Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa uzima na uhai hatimaye ametupa kibali tuko katika eneo hili la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwamba kabisa naomba nimshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama yetu mpendwa Mheshimiwa Samia Suluhu kwa kazi kubwa ambayo anaifanya kwa Watanzania. Naomba nimpongeze sana. Vile vile naomba nimpongeze Waziri Mkuu kwa kazi kubwa ya kuendelea kuisimamia Serikali. Anafanya kazi nzuri, tunaona anahangaika katika Mikoa mbalimbali kuhakikisha nchi yetu inasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze Serikali kwa ujumla kwa kazi kubwa kupitia mama yetu Mheshimiwa Samia; tulipewa fedha nyingi kupitia fedha za UVIKO ambazo zimekuja katika Majimbo yetu, zimetuwezesha kujenga Zahanati, Vituo vya Afya, Shule Shikizi na Shule za Sekondari. Naomba niipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. Kusema kweli sisi Wabunge wa Majimbo tunajivunia sana kwa sababu kazi imeonekana na bajeti imeonekana. Naomba tuipe pongezi kubwa sana Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa ambayo wameifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kazi kubwa imefanyika, tumeona kwenye majengo ya Shule Shikizi na Shule za Sekondari tumeweka vifaa kama madawati na kadhalika, pia tumejenga Vituo vya Afya na Zahanati, lakini mpaka leo bado hatujapata vifaa. Tumeanza kujenga majengo mengine mwezi wa Tatu mwaka 2021, mengine tumepewa fedha mwezi wa Kumi mwaka 2021, tayari yamekamilika lakini mpaka leo vifaa tiba hatujapata. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo langu nimepewa fedha za Hospitali ya Wilaya, nimejenga Hospitali ya Wilaya lakini mpaka leo hatujaweza kuifungua kwa sababu hatuna vifaatiba. Tunaiomba Serikali sasa ijielekeze kwenye vifaatiba ili majengo yale yaweze kufanya kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa tuna kero kubwa sana ya watendaji wa kazi ambao ni walimu, manesi na madaktari. Leo naomba nimshukuru sana Waziri mwenye dhamana ambaye ni Waziri wa Utumishi, ametuambia kutakuwa na ajira kama 30,000 ambapo atakuja kwenye bajeti yake kuisema. Naomba tuipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanaendelea kutuonyesha sisi Watanzania. Tulikuwa tunapata kero kubwa kwa ajili ya watumishi, lakini leo tunatarajia sasa watumishi watapatikana katika maeneo yetu kwa sababu tumejenga Shule na Zahanati lakini hakuna watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado kidogo kuna changamoto kwa ajili ya walimu wenye madai yao, bado hatujaweza kuwafikia wote, wengine hawajapata madai yao, wanadai malimbikizo ya madeni yao. Tunaomba hilo tulifanyie kazi kwa sababu wanafanya kazi kubwa, wanakaa katika mazingira magumu. Naiomba sana Serikali yangu sikivu iwaangalie hawa walimu wanaodai madai yao limbikizi waweze kulipwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niipongeze sana mifuko ya kijamii pamoja na mashirika. Hii mifuko inajitegemea na vilevile kuna vikwazo kupitia mashirika yetu haya, yana uwezo wa kuajiri, sasa tumewawekea vikwazo wasiajiri mpaka kibali kitoke Utumishi. Nilikuwa naomba haya mashirika kwenye ngazi labda kuanzia vibarua, makarani na wengineo hapa tumewapa fursa waajiri wenyewe, lakini kupitia ngazi ya Mameneja na Wakurugenzi iende Utumishi ili waweze kuajiri. Kwa sababu kuna vikwazo, unakuta wanatamani kuajiri watu, lakini kuna vikwazo lazima wapate vibali ili kazi ziweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naiomba Serikali yangu kupitia utumishi tuwape ruhusa waajiri kuanzia ngazi ya vibarua mpaka makarani, zile kazi ambazo ni za kawaida, waajiri wenyewe ili kazi zile nyepesi na rahisi zaidi waweze kuzifanya ili majukumu yao yaweze kwenda vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakuja TARURA. Naomba niipongeze Serikali yangu; na kupitia Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia, najua bajeti iliyopita kila Mbunge wa Jimbo alipata shilingi bilioni 1,500. Zile fedha zimetusaidia sana, zimefungua barabara, kazi kubwa imefanyika, inaonekana; barabara za vijiji na vitongoji sasa hivi zimeunganika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, ndani ya maeneo yetu ya vijijini kuna madaraja makubwa. Tumeona Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa wakati akiwasilisha bajeti yake, ameonesha madaraja makubwa yaliyojengwa na mama yetu Mheshimiwa Samia kwa fedha nyingi. Naomba Serikali sasa iongeze bajeti kwenye TARURA ili sasa madaraja yote ya vijijini, kuunganisha vijiji na vitongoji yaweze kujengwa kwa ajili ya usalama wa wananchi wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kipingi hiki cha mvua, leo hii mvua zikinyesha katika maeneo yetu, vitongoji na vijiji watoto wa shule katika mito yetu wanashindwa kuvuka kabisa. Ina maana mvua zikianza kunyesha watoto wengi hawaendi kwenye masomo inavyotakiwa katika muhula.
Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba sana, sasa ifike kipindi TARURA tuiongezee bajeti. Madaraja yote makubwa ndani ya vijiji na vitongoji vyetu, yajengwe na TARURA yenyewe. TANROADS inashughulika na barabara kubwa na madaraja makubwa, sasa naomba TARURA tuiongezee fedha ili iweze kufanya kazi vizuri zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna vitu vingi tunavyovifanya katika nchi yetu, tunajenga vituo vya polisi katika maeneo yetu na tunaendelea kuchangia na wananchi wanaendelea kuchangia, kuna maboma, lakini naomba ndani ya kata zetu unakuta polisi anakaa kwenye Ofisi ya Mtendaji anakuwa yeye polisi peke yake. Sasa kama kuna uhalifu ndani ya maeneo yetu au kuna kitu chochote kimefanyika katika maeneo yetu ya kata, ina maana wale wahalifu wanachukuliwa wanapelekwa katika Ofisi ya Mtendaji maana yake hana sehemu ya kuwatunza. Nilikuwa naomba kupitia Serikali yetu sikivu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ufike muafaka katika kila kata tujenge vituo vidogo vidogo vya polisi ili wajitegeme. Ukiangalia sasa hivi katika maeneo yetu kuna uhalifu mwingi. Watu wako mbali unakuta kilometa 20, kilometa 30, kilometa 60, kilometa 70 hawana kituo cha polisi. Naomba sana tujielekeze sasa kuhakikisha tunajenga vituo vidogo vidogo kwenye kata zetu kwa ajili ya ulinzi na usalama wa Watanzania tunaoendelea kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, najua kuna mengi ambayo yamefanyika katika nchi yetu na ni mazuri, sasa hivi hatuna hata la kusema, kazi kubwa imefanyika. Tumeomba pesa tumeletewa, kero nyingi kusema kweli zimepungua hata leo Wabunge sidhani kama tutaongea sana kwa sababu tunaona pesa tunaletewa miradi inafanyika, kero kubwa tu tuliyokuwa nayo sisi Wabunge, watendaji kazi hatuna, tunaomba sasa ajira ya watendaji kwa sababu tayari tumeshaambiwa watendaji wataajiriwa au kuna ajira zinakuja. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niseme ahsanteni sana. Naomba niunge mkono bajeti hii ya Waziri Mkuu kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)