Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango wangu katika hotuba iliyoko mbele ya Bunge letu Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze napongezi kwa ofisi ya Waziri Mkuu kwa kazi nzuri sana ambayo wameifanya. Tumeona utekelezaji wa miradi mbalimbali ambayo hivi punde tumetoka kuikagua katika maeneo tofauti tofauti katika nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, kipekee kupitia hotuba yangu ningependa pia nitoe mchango katika eneo la ukusanyaji wa mapato, nikitoa pongezi kubwa sana kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa namna ambavyo wameendelea na zoezi zuri kabisa la kukusanya mapato bila kutumia mitutu ya bunduki wala bila kufunga biashara za watu. Hii inaonyesha wazi dhamira ya Mheshimiwa Rais, kwamba yeye ana mentality ya kibiashara na ana amini kwamba kupitia biashara ndivyo tunaweza kupata kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ningependa kuchangia eneo la mfumuko wa bei lakini nikigusia eneo zima la mafuta. Kama ambavyo mzungumzaji wa mwisho ametoka kusema, ni kweli mafuta yanapopanda bei, maana yake kila kitu kitakwenda kupanda bei; kwa sababu gharama za usafiri, usafirishaji mitambo na kadhalika kwenye maeneo yote ya udhalishaji inategemea nishati ya mafuta.

Mheshimiwa Spika, sasa ni nini muarobaini wa hili jambo? Kwa sasa kwa hali tuliyokuwa nayo ambayo imetokana na vita, baina ya Ukraine na Russia, namna pekee ambayo inaweza kutusaidia ni Serikali kuweka ruzuku katika eneo zima hili la uagizaji wa mafuta ili angalau sasa kuweza ku-stabilize bei.

Mheshimiwa Spika, kuhusu mfumo wa uagizaji mafuta kwa pamoja, eneo hili ningeomba sana kwa ridhaa yako uwasiliana ikiwezekana na Wizara ya Nishati, angalau tupate semina ya uelewa wa pamoja. Hatuwezi tukakwepa mfumo wa bulk procurement system ambao ndio unaotufanya leo tunatamba kuwa na storage ya mafuta ya siku 36. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tungeruhusu kila mmoja aagize mafuta kwa wakati wake, tusingeweza kuwa na control hii ambayo leo tunayo na mfumo huu umeanzishwa mwaka 2011 kupitia Bunge lako Tukufu likiwa ni sehemu la mwanzo wa mfumo huu.

Mheshimiwa Spika, mfumo huu umetusaidia sana kudhibiti baadhi ya mambo. Maana yake nini; kwenye mfumo huu wa uagizaji wa pamoja wafanyabiashara wa mafuta wanakutana na viwanda ambavyo vinasambaza mafuta kwa maana ya refineries; tunaangalia bei shindani, na kwenye mamfuta vitu vitatu ni muhimu sana kuzingatia; kwanza reliability, availability, na affordability; hivi ndivyo vitu vitatu vya msingi vya kuangalia wakati wa kuagiza mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapokwenda kupata sasa tonnage watu wote tunapeleka oda zetu kwa yule ambaye ameshinda tenda na anasafirisha mzigo wote kwa wakati mmoja. Anaposafirisha mzigo kwa wakati mmoja maana yake hata shipping cost zinakuwa zimeshuka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, zamani wakati kila mmoja alipokuwa anaagiza kutoka kwenye kila kichochoro chake maana yake hata demurrage pale bandarini ilikuwa inaongezeka kwa sababu unasubiri mafuta yako katika meli kumi tofauti tofauti. Lakini leo tunaagiza mzigo katika meli moja kubwa inaleta, hata kama ni metric ton 600,000 zinatua kwa pamoja; demurrage imeshuka kutoka dola 30 hadi 45 kwa siku, sasa hivi dola moja mpaka tatu kwa siku. Kwa hiyo, haya ni mapinduzi makubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, umuhimu wa mfumo huu ili tuelewe, ndiyo maana nasema lazima tupate semina ya kuelewa hili jambo vizuri. Leo nchi zote zinazotuzunguka hapa zimejiunga katika mfumo wa bulk procurement system. Uganda wamo, Burundi wamo, Rwanda wamo, Malawi wamo, Zambia wamo na DR Congo wimeingia. Hata nchi Mauritius imekuja kujifunza namna bora ya kuingia katika mfumo huu wa manunuzi ya pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema, makampuni yanayozalisha mafuta duniani yanafahamika. Kwa hapa kwetu tuna Trafigura au DAX Energy; ya kizawa, tuna GBP ambapo mmiliki ni mwenyeji kutoka Kigoma, anashusha katika Bandari ya Tanga. Kuna Hans Energy, mwenyeji wa Mara, wakati mwingine anashusha katika Bandari ya Dar es Salaam, wanapata hizi tenda. Kwa hiyo, hakuna shida ya kuwa na wasiwasi kwamba eti kuna meli sijui zimepaki Bandarini huko kwenye bahari zina mafuta. Huko ndiko tulikotoka wakati ule tulipokuwa tunaletewa mafuta machafu, ambayo yalikuwa hata ukiweka kwenye magari, kila siku magari yanakufa pampu barabarani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumetoka huko, hakuna businessman mzuri, smart akaweka meli kwenye bahari. Biashara yote inafanyika kwenye mtandao na hii ni kama zilivyo kwenye Bureau De Change, bei ya mafuta kila siku ukiingia kwenye mtandao unaiona. Nasi source yetu ni Arab Gulf ndiko tunakochukulia mafuta zaidi. Ukiangalia kwenye mtandao pale unaona bei ya mafuta kila siku kama ilivyo kwenye stock exchange, hakuna namna kwamba eti utakuta meli imekaa kwenye deep sea huko ambayo siyo ya wizi au siyo ya maharamia iletwe kwenye nchi ambayo ni ya kistaarabu kama Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninachoshauri, Serikali iwe na mpango mkakati madhubuti wa kuongeza storage facility katika TIPER. Sasa hivi TIPER tunapokea mafuta lakini bado kwa hali hii ambayo tunayo, ni lazima tuongeze storage capacity ili tuweze kuwa na ujazo wa kuwa na mafuta hata wa miezi mitatu mpaka minne. Ila katika mfumo mzima wa kodi, mfumo huu ndiyo unaotusaidia zaidi. Kwa sababu gani? Pale ambapo makampuni haya ya mafuta yanapotoa order zao, tayari TRA anajua kabisa kwamba kampuni ‘X’ itaingiza metric ton kiasi fulani na kodi yetu tutakusanya kiasi fulani. Hata kama yatapita kwenye mita, lakini tayari mchakato wa awali wa kujua kwamba Serikali inapata kodi kiasi gani unajulikana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge, niwaambie, mafuta ndiyo bidhaa pekee ambayo inalipiwa kodi zote kabla hata hayajaanza kutumika. Inapoanza kuwa discharged kutoka kwenye meli kwenda kwenye matenki yale ya kuhifadhia, tayari pale kodi zote za Serikali zinakuwa zimelipwa. Kwa hiyo, huo mfumo umetusaidia sana kama Taifa na ningeomba sana wala tusiuguse. Kama kuna maboresho yanaweza kufanyika, lakini kwa tunavyokwenda mpaka sasa uko vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo ningetaka kuchangia ni MSD. Bohari ya Madawa haifanyi kazi vile inavyopaswa. Tuna shida kubwa sana katika Bohari ya Madawa kwa maana kwamba Halmashauri nyingi tumeweka fedha pale ili tuletewe vifaatiba na vitendanishi, lakini hivi tunavyozungumza ni zaidi ya miezi sita hakuna vifaa ambavyo vinapatikana katika hospitali zetu. Sasa jukumu la Bunge ni kusimamia na kuishauri Serikali.

Mheshimiwa Spika, tunaomba Bunge lako Tukufu lielekeze Serikali kama MSD kazi imewashinda, basi atafutwe mtu ambaye anaweza kwenda kusimamia ile kazi vizuri. Huko nyuma tumeona walikuwa na mpango mzuri sana. Walikuwa na mpango mzuri kiasi kwamba waliwahi kupata tender ya kusambaza dawa katika nchi zote za SADC, lakini nadhani kwa haya yaliyotokea hapa nyuma na kushindwa kufanya kazi zao kwa ufanisi, hata ile kazi ambayo ingeweza kuingizia Taifa kipato sasa imekwenda kwenye eneo likinge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya maneno hayo, nakushukuru sana. Ahsante sana kwa nafasi hii. (Makofi)