Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kunipa nafasi hii ili na mimi kwa niaba ya wananchi ya Jimbo la Bukene niweze kuchangia hotuba hii ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia Afya njema, lakini niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kazi kubwa wanayofanya na kupeleka fedha nyingi za maendeleo katika maeneo yetu kule. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitazungumzia maeneo ambayo yametajwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu na nitazungumzia kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa mwaka 2022/ 2023. Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2022/2023 ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango mkubwa wa Miaka Mitano unaoanza 2021/2022 hadi 2025/ 2026. Huu mpango wa miaka mitano umegawanywa katika mipango mitano ya mwaka mmoja mmoja. Mpango wa kwanza ulikuwa huu wa mwaka 2021/2022 na sasa hivi tupo kwenye mpango wa pili wa 2022/2023 ambao ndio mapendekezo yake yameletwa rasmi ili sisi Waheshimiwa Wabunge tuyajadili na kuweza kutoa maoni yetu.

Mheshimiwa Spika, sasa jambo moja kubwa ambalo nimeliona katika mapendekezo ya mpango huu wa 2022/2023 ni mwendelezo wa miradi ya kielelezo na kimkakati ambayo ilianza mwaka uliopita wa mpango. Mradi mmoja wa kimkakati na kielelezo ambao umetajwa ndani ya mpango huu ni mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga. Wote tunafahamu faida kubwa ambazo nchi yetu itapata kutokana na ujenzi wa bomba hili la mafuta.

Mheshimiwa Spika, kwetu sisi watu wa Jimbo la Bukene Mradi huu wa Bomba la Mafuta kutoka Hoima Uganda mpaka Tanga una umuhimu wa kipekee sana pale kwangu kwenye Jimbo la Bukene ndipo itajengwa project moja kubwa sana inaitwa Courting Yard ambayo itagharimu zaidi ya shilingi bilioni 600. Hii Courting Yard ndio project ambayo mabomba yote ya mradi huu, mabomba yote yatakayolazwa chini kutoka Hoima mpaka Tanga yatapakwa rangi maalum ili yaziweze kuoza hiyo shughuli yote itafanyika ndani ya Jimbo langu la Bukene eneo linaitwa Sojo ambako wananchi wameshahamishwa hekari 140 zimeshatwaliwa tayari kwa kuanza ujenzi mkubwa wa project hii ambayo itagharimu zaidi ya Bilioni 600. Kwa hiyo, bilioni 600 zinakwenda kuwa injected ndani ya jimbo langu na nina uhakika kabisa itatokea multiplier effect kubwa sana ya kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, nashukuru shughuli zinakwenda vizuri, wale wananchi waliopisha hizo ekari 140 wote wameshalipwa fidia. Waliotaka kulipwa cash wamelipwa, waliochagua kujengewa nyumba wamejengewa na shughuli hii imekwenda vizuri. Jambo ambalo napenda kusisitiza hapa ni manufaa ya ajira ambayo nimekuwa nikiyasema mara zote na tumekuwa tukiahidiwa kwamba upendeleo maalum kwa watu ambao wanatoka maeneo ya karibu pale waweze kupata ajira ambazo hazihitaji utaalam mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata ile local content, makampuni ya pale yaweze kufanya supply kwenye makampuni ambayo yanafanya kazi pale. Hivi karibuni kuna kampuni ambayo itafanya ujenzi pale inaitwa ISOPH imekuja pale Nzega, imeanza vizuri imeitisha wafanyabiashara na wadau na kuwaeleza fursa ambazo zitapatikana pale.

Msisitizo wangu hapa kwa Ofisi ya Waziri Mkuu hasa sehemu ya ajira na kazi ni kama ambavyo nilikuwa nimeshaomba awali kwamba hawa wazabuni wa Tanzania, local ni lazima watambuliwe na wawezeshwe ili kushindana na makampuni mengine ya nje kwa sababu bila kufanya hivyo kazi zote zitachukuliwa na makampuni yale ya nje.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, haitoshi kuja tu pale kusema kutakuwa na kazi ya ku-supply chakula, kutakuwa na kazi ya ku-supply usafiri kwa maana ya kutoa mabasi, kutakuwa na kazi hizi, haitoshi kusema hivyo, lakini hawa wafanyabiashara wa ndani wazabuni wa ndani lazima watambuliwe na wasaidiwe kama wanachangamoto za kibenki wasaidiwe kupata mikopo, changamoto za kiuwezo ili waweze kushindana na makampuni ya nje yanayofukuzia kazi pale, kwa sababu bila ya kuwawezesha, bila kufanya jitihada maalum za kuwawezesha, kazi zote zitakazofanyika pale zitachukuliwa na makampuni ya nje. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pale Halmashauri yangu ya Nzega kutokana na thamani ya kazi zitakazokuwa pale, tunatarajia kupata ushuru wa huduma wa zaidi ya bilioni 1.8. Hapa Ofisi ya Waziri Mkuu itusaidie kwa sababu tulikubaliana kwamba sisi kama Halmashauri ya Nzega tutawasiliana na mtu mmoja tu wa EACOP badala ya kuwasiliana na yale makampuni madogo madogo ili ushuru wa huduma wa kampuni zote tuupate kutoka EACOP tu, ambao ndio wasimamizi wakubwa wa hiyo project yenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi mwingine ambao umetajwa katika mapendekezo ya mpango wa miaka mitano ni ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge, ninafahamu kwamba vipande karibu vyote kazi zimeanza na zinakwenda vizuri isipokuwa kipande cha Tabora mpaka Isaka kilometa 165 ambako ndiyo Jimbo langu la Bukene lilipo bado hatua za kumpata Mkandarasi ndiyo zinakamilishwa, lakini kwenye eneo hili msisitizo tu ni kwamba wananchi wa Jimbo la Bukene tunasubiri kwa hamu mradi huu wa reli ya kisasa kwa sababu pale Bukene itajengwa station kubwa ambayo itatumika kushusha mizigo na mizigo yote ambayo itahudumia Nzega na Igunga itashushiwa Bukene. Kwa hiyo, tunasubiri kwa hamu hii lot kipande hiki cha Tabora Isaka nacho kipate Mkandarasi ili shughuli ya ujenzi iweze kuanza kufanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine la faraja ambalo limezungumzwa katika mpango wa maendeleo wa miaka mitano ni kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya kilimo. Kilimo katika nchi yetu kimeajiri zaidi ya Watanzania asilimia 65, kwa hiyo kwa namna yoyote ile ukitaka kufanya mabadiliko kwa Watanzania ukitaka kuinua hali zao za kiuchumi, ukitaka kuinua hali zao za kimapato basi hakuna njia nyingine yoyote zaidi ya kufanya mapinduzi kwenye sekta ya kilimo. Kwa sababu ndiyo inaajiri asilimia 65 ya Watanzania wote.(Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tatizo la kilimo chetu ni tija yaani kilimo chetu hakina tija siyo kwamba watu hawalimi, wanalima lakini kilimo chao hakina tija na ili tupate tija kuna mambo ambayo huwezi ukayaepuka katika kilimo. Kwa hiyo, katika mpango zimeelezwa jitihada za kubadili namna yetu ya ulimaji kwamba tuende kwenye matumizi ya mbegu bora, tuende kwenye matumizi ya mbolea, tuende kwenye matumizi ya viuatilifu lakini na huduma za ugani.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu hapo ni kwamba, kuanzia sasa hebu tuwe na mipango ambayo inakuwa na malengo ambayo yanapimika ili kila baada ya mwaka tunakuwa na jambo ambalo tunaweza tukalipima tuepukane kuwa na malengo ya jumla tu kwamba malengo yetu ni kuongeza matumizi ya mbolea yaani sentensi ambayo is too general, au malengo yetu ni kuongeza matumizi ya mbegu bora lakini lazima tuwe na malengo specific tuseme tuwe na base lane, tuseme labda katika matumizi ya mbolea sasa hivi tuko wapi na baada ya mwaka mmoja tunataka tuongeze matumizi ya mbolea kutoka wapi kwenda wapi? Then baada ya mwaka moja tunaweza tukapima tukaangalia tumesonga mbele au hatujasonga mbele. Hivyo hivyo kwa mbegu bora, hivyo hivyo kwa viuatilifu.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine kubwa sana katika kilimo ambalo ni changamoto na linakosesha tija ni uhakika wa masoko na bei bora kwa mazao ambayo tunalima. Kwa hiyo, naunga mkono eneo hili kwenye mapendekezo ya mpango kutiliwa mkazo na kuongeza msukumo ili kuleta mapinduzi ya hali za maisha na kiuchumi kwa watu wetu, kwa sababu kilimo kinaajiri asilimia 65 na huwezi kuleta mabadiliko yoyote ya kiuchumi kama hujaleta mapinduzi ya kutosha kwenye sekta ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono asilimia100. Ahsante sana. (Makofi)