya Kamati za Bunge na Wabunge wote waliochangia wamechangia hoja ile na yeye kama mchangiaji ni vyema akachangia hoja ili tuweze kuihitimisha hoja. (Makofi)
SPIKA: Nafikiri kwa sababu hapo mwanzo alikuwa anaelezea utangulizi sasa anaenda kwenye hoja. Kwa hiyo, akishaanza hizo hoja ndiyo tutajua anazungumzia hoja za Kamati, kwa sababu pia Wabunge mmechangia humu ndani. Kwa hiyo, yeye yale yanayohusu Wizara yake ni muhimu ayatolee ufafanuzi. Kwa hiyo, mpaka tuanze kumsikia ndiyo tutajua kama ametoka nje ya hizi Kamati tatu na taarifa zake na je hilo jambo ambalo analolisema lilichangiwa humu ndani au hapana. Mheshimiwa Naibu Waziri karibu uendelee na mchango wako. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa ruhusa hii. Naomba nitoe ufafanuzi kwenye hoja iliyotolewa na Bunge kuhusu mtaji wa Benki ya Kilimo ya Tanzania. Kwanza naomba nikiri kwamba ni kweli Serikali iliahidi kutoa mtaji wa kupeleka katika Benki ya Kilimo ya Tanzania lakini mpaka sasa imetoa Bilioni 60 kutokana na uchache au uhafifu wa bajeti tuliyokuwa nayo. Serikali ipo katika juhudi mbalimbali kuhakikisha kwamba imeongeza mtaji katika benki hiyo kwa maendeleo ya benki hiyo lakini wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, juhudi ambazo Serikali imechukua, kwanza Serikali imechukua mkopo nafuu wa Dola za Kimarekani Milioni 92.55 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na kuikopesha TADB. Pili, Serikali imeamua kuifutia Benki ya Kilimo mkopo wa Dola za Marekeni 92.55, takribani Bilioni 216 na kugeuza kuwa mtaji wake ndani ya benki hiyo. Tatu, Serikali imechukua mkopo nafuu wa Euro Milioni 80 takribani Shilingi 185 kutoka Benki ya Maendeleo ya Ufaransa na kuikopesha benki hiyo. Hatua nyingine ambayo imechukuliwa na Serikali, ni Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliipatia Benki ya Maendeleo pesa takribani Dola za Kimarekani Milioni 25 kwa ajili ya dhamana kwa wakulima wadogo kutoka IFAD. Aidha, Serikali inaendelea kuangalia vyanzo vingine vya fedha ili kuipatia benki hiyo kwa maendeleo ya benki hiyo lakini na wananchi kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ilizungumzwa na baadhi ya Wabunge ni kuhusu makinikia. Kwa mujibu wa taarifa ya CAG ya mwaka 2021 ukurasa wa 63, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alibainisha kuwa baadhi ya mashauri ya kodi hususan yanayohusiana na sakata la makinikia yaliondolewa katika Mahakama za Rufaa za Kodi ili kushughulikiwa kwa utaratibu wa majadiliano kati ya Serikali na Kampuni za Madini. Katika majadiliano hayo Serikali ilijenga hoja na kufanikiwa kupata mafanikio haya yafuatayo: -
(i) Kulipwa Dola za Marekani Milioni 300, takribani Shilingi za Kitanzania Bilioni 700.
(ii) Kampuni ya Barrick kukubali kufuta kesi ya madai ya fidia kwa Serikali Dola za Marekani Bilioni 2.7.
(iii) Pia, kupewa umiliki wa asilimia 16 kwenye migodi ya kampuni hiyo ambapo imeunda kampuni mpya inayojulikana kwa jila la Twiga Mineral Cooperation. Barrick wao wana asilimia 84 na Serikali ina asilimia 16 katika hisa iyo.
(iv) Serikali imepokea jumla ya gawio la Dola za Marekani Milioni 36 na kupokea gawio kutokana na marekebisho ya mkopo kwa wanahisa. Dola za Marekani Milioni 16 kwa kipindi cha 2020/2021 na Barrick imekubali kutenga kiasi cha Dola za Marekani Sita kwa kila wakia kwa dhahabu zote ambayo itauzwa kwa ajili ya shughuli za kijamii.
Mheshimiwa Spika, kwa msingi huo, sakata la madai ya kodi ya Shilingi Trilioni 360 lilihitimishwa kwa Serikali kuridhia makubaliano haya kama ilivoainishwa katika maelezo ambayo ameyatowa Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mipango katika Bunge lililopita.
Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ilikuwa ni malimbikizo ya madeni hasa TANROADS. Serikali imechukua juhudi kubwa sana, kwa sababu madeni haya Serikali ya Awamu ya Sita imeyarithi, lakini imechukuwa juhudi kubwa sana katika kulipa madeni hayo yaliyokuwepo na tunaendelea. Nilihakikishie Bunge lako Tukufu kwamba tutaendelea kulipa na miradi yote ambayo imeandaliwa na Serikali ya kimkakati basi itatekelezwa na tutalipa certificates hizo zikishaletwa kwa wakati kabisa.
Mheshimiwa Spika, ilikuwepo hoja ambayo imezungumzwa kuhusu utaratibu wa kufuta madeni chechefu katika benki zetu za TIB na TCB. Serikali imeshaanza kuchukua hatua za kuondoa madeni chechefu katika benki za TIB na TCB ambapo taratibu zinaendelea kuhakikisha madeni hayo yanaondolewa kwenye vitabu vya benki.
Mheshimiwa Spika, ipo hoja ambayo imezungumzwa kuhusu kukosekana kwa bodi kunasababisha mashirika kukosa umakini wa kufanya kazi. Serikali imeendelea kuweka juhudi katika kuhakikisha Taasisi na Mashirika ya Umma yanakuwa na Bodi za Wakurugenzi hai. Kwa sasa Serikali imeshafanya uteuzi wa Bodi za Wakurugenzi zipatazo 23 kati ya Bodi 31 ambazo zimesalia Bodi Nane na hizo Serikali inachukuliwa hatua katika kipindi kifupi kabisa Serikali itakuwa imefanya uteuzi wa Bodi hizo.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri hebu rejea hapo kwenye takwimu za Bodi.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka juhudi katika kuhakikisha Taasisi na Mashirika ya Umma yanakuwa na na Bodi za Wakurugenzi hai, kwa sasa Serikali imeshafanya uteuzi wa Bodi za Wakurugenzi zipatazo 23 kati ya Bodi 31 ambazo zilikuwa hazina Bodi. Serikali inakamilisha utaratibu wa kuteua Bodi za Taasisi Nane zilizosalia…
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam.
T A A R I F A
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Bodi anazosema Serikali iko katika mpango wa kuteua Wajumbe wake kwa taarifa ya CAG, Bodi zingine zipo toka mwaka 2015, Serikali bado tu inaendeleaa na utaratibu wa Wakurugenzi wameshakuwa wamiliki wa hizo kampuni. Ahsante.(Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Hamadi Chande unapokea taarifa hiyo. (Kicheko)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nina ukakasi kidogo wa kupokea hiyo taarifa, lakini mimi niseme tu kwamba takwimu ambazo tunazo ni hizi 31 na 23 tumeshafanya uteuzi wa bodi, zilizosalia ni nane. Nadhani tuna asilimia zaidi ya 70, kwa hiyo awe na subira tu Mheshimiwa Mbunge ataona matokeo hivi karibuni, bodi zilizobakia tunateua. (Makofi)
SPIKA: Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa sababu kwenye taarifa ya Kamati walitaja Bodi zaidi na ni sehemu ya maazimio ya Kamati. Mwenyekiti wa Kamati ambayo inazungumzia hizi Bodi ili tutakapofika kwenye maazimio tusianze tena kurejea nyuma. Mwenyekiti wa Kamati zile takwimu ulizonazo na hizi Bodi anazozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri ni tofauti ni hizi au hili ni jambo jipya.
MHE. JERRY W. SILAA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Spika, kuna tofauti kubwa sana. Taarifa tulizonazo kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina mpaka kufikia tarehe 31 Oktoba, jumla ya mashirika 23 hayana Bodi za Wakurugenzi. Kuna mashirika 12 ambayo tayari Mheshimiwa Rais ameshateua Wenyeviti wa Bodi lakini bado Wajumbe hawajateuliwa. Kwa hiyo, jumla ni mashirika 35 mpaka kufikia tarehe 31 Oktoba wakati tunaandaa taarifa hii mashirika hayo hayana Bodi.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, hizi takwimu anazosema Mwenyekiti zipo sawasawa? Nataka tu kwenye takwimu ili wakati wa Azimio tusije tukaazimia na yale ambayo Serikali imeshayafanyia kazi.
Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma anasema Bodi 23 kufikia mwishoni mwa Oktoba zilikuwa hazina Wajumbe wala hazina Wenyeviti, Bodi 12 zina Wenyeviti ambao Rais ameshawateua lakini Wajumbe wale wanaoteuliwa na vyombo vingine ama na Mawaziri bado. Hizi takwimu zipo sawasawa?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa swali hilo. Suala hili la Bodi ambazo tuko na uhakika nazo ni Bodi 23 ambazo Wajumbe wake wameshateuliwa na zimeshakamilka. Hizi nyingine labda zipo kwa upande wa Taasisi nyingine ama Wizara nyingine lakini mimi nazungumzia ambazo ziko ndani ya Wizara ya Fedha.
SPIKA: Hivi Treasury Register anaripoti wapi? Mheshimiwa Mwenyekiti Treasury Register anaripoti wapi? (Makofi)
SPIKA: Mwenyekiti, Treasurer Registrar anaripoti wapi?
MHE. JERRY W. SILAA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Spika, Msajili wa Hazina anaripoti Wizara ya Fedha na Mipango. (Makofi)
SPIKA: sawa. Mheshimiwa Naibu Waziri, mimi nimekuelewa hoja yako. Ni kwamba hizi taasisi zinaweza kuwepo lakini kwa sasa hivi hapo hauna takwimu nazo, kwa hiyo sisi tutaendelea na azimio letu kuhusu hizi taasisi. Mheshimiwa Waziri wa Nchi anataka kutoa ufafanuzi.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa sana ya kikao chako hiki cha Bunge, kwa spirit ambayo ameingia nayo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, na hasa baada ya kukuta tatizo hili la teuzi za bodi kwamba ni tatizo ambalo limekuwa likijitokeza sana Serikalini; Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo na Chief Secretary na taasisi zinazohusika walishapewa kazi ya kusimamia.
Mheshimiwa Spika, itakuwa ni kumtendea haki Mheshimiwa Rais na kazi nzuri ambayo imekwishakufanywa kwani katika kipindi hiki…
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Taarifa.
SPIKA: Mheshimiwa Tabasam ngoja nijaribu kuelewa hoja kwanza kabla hujatoa taarifa yako, maana hajaanza bado kutoa hoja. Mheshimiwa Waziri wa Nchi.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nadhani itakuwa ni vizuri kama katika kipindi hiki ambacho tunaelekea kuhitimisha hoja hii tukapata fursa ya kupata taarifa ambazo ziko kamili. Ninaheshimu taarifa za Mwenyekiti ambazo zimeishia mwezi Oktoba, lakini tangu mwezi Oktoba, mpaka sasa tunaweza kuwa na taarifa ambazo ni current.
Mheshimiwa Spika, kwa heshima kubwa sana, kama utaridhia, tuweze kupata taarifa hizo ambazo tunaweza kuzipata sasa hivi kutoka kwa Treasurer Registrar ili azimio letu tukishalipitisha hapa liwe ni azimio ambalo limebeba dhana kamili ya idadi kamili ambayo inatakiwa kuwasilishwa. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Sasa, kulikuwa na taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam, sijajua taarifa nyingine inatoka wapi. Sasa ngoja, kwa sababu mtapata fursa ya kuchangia, Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI nawe ni kuhusu Bodi pengine zilizokuwa chini yako ambazo umezifanyia kazi kati ya huo muda. Sawa, Mheshimiwa Tabasam.
T A A R I F A
MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Spika, leo tupo serious na tumeamka vibaya, na ninaomba kabisa Waheshimiwa Mawaziri waje na nidhamu kabisa kwa siku ya leo, kwa sababu suala la vetting liko chini ya Ofisi ya Rais ambapo Waziri anayekuja kuzungumza maneno haya vetting iko kwake, na yeye ndiye sehemu ya ucheleweshaji wa vitu hivi. Tusubiri tufike mwisho leo. (Makofi)
SPIKA: Mwenyekiti nimekuona. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI, naona ulisimama.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nami nilitaka kutoa tu taarifa; kwamba katika bodi tatu, sijajua taarifa ya Mwenyekiti wa Hesabu za Mashirika ya Umma au Uwekezaji katika Mashirika ya Umma kama na za kwetu zimo. Endapo zimo, kwa Bodi ya DART tayari imeshaundwa, kwa Bodi ya Masoko ya Kariakoo tayari imeshaundwa, na Bodi ya Mikopo ya Serikali za Mitaa pia nayo tayari tumeshaiunda, kwa hiyo kwa upande wangu wa TAMISEMI bodi zote tatu zipo.
SPIKA: Haya, ahsante sana. Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, naona ulikuwa umesimama.
MHE. JERRY W. SILAA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UWEKEZAJI WA MITAJI YA UMMA: Mheshimiwa Spika, naomba nitoe maelezo madogo kutokana na taarifa zilizotolewa hapa, na kwa kuwa jina la Mheshimiwa Rais limetajwa, naomba ninukuu Hotuba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, aliyoitoa tarehe 30, Machi 2022, nanukuu; “CAG umeeleza kuwa, mwenendo wa Mashirika ya Umma ambayo umebainisha Mashirika 38 ya Umma yanaendeshwa bila kuwa na Bodi. Hii inashangaza kwa miaka kadhaa mashirika yanaendeshwa hakuna Bodi za Wakurugenzi. Mimi nakumbuka nilipoingia nilipata mtiririko wa maombi ya bodi na yote nimeshayatoa. Sasa kama Waziri ana mashirika, bado anaendesha mashirika yasiyo na bodi, siwezi kumuelewa na sijui tatizo ni nini.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimesema niyaseme haya kwa sababu kuna mashirika ama kuna Wizara wakati mwingine zinatupa mzigo wa uteuzi kwa Mheshimiwa Rais, lakini Mheshimiwa Rais alishasema hadharani kwamba yeye anateua bodi kwa wakati, la kwanza.
Mheshimiwa Spika, lakini la pili, Ofisi ya Msajili wa Hazina inao mfumo ambao unatoa taarifa kwa Wizara miezi tisa kabla bodi haijamaliza muda wake ili mchakato na urasimu wote wa vetting ukamilike kwa wakati. Kwa hiyo tunaporipoti hapa, tunaripoti mambo ambayo tunauhakika nayo na yamethibitshwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na yako sahihi, na kwa nyongeza, tarehe 30, Oktoba ni siku nne kuanzia sasa ndiyo taarifa yetu imetoka.
SPIKA: Haya, ahsante sana. Mheshimiwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, malizia mchango wako.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia tena fursa hii. Nimalizie mchango wangu kwa hoja iliyokuwa inazungumzia Sheria ya Manunuzi kwamba ina upungufu.
Mheshimiwa Spika, hili nikiri kwamba sheria hii ina upungufu; na kama alivyoeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali hatua ambayo imefikiwa kwa sasa ya kufanya marekebisho ya sheria hiyo iko katika ngazi ya maamuzi na karibuni hivi itaingia Bungeni kwa ajili ya kupata mapendekezo na maoni kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge. kwa hiyo niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba suala la Sheria ya Manunuzi na sura 410 lipo katika hatua ya maamuzi kwa sasa.
Mheshimiwa Spika, wapo wachangiaji wengi ambao walichangia kuhusu manunuzi. Kwamba kuna upotevu mkubwa sana wa fedha katika manunuzi. Naweza kusema kwamba zaidi ya asilimia 70 ya fedha za bajeti za Serikali zipo katika manunuzi. Kwa hiyo hii ni sehemu moja nyeti na muhimu sana na Serikali imeichukulia hatua sehemu hii kwa kiasi kikubwa sana. Kutokana na mapungufu yaliyokuwepo pale, Serikali imeamua kuanzisha mfumo mpya wa manunuzi ambao unaitwa NEST ili kuepuka changamoto ambazo zinajitokeza wakati wa kufanya manunuzi.
Mheshimiwa Spika, na hii yote ni kwa sababu ya mfumo tulio nao si rafiki kwa matumizi ya watumiaji na pia utoaji wa taarifa sahihi. Kwa hiyo tumeamua Serikali kuanzisha mfumo huu, na faida ambazo zinaweza kupatikana kutokana na mfumo wa sasa wa NEST ni nyingi sana. Kwa mfano, itaongeza uwazi (transparency) kwa sababu mfumo uliokuwepo usiri ulikuwa ni mkubwa sana ambao unaweza kupelekea mianya ya rushwa. Mfumo huu utakuwa uko wazi na watumiaji wote watakuwa wana-access.
Mheshimiwa Spika, jambo lingine, utaongeza uwajibikaji; kutakuwa na uwajibikaji mkubwa sana katika mfumo huu. Faida nyingine ambayo inaweza kupatikana katika mfumo huu ni kuweka ukomo wa bei za bidhaa, yaani kuweka bei kikomo au bei elekezi, kwamba bidhaa hii bei yake ni hii hapa ili kusudi kuepuka manunuzi holela. Maana inawezekana bidhaa moja hii mfano ya kalamu kwa idara tofauti zikawa na bei tofauti kutokana na mfumo ambao ulikuwepo, lakini kwa sasa mfumo huu unaenda kujenga na kutuweka wazi. Na huu ndiyo mwarobaini pekee wa ku-save fedha za Watanzania.
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, taarifa.
SPIKA: Kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Deus Sangu, Mheshimiwa Naibu Waziri.
T A A R I F A
MHE. DEUS C. SANGU: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana; naomba kumpa taarifa mzungumzaji. Mfumo huu wa TANEPS ambao upo sasa ni mfumo ambao umewekwa hivi karibuni, mwaka 2020 ndio ulikuwa mandatory kwa taasisi zote za umma na umegharimu mabilioni ya fedha za Watanzania. Leo hii ndani ya miaka miwili Serikali yenyewe iliyoweka huo mfumo inatuambia kwamba ni redundant na hauna maana, na wanatuambia wanakuja na mfumo wa NEST ambao uta- address matatizo haya. Hivi kweli huu sio ufisadi mwingine? (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Sangu kwa kawaida taarifa huwa haina maswali lakini, Mheshimiwa Naibu Waziri wa fedha na mipango unaipokea taarifa hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, hii taarifa siipokei kwa sababu unaweza kuishi na mke hata kwa siku tatu tu; bila kujali gharama ya mahari uliyotoa; ukaona kwa mwenendo huu sasa huyu hanifai tena. Kwa hiyo unaweza kuacha. Hata kama umetumia siku tatu, achilia miaka miwili. Kwa hiyo taarifa hii mimi siipokei.
Mheshimiwa Spika, mfumo huu tunaotarajia kuutumia endapo utatumika, kwa utafiti mdogo ambao tumeufanya, utakoa zaidi ya shilingi trilioni mbili. Pia mfumo huu utawezesha Ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali angalau kuwa na matokeo mazuri badala ya kuwa na matokeo hasi siku zote, kwa sababu tunakwenda kujadili na kuona wapi kuna mwanya au kuna viashiria vya upotevu wa fedha kabla mradi haujaanza, tofauti na mfumo ambao ulikuwepo.
Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kutoa wito kwa taasisi zote za Serikali kujiunga na mfumo huu ambao utasaidia matumizi halali. Ahsate sana. (Makofi)