Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia katika hotuba ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, najikita kwenye ukurasa 33 ambapo ameainisha kwamba Serikali imeendelea kutekeza miradi ya ujenzi wa Mahakama mbalimbali nchini. Tuna kero kubwa ambayo ni kwikwi katika Taifa ni mlundikano wa mahabusu ndani ya Mahakama na wafungwa, hii ni kero kubwa kwa Taifa na inasababisha athari kubwa.
Mheshimiwa Spika, mpaka hapa tunapoongea mahabusu na Mahakama ndani ya nchi yetu wako zaidi ya 30,000 hawa zaidi ya 30,000 ni kiwango cha juu kabisa tumeshazidi yaani Mahakama zetu zimekosa uwezo na Magereza wa kuweza kumudu hawa watu.
Mheshimiwa Spika, nilijua mkakati utakuja madhubuti katika kutekeleza hili ili tuweze kupambana na adha hii, kwa sababu ndani ya Magereza kuna vitu vingi. Kuna kesi ambazo ni kesi za ajabu, yaani unakwenda Magereza unaenda kutembelea wafungwa unakutana na msichana amepoteza 10,000 ya bosi wake, yuko pale miezi nane, ni kesi ngumu.
Mheshimiwa Spika, ninapendekeza kwa sababu wale wakiwa kule tayari wana-adopt tabia ngumu na mbalimbali mbaya ambazo kwenye jamii hazikubaliki, ni bora tungekuwa na sera maalum au utaratibu wa kuweza kuchukua haya makosa madogo madogo na kuwafunga vifungo vya nje. Tukifanya hivi tunaweza kusaidia kupunguza adha ya mlundikano wa Magereza zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kingine kikubwa Magereza yetu pia yamejaza katika hao 30,000 kuna wakimbizi ndani yake ambao hapa nchini kwetu wanapita tu au hii ni njia. Kwa hiyo, hapa wanatokea Nairobi, wanakuwa-charged hela wanapita, hapa sisi tunaenda kuwekeza pesa tunajenga self- house tunawaweka, wanakula pesa za Watanzania, pesa za walipa kodi, halafu kifungo kikiisha wanaangalia tu kama kawaida. Kwa hiyo, tunapoteza fedha nyingi kutumia kwa hao watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa tuna takwimu ya wakimbizi 5,756 wako Tanzania na kwa siku mtu mmoja anakula shilingi 2,500 mara idadi hiyo, kwa siku wanakula zaidi ya shilingi milioni 14, ukihesabu kwa mwaka ni zaidi ya shilingi bilioni tano. (Makofi)
SPIKA: Sawa. Mheshimiwa Felista Njau tusaidie jambo moja, hawa ni Wakimbizi au wahamiaji haramu?
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, ni wahamiaji haramu.
SPIKA: Eeh! Ni lazima taarifa yako iwe inawasema hivyo kwa sababu Wakimbizi kuwekwa ndani tena inakuwa kidogo siyo sahihi.
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, sawa. Hao wahamiaji haramu ambao wanaopita, kwa hiyo wanatumia shilingi zaidi ya bilioni tano milioni mia moja kumi na moja ambazo ni pesa za walipa kodi ya Watanzania. Ukikaa ukafikiria unaweza ukaona labda, halafu hakuna mtu anayeshtuka wala hakuna hatua, kikubwa ingewezekana wakifika hapa wachukuliwe na escort mpaka mpakani wanapoelekea ili tuokoe hii pesa ya Watanzania ambayo inachukuliwa bure na hawa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wakati tunazungumza haya ziko hospitali hazina dawa, wakati tunazungumza haya ziko barabara mbovu, pesa hii ingeweza kuelekezwa kule na ikaleta tija. Ukijumlisha hii pesa kwa pesa ya Tanzania kwa darasa moja la Shilingi Milioni 20 unajenga madarasa 250, kitu ambacho hili tungelichukua kama special case tukaenda nalo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, jambo lingine gumu wahamiaji hawa haramu wapo waliotumikia kifungo chao, wamemaliza kifungo na wapo nchini 2,200 wanakula pesa za walipa kodi, wanakula pesa za Watanzania, wahamiaji haramu 2,200 wapo tu wamemaliza kifungo, hawapelekwi kwao, hawako ndani wako tu pale wanambwela wanakula hela za Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninaomba hatua zichukuliwe Uhamiaji, Mambo ya Ndani na Polisi washirikiane katika hili ili kuokoa pesa nyingi za walipa kodi zinazopotea. Tunalia adha ya umaskini, tunalia janga, sasa hivi tuko kwenye umaskini mkubwa huko nje kila mtu ana kilio, lakini pesa hii ingeweza kuwezesha hata vikundi vya akina mama ambao leo wanatembea wana adha kubwa, hili tulichukue kwa unyeti wake ili lilete tija kwa Taifa letu. (Makofi)
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, taarifa.
T A A R I F A
MHE. ALI HASSAN OMAR KING: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Felista Njau, kati ya hawa Wahamiaji Haramu ambao wamemaliza kifungo chao wamekuja jamaa zao kuwataka wasafirishwe, basi bado kuna ugumu wa kuwatoa na bado tumewashikilia. Nataka nimuongezee hiyo taarifa. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Felista Njau unaipokea taarifa hiyo?
MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika suala hili niombe Wizara ziungane ili kulitatua kwa wakati na kwa muda ili kuokoa pesa hizi zinazopotea.
Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ninataka nilichangie kwa ufupi ni kwamba kuna kipande cha barabara inayotoka Morogoro kuja Dodoma, hiki kipande ni kama vile watu hawaoni, lakini ni kipande kigumu ambacho kina mabonde, ukisafiri usiku unaweza ukafikiri haupo Tanzania, lakini kwenye barabara hiyo kwa siku unakutana na malori manne, matano yamedondoka yako chini, hakuna effort zozote zinazochukuliwa katika kurekebisha barabara hii ambayo umuhimu wake mkubwa kwanza ni barabara inakuja Makao Makuu ya nchi.
Mheshimiwa Spika, pili, barabara hii inaunganisha nchi za jirani kwa maana ya Uganda, kwa maana ya Congo, kwa maana ya Rwanda, kwa maana ya Burundi. Barabara hii ni ya msingi kwa maana ya diplomansia yetu ya kiuchumi, inasafirisha malori yanayosafirisha bidhaa kuelekea nchi mbalimbali, lakini imesahaulika kabisa.
Mheshimwia Spika, lakini kwenye barabara hiyo kwa siku unakutana na malori manne mpaka Matano yamedondoka, na hakuna efforts zozote zinazochukuliwa katika kurekebisha barabara hii ambayo umuhimu wake ni mkubwa. Kwanza inakuja makao makuu ya nchi, pili, barabara hii inaunganisha nchi za Jirani za Uganda, Congo, Rwanda pamoja na Burundi. Kwa hiyo, barabara hii ni ya msingi, kwa maana ya diplomasia yetu ya uchumi kwa sababu malori yanasafirisha bidhaa kuelekea nchi mbalimbali, lakini imesahaulika kabisa.
Mheshimiwa Spika, mwaka jana, nafikiri ni Oktoba, Msemaji wa Serikali alisema tayari upembuzi yakinifu umefanyika tunatafuta Mkandarasi, lakini naona kuna ukimya mkubwa katika barabara hii. Naomba tulichukulie kipaumbele kwa sababu Wabunge wanapita hii barabara na watakuwa ni mashahidi wangu, barabara ni mbovu kwa kiwango cha tofauti. Naomba hilo lichukuliwe kama ushauri wangu. Ahsante. (Makofi)