Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kutoa mchango wangu kwa bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2022/ 2023.
Kwanza kabisa nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uhai na hatimaye leo tumekutana katika ukumbi huu tukizungumza maslahi mapana ya Taifa letu. Kwenye mchango wangu leo naomba kwanza nitajielekeza kwenye migogoro ya ardhi ndani ya Taifa letu. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye hotuba yake. Ukurasa wa 45(75) Ardhi, ametuambia naomba kunukuu: “Ardhi ni rasilimali muhimu katika kukuza uchumi na kuondoa umasikini.” Naomba niishie hapo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kutambua kwamba ardhi ni rasilimali muhimu, lakini rasilimali hiyo muhimu inaweza ikatuondoa kwenye wimbi kubwa la umaskini wa Watanzania tulionao. Hata hivyo, napata shida kidogo kama Serikali inatambua kwamba ardhi ni rasilimali muhimu na ndio kichocheo cha uchumi katika Taifa letu, ni kwa nini Serikali imekuwa na kigugumizi cha kutatua migogoro ya ardhi ndani ya Taifa letu? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu imekuwa na migogoro mingi sana ya aina tofauti tofauti. Tumekuwa na migogoro ya mipaka, ya vijiji kwa vijiji, wilaya kwa wilaya, mikoa kwa mikoa, migogoro baina ya hifadhi na wafugaji, wakulima na wafugaji, wakulima na wahifadhi. Migogoro hii tumekuwa tukiisema kila siku. Tangu nimeingia Bunge la 11 nimekuwa nikisema suala zima la migogoro hii. Lakini nakumbuka bajeti ya mwaka 2017/2018 tuliambiwa Wabunge wote, tuainishe migogoro yetu tuliyonayo ndani ya majimbo yetu na ndani ya maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliorodhesha migogoro tukaletewa kitabu kimoja kikubwa sana kila Mbunge akapewa zaidi ya kurasa 1,000, tukijua kwamba Serikali imekwenda kutambua migogoro hiyo na inakwenda kuifanyia kazi. Sio hilo tu, baada ya hilo ikaundwa Tume ya Mawaziri Nane, Bunge lililopita wakatumia helikopta, kodi za Watanzania wakazunguka nchi hii nzima kwenye maeneo mbalimbali kupitia ile ripoti tuliyowapa. Mpaka leo ile ripoti iko chini ya uvungu, haijawahi kutoka hadharani, hivi shida ni nini kwa Serikali Sikivu, inayowapenda Watanzania wake, kwenda kuwaondolea wananchi hawa migogoro ili twende tukakuze uchumi wa Taifa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sio hicho tu mwaka jana pia Tume hiyo hiyo ya Mawaziri Nane, wamezunguka tena nchi nzima kwenda kukagua migogoro. Walikotoka leo moto umewaka kuliko ilivyokuwa. Watu wanauawa kisa ni mpaka wewe upo Wilaya A na mimi nipo Wilaya B yaani utafikiri sijui tupo Taifa gani hata Ukraine haipo hivyo. Haijafikia namna hiyo katika suala zima la migogoro katika Taifa letu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi ina zaidi ya miaka 10, lakini Tume hii hivi inafanya kazi gani? Ukija kwenye bajeti wanapewa mishahara, lakini tunaambiwa Tume hii kazi yake, ni kuratibu na kutoa mafunzo kwa Halmashauri zetu ili Halmashauri ziweze kutekeleza. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukawa unatengea watu fedha kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kwenda kutatua migogoro, badala ya kwenda kutoa fedha ya kwenda kupima ardhi ya kupanga, kupima na kumilikisha. Leo tunavyozungumza kuna ardhi ya wawekezaji wanatajwa sana. Mkulima leo ardhi yake haijulikani, mfugaji leo ardhi yake haijulikani iko wapi lakini maliasili (wanyama) ardhi yao inajulikana mahali ilipo. Leo mfugaji wa nchi hii mwenye ng’ombe 100, ng’ombe 200 hana tofauti na mtu anayemiliki bangi au madawa ya kulevya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, leo mfugaji wa Taifa letu ambapo pia kwenye hotuba ya Waziri Mkuu amekiri kwamba, tumeongeza pato kwa kusafirisha nyama nje ya nchi, maziwa pamoja na ngozi, lakini ukija kuangalia hali ya mfugaji wa Tanzania malisho anajitafutia mwenyewe, majosho anatafuta mwenyewe, madawa anatafuta mwenyewe, kila kitu anajitafutia mwenyewe. Leo ng’ombe wakitoka wamechunga kwenye Hifadhi, huyo mfugaji hataweza kumiliki chochote kwenye ile mifugo. Tulizungumza Bunge lililopita hata mwaka jana nilisema namna mfugaji wanavyomfanya katika Taifa hili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mfugaji huyo huyo tukija hata kwenye shughuli zetu mbalimbali hata za Mwenge tu hizi Mheshimiwa Nusrat amesema, mfugaji huyu tunamfuata aweze kutuchangia kitoweo, lakini pili atoe na mchango wa mafuta ili Mwenge uweze kuzunguka ndani ya nchi yetu; na wakati Ole Sendeka anasema suala la Mwenge kwamba ulikuwepo na Mwalimu alisema kwamba utawashwa na nimsaidie tu hiyo nyingine ya kuzunguka ni ya kwake. Mwalimu alisema tutauwasha Mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro na sio kuukimbiza kuzunguka nao barabarani. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mifugo ambayo wanachanga vitoweo kwa ajili ya kuzungusha Mwenge barabarani brother pole sana. Ahakikishe apambane apate hati miliki ya kuweza kumiliki ardhi yako ya kuchunga mifugo na ili aweze kupata tija ya mazao yake na mifugo na kujenga uchumi wa familia yake na kipato chake na sio kutetea suala zima la kuzungusha Mwenge, anasema eti ni Mwalimu alisema. (Makofi/Kicheko)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa.
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumpa Taarifa mzungumzaji Mheshimiwa Kunti kwamba, Mwenge wa Uhuru katika azma yake ya kuanzishwa ilikuwa mwaka 1958 na katika azma ile ile ya yale yaliyoelezwa ni katika kuhakikisha kwamba kunakuwa na umoja, amani, upendo na mshikamano. Baada ya Uhuru mwaka 1961 tulivyopata Uhuru Mwenge ule uliwekwa Mlima Kilimanjaro na baada ya hapo purpose yake tulipoingia katika Mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa ulirithiwa na kuasisiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa maana ya kwamba ukawa na jukumu sasa la kusimamia masilahi ya nchi. Mojawapo la kwanza, ni kuhakikisha unamulika masuala yote ya rushwa katika miradi ya maendeleo, unakwenda kufanya usimamizi kwa kufanya monitoring na evaluation katika miradi mikubwa ya maendeleo ya nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha zote zinazotolewa katika bajeti ya Serikali hii pamoja na kuwa na Mfumo wa Kiserikali wa kiutawala kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inahitaji kuwa na overseeing body au institution nyingine ambayo inakwenda ikiwa independent kama Mwenge wa Uhuru ambao wajibu wake unapokwenda katika maeneo hayo ni kuhakikisha kwamba, kama kwa mwaka wa jana tu Mwenge wa Uhuru uligundua miradi zaidi ya 46 yenye thamani ya fedha zaidi ya shilingi bilioni 40 na haya mambo yapo kwenye uchunguzi PCCB watachukua hatua. Kwa hiyo, kilichopo kwenye hii dhana… (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante amekuelewa. Haya Mheshimiwa Kunti, malizia dakika yako moja.
MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri alikuwa na muda wa kuja kujibu hoja za Wabunge na huu haukuwa wakati wake. Pili, kwenye suala la ufisadi hiyo hiyo miradi tunayokwenda kuzindua na Mwenge bado tunakutana na ufisadi 150 kidogo. Kwa hiyo, naomba tu Mheshimiwa Waziri atulia muda wake utafika atajibu hoja za Wabunge wala asitake kupata kuwa na haraka. Naomba niendelee na mchango wangu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala la migogoro ya ardhi tuliyonayo leo viongozi wa Chama cha Mapinduzi ambao wamepewa dhamana na Taifa hili; na watu wanaendelea kuumia na kupoteza maisha na mali zao kwa sababu ya kushindwa kufanya maamuzi ya kutatua migogoro kwa kwenda kusema kwamba wewe eneo lako ni hili na wewe eneo lako ni hili. Hawataki kuweka bayana hizo, hakika Mwenyezi Mungu atakuja kuwahesabu siku ya hukumu. Naomba niwashauri kwenye migogoro ya ardhi, cha kwanza Sheria ya Tume ya Mipango ya Ardhi imepitwa na wakati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaiomba Sheria hiyo ije hapa tuifanyie marekebisho ili Tume hii tuipe mamlaka ya kuweza kusimamia mpaka chini kwenye halmashauri zetu na kuweza kwenda kutatua hiyo migogoro. La pili, mamlaka zetu za halmashauri ambazo na zenyewe zinahusika kwenye suala zima la upimaji na upangaji na umilikishaji, twende sasa TAMISEMI tunawaomba sasa, waende wakatenge Mafungu kwa ajili ya suala zima la upimaji na umilikishaji wa ardhi kwa wananchi wetu na kwenda kuondoa migogoro. Suala la tatu…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)