Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ubungo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. PROF. KITILA A. MKUMBO: Mheshimiwa Spika, nami nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri sana aliyoitoa jana hasa kwa matumizi yake ya picha na video ambayo yalionesha wazi kwamba kazi kubwa inaendelea katika sehemu mbalimbali hapa nchini. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, bahari mbaya Mheshimiwa Waziri Mkuu jana alisahau au aliamua kuacha kwa makusudi tu, moja ya mafanikio muhimu sana alipokuwa anazungumzia eneo la utamaduni, sanaa na michezo. Ukweli wenyewe ni kwamba, kwa hakika mwaka huu tena Yanga itachukua ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC. Kwa hiyo, alitaja pale mengi lakini hili akaliacha, sasa nimeona nilitaje. (Makofi/ Kicheko)
Mheshimiwa Spika, mwaka huu na mwezi huu wa Aprili, nchi yetu inaadhimisha miaka 100 ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kama angekuwa hai, mwezi huu angefikisha miaka 100. Ni fursa nzuri kwa nchi yetu kuendelea kutafakari mchango wa Mwalimu, lakini pia ni fursa nzuri kuendelea kutafakari historia ya nchi yetu; miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika na miaka 58 ya Muungano wetu wa Tanganyika na Zanzibar. Siku ya Jumatatu tarehe 29 Julai, mwaka 1985, Mwalimu alitoa hotuba yake ya mwisho katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa Rais. Katika hotuba ile alitumia nafasi ile kuipitisha nchi katika mafanikio yaliyopatikana katika uongozi wake na katika changamoto ambazo zilijitokeza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, moja ya jambo zuri sana katika hotuba ile, ni ukweli kwamba Mwalimu alikuwa muwazi na mkweli kwa makosa ambayo aliyafanya katika uongozi wake. Alitaja mengi, lakini muhimu yanajitokeza wazi. Moja, alikiri na alitumia neno la Kiingereza, alisema: “it was a major error kufuta Mamlaka za Serikali za Mitaa.” Kosa la pili ambalo aliliita: “the other most serious mistake,” ilikuwa ni kufuta Vyama vya Ushirika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kosa la kwanza tulilisahisha yeye mwenyewe akiwemo mwaka 1982 kwa Bunge hili kutunga Sheria ya Kurejesha Mamlaka ya Serikali za Mitaa na tukaingiza kwenye Katiba ibara 145 na 146. Pia tumefanya marekebisho makubwa tangu wakati huo hasa mwaka 1996 - 1998 pale ambapo tuliamua kuanza kutekeleza Policy ya D By D (Decentralization by Devolution) maarufu kama Sera ya Ugatuaji wa Madaraka Mikoani.
Mheshimiwa Spika, sera hii ina mambo makubwa mawili. Kwanza ni kuhamisha majukumu ya kusimamia matumizi ya fedha za maendeleo na watumishi kutoka Serikali Kuu kwenda Serikali za Mitaa. La pili, tuliona kabisa kwamba huduma za jamii ili ziweze kuwa endelevu; zingekuwa tu endelevu kama wananchi wangeshiriki kikamilifu katika kubuni kwa maana ya kuibua miradi, kushiriki kwenye utekelezaji wake na kuisimamia pale ambapo imeshakamilika.
Mheshimiwa Spika, kwa maoni yangu, tuna mambo matatu ya kusahihisha katika eneo hili la Local Government. Kwanza ni kuhusu mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali ya Mitaa. Ukisoma ile document, mahusiano yanayotarajiwa kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa ni mahusiano ya kiushauri na kiuwezeshaji; kwamba Serikali Kuu itaishauri na kuiwezesha Local Government.
Mheshimiwa Spika, zimetoka tathmini za wataalam, tena report imetoka juzi tu ya wataalam wetu hapa nchini, wanatueleza; na uhalisia Wabunge wanafahamu. Uhusiano uliopo kati ya Local Government zetu na Serikali Kuu hasa kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni wa kimaelekezo; kwamba kazi kubwa ya Serikali Kuu ni kuelekeza mamlaka zile na mamlaka kutekeleza. Kwa hiyo, siyo ushauri. Hivyo, ile dhana ya kwanza ya kuipa mamlaka Serikali za Mitaa inapotea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la pili ambalo ni muhimu, ni kiwango kidogo cha ushirikishwaji wa wananchi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Tulisema wananchi washiriki kwenye kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo. Kwa sasa kwa kweli ukifuatilia kwa karibu, na tathmini zinaonesha hivyo, wananchi wengi wamekuwa wapokeaji na washangiliaji wa mafanikio ya miradi ya maendeleo. Ushiriki unazidi kupungua.
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu ni lile ambalo pia kwenye hotuba ya Mwalimu amelizungumza. Kwa wakati wake aliona kwamba changamoto na sifa zote zilikuwa zinaelekezwa kwake. Ni kwamba changamoto zote ni kwake na zikitokea sifa za mafanikio zinaelekezwa kwake. Jambo hili halikumpendeza na akalikemea. Naomba ninukuu maneno yake aliyoyasema. Alisema kwa Kiingereza: “our President is important, but he is not Tanzania. The Vice President and the President of Zanzibar are important, but they are not Tanzania. We; all of our people organized together, are Tanzania.” (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nasisitiza kwamba ni muhimu kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa miradi ya maendeleo na mafanikio yanayopatikana. Pia pale ambapo mafanikio yanapatikana ni muhimu sana wananchi waonekane kwamba ni sehemu ya mafanikio. Ni muhimu sana Halmashauri zetu zionekane kwamba ni sehemu ya mafanikio.
Mheshimiwa Spika, haiwezekani mradi wa maendeleo utekelezwe Kakonko halafu sifa zote ziende Serikali Kuu, sifa zote ziende kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, sifa zote ziende kwa Waziri Mkuu, sifa zote ziende kwa Mheshimiwa Rais, siyo sahihi. Lazima utukufu wa mafanikio pia ugawanywe ili ile sense of ownership iwepo miongoni mwa wananchi. Kwa sababu wanapoona kuwa miradi tumetekeleza, tumesifiwa sisi, mafanikio ni yetu, ile sense of ownership inakuwepo. Vilevile changamoto zikitokea, haiwezekani changamoto zote zimetokea, tumwelekeze mtu mmoja au watu wawili. Lazima tuwe na sense of ownership ya changamoto na mafanikio. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la tatu la kurekebisha ni lile ambalo limejitokeza. Tumesema tunatekeleza Sera ya Ugatuaji, lakini ukweli ni kwamba hii inaitwa devolution. Wataalam wa Local Government sasa wanasema kinachoendelea siyo devolution, isipokuwa ni deconcentration, kwa maana umemega madaraka kidogo yakashuka kule chini. Nami naita ile ni ugutuaji, siyo ugatuaji ni ugutuaji. Turudi kwenye sera yetu ya msingi ya ugatuaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ambalo nataka kuchangia kwa sababu kengele ya kwanza imegonga, ni eneo hili ambalo Mheshimiwa Waziri Mkuu amelieleza kwenye hotuba yake ukurasa wa 78 mpaka 83. Ni hoja kuhusu upandaji wa bei za bidhaa na hatua ambazo Serikali inazichukua; nami naunga mkono zile hatua ambazo amezieleza pale ikiwemo kudhibiti wafanyabiashara wasipandishe bei holela. Pia ameeleza vizuri sababu za mfumuko wa bei na bei ya mafuta kupanda.
Mheshimiwa Spika, maelezo ni mazuri, lakini maelezo peke yake hayatoshi. Muhimu sana kwa Serikali ni kwamba Serikali inachukua hatua gani kuwapunguzia wananchi makali ya maisha kutokana na kupanda kwa bei? Hili ni jambo la msingi. Sote tunajua bei zimepanda katika hali ambayo siyo ya kawaida. Chukua mfano, kati ya Aprili mwaka 2020/2021 bei ya mafuta ilipanda kwa wastani wa shilingi 36, lakini Aprili, 2021/2022 hii ya juzi, imepanda kwa shilingi 738. Siyo kiwango cha kawaida cha upandaji wa bei ya mafuta. Sote tunatambua kwamba siyo kwa sababu yetu au Serikali, lakini hoja ya msingi kwa Serikali ni kwamba, inachukua hatua gani kuwapunguzia wananchi makali? Waingereza wana msemo unaosema, desperate times calls for desperate measures. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, maoni yangu ni kwamba tuko katika kipindi ambacho siyo cha kawaida na Serikali lazima ichukue hatua ambazo siyo za kawaida. Ushauri wangu hapo ni kwamba Waziri wa Fedha na Mipango na Kamati yetu ya bajeti, haraka iwezekanavyo wakae waangalie katika bajeti yetu ni wapi tunaweza kuchukua hatua za kusaidia?
Mheshimiwa Spika, mapendekezo yangu ni kwamba katika zile levy, shilingi 792 ambazo zinakusanywa moja kwa moja kama Levy kwenye mafuta, Kamati ya Bajeti inaweza ikashauri tukachukua shilingi 300/= mpaka shilingi 400/=, tukaondoa kwa muda mfupi kwa miezi mitatu au minne tukitarajia kwamba mwezi Julai mpaka Agosti, kwa jinsi wataalam wanavyosema, hali itarudi kama kawaida. Tukifanya hivyo, tutakuwa tumempunguzia mwananchi ukali wa maisha. Hizo fedha ambazo zinapungua kwenye miradi ya maendeleo, sasa hivi Serikari yetu bahati nzuri inakopesheka, ikope ili miradi ya maendeleo isisimame. Hayo ndiyo mapendekezo yangu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, narudia tena, desperate times calls for desperate measures. Hatupo katika hali ya kawaida, lazima Bunge lako lichukue hatua ambazo siyo za kawaida. Inapofika wakati wananchi wanaumia, msemaji wao mkubwa katika nchi ni Bunge. (Makofi)
MheshimiwaSpika, Bunge hili haliwezi kukaa kimya; haliwezi kuridhika tu na maelezo ya Serikali kwamba maelezo bei zimepanda kwa sababu moja, mbili, tatu; haitoshi. Muhimu sana tunachukua hatua gani kupunguza makali ya maisha kwa wananchi? Hili ndilo jambo la msingi, na Serikali hii ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa jinsi alivyoonesha upendo mkubwa kwa wananchi wake, naamini tukimshauri atachukua hatua. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)