Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Kawe
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nakushukuru kwanza wewe kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyofanya kuwasaidia Watanzania. Pia nimshukuru Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hussein Mwinyi kwa namna anavyofanya kuisaidia Zanzibar. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa ufupi sana mimi nataka kujadili hoja iliyo mezani ya ofisi au hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nianze kwa kusema maneno haya, kwamba namshukuru sana Mungu, kwamba ninafikiri kuna sababu zinazoifanya nchi yetu ibaki pale ilipo kwa muda mrefu. Sababu mojawapo ambayo nimefikiri sana ni kwamba nchi yetu inahitaji dira au inahitaji ajenda ya taifa au maono ya taifa au mwelekeo wa taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, dunia ina mataifa kama 197 hivi lakini kuna mataifa 193 yanayokubalika na Umoja wa Mataifa. Kwa neema ya Mungu mimi nimewahi kufika zaidi ya mataifa 143, ni mataifa hamsini tu ya duniani ambayo sijawahi kufika. Lakini mshangao ambao nimekuwa nao sana kwa miaka mingi ni kwamba mataifa yote yenye watu wa asili ya Afrika, kwa maana ya ngozi yetu yanaasili za kufanana yana matatizo yanayofanana na yapo nyuma kwa aina ya kufanana. Suala hili limenifanya nijiulize sana kwa nini mataifa yenye asili ya watu wa Afrika wheather Latin America, or Afro- Caribbean kwa maana ya Jamaica Hyatt na mengine yana matatizo yanayofanana?
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja nikaligundua juu ya mataifa haya; kwamba mataifa haya hayana maono ya muda mrefu yanayoifanya nchi iwe guided kiasi kwamba kila utawala unapoingia katika mamlaka ufuate maono ya muda mrefu. Simaanishi kwamba hakuna maono kabisa, lakini hebu nitoe mfano kidogo. United Arab Emirates wana mpango wa kuanzia mwaka 2050 mpaka 2117 wa kuhamishia makazi ya kwanza katika Sayari ya Mars, ni mpango wa taifa wa muda mrefu. Lakini pia United Arab Emirates wana mpango wa kuwa nchi ya kwanza duniani katika nchi 10 zenye hifadhi ya chakula cha kutosha kufikia mwaka 2051. Vilevile, United Arab Emirates wana Mpango wa Taifa wa Clean Energy kuanzia 2020 mpaka 2030. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hakuna taifa lililoendelea duniani bila mpango wa muda mrefu. Tusipokuwa na mpango wa muda mrefu kasi ya maendeleo haitaenda kama inavyotakiwa. Niliwaza kwamba inawezekana labda tunashindwa kupanga mpango wa muda mrefu kwa sababu labda katiba haituruhusu au sheria haituruhusu. Nikasoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 63 (3)(c) inasema hivi: -
(3) Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake -
(c) kujadili na kuidhinisha mpango wowote wa muda mrefu au muda mfupi unaokusudiwa kutekelezwa katika Jamhuri hii ya Muungano, na kutunga sheria ya kusimamia utekelezaji wa mpango huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, nikaona kumbe katiba yetu inaruhusu, kwamba Serikali inaweza kuleta mpango wa muda mrefu wa namna ambavyo Tanzania iwe miaka 50 ijayo, Tanzania iwe miaka 80 ijayo ili kila utawala unaoingia madarakani ufuate maono ya nchi ambayo nchi imejipangia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hatari itatupata siku zijazo. Kwamba, ndiyo maana unasikia watu wanasema tunahitaji Rais mwenye maono, tunahitaji Rais mwenye maono kwa sababu nchi haina maono, tunahitaji nchi yenye maono ili kila Rais anayeingia madarakani afate maono ya nchi tuliyoiweka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama tutaruhusu kila mtu anayeingia madarakani aongozwe na kichwa chake anavyowaza yeye kuna siku tutapata Rais wa ajabu tutadondokea pua hatutaamini macho yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, unakumbuka vizuri baada ya vita vya pili vya dunia nchi za ulaya zilifilisika kabisa. Ukiangalia Wa-Marekani wakaanza mpango unaoitwa marshal plan, marshal plan kipindi kile Rais wa Marekani alikuwa Truman, wakaanza mpango wa kuzisaidia nchi 17 za ulaya magharibi zilizokuwa zimefirisika kabisa. Nchi hizo wakazipa almost dola bilioni 13 ambayo ni bilioni 115 kwa sasa. Marekani akawaambia kila nchi izalishe mpango wake wa muda mrefu na dira yake. Kila nchi ikazalisha dira yake, mpango wake na zikapewa hizo fedha; nan chi hizo zikatoka hazipo kama sisi tulivyo. Sisi mpango tulionao sasa ni kufikia tu 2026.
Mheshimiwa Naibu Spika, maombi yangu ni kwamba tuipe dira nchi yetu, tuwe na mpango wa zaidi ya miaka 50 au miaka 60 au miaka 100 ya Tanzania ijayo ili mitaala yote ya shule na ilani zote za chaguzi na watoto wote waweze kuiona Tanzania kwenye three D na waweze kujifunza na kuiona Tanzania ijayo; vinginevyo tutapoteza muda mwingi sana kwa kuzunguka pale pale na kufanya mambo yale yale. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikupe mfano; tumekuwa na regime iliyopita ilifanya vizuri sana. Tumekuwa na Rais wetu Mwalimu Nyerere aliendelea kwa namna yake akaja Mwinyi aliendelea kwa namna yake, lakini alipoishia Nyerere, Mheshimiwa Mwinyi hajaendelea pale, alipoishia Mwinyi, Mkapa hajaendelea pale, alipoishia Mkapa, Kikwete hajaendelea pale, alipoishia Kikwete, Magufuli hajaendelea pale tunakuwa kila Rais anayeingia madarakani anaanza chake na matokeo yake tutapata Rais wa ajabu tutaangukia pua hujawaji kuona. There is no country that can develop within a single regime, nchi zote zinazoendelea ni mwendelezo wa regime ya kwanza, regime ya pili, regime ya tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, na ili regime ibaki kwenye guidance lazima yawepo maono ya taifa ili Rais anayeingia madarakani ayatumikie maono ya taifa na sisi wananchi tuyaone kama maono ya taifa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima tu-define ni kitu gani sisi tunakiita maendeleo, tunachokiita maendeleo sisi si lazima kiitwe maendeleo Marekani. Kwa mfano; tunaweza kuwa na namna yetu ya kusema kwetu sisi maendeleo …
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gwajima sekunde tatu malizia.
MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: …kwetu sisi maendeleo kila mtu awe na maji safi, kwetu sisi maendeleo tuwe na hospitali. Kwa hiyo, ninaomba kusema ni muhimu sana nchi yetu iwe na Dira ya Taifa na Maendeleo ya Taifa ili kila Rais anayeingia madarakani awe mzuri awe wa namna gani asimamie maono ya nchi tuliyoyaweka na wala si maono yake mwenyewe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)