Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Arusha Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami niungane na wenzangu kushukuru sana kupata fursa hii adimu niweze kutoa mchango wangu kwenye Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Mwaka 2021 ajenda yangu kubwa ilikuwa utalii; mwaka huu ajenda yangu kubwa itakuwa ni sekta ya madini. Kabla sijaenda kwenye sekta ya madini, naomba nizungumzie changamoto tulizokuwanazo katika uwanda mzima wa biashara sisi kama Watanzania na pia kama Bunge. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Ukiangalia Sheria yetu ya Mwaka 2007, ukienda ukurasa wa 72 Kifungu cha 31, tunaambiwa kwamba “The Business Licensing Act of 1972 is hereby repealed.” Kwamba sheria hii ya mwaka 1972 ilifutwa, lakini cha kushangaza sheria hii ambayo ilifutwa mwaka 2007 kupitia sheria ya Business License Act ya 2007 Kifungu 31, bado tukaenda kuifanyia marekebisho mwaka 2014, 2015 na 2018. Yaani Bunge lako hili lilifuta sheria ya mwaka 1972, likaanzisha sheria ya mwaka 2007, lakini bado likaenda mwaka 2014 lirekebisha sheria ambayo ilishafutwa tayari. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye sheria hii ya mwaka 1972, ukienda kwenye ukurasa wa 9, kuna Act (No. 2) of 2014 Section No. 6; ilifanyia marekebisho ya sheria ambayo imefutwa. Pia ukienda kwenye ukurasa wa 12, mwaka 2015 yalifanyika marekebisho kupitia Sheria ya Fedha kwa kuongeza maneno yafuatayo, pia ilienda ikafuta na jedwali, yaani imekwenda kurekebisha kitu ambacho Bunge tayari ilishafuta.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo uone ni namna gani tulikuwa na changamoto kubwa katika nchi yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ukienda kwenye Sheria yetu ya Madini, ukiangalia kanuni yetu, tulikuwa na kanuni ya mwaka 2002 ambayo tulikwenda kuifuta mwaka 2019. Mara baada ya kuifuta, tukaja kufanya marekebisho mengine mwaka 2021. Kinachonishangaza, ukiangalia hii Kanuni, inasema imekuwa gazetted tarehe 2/7/2021. Nimekwenda kutafuta gazeti la Serikali la tarehe 2/7/2021, sijaikuta hii kanuni. Ila nimekwenda kuikuta kwenye gazeti la Serikali la tarehe 9/7/2021. Gazeti lenyewe pia ukiangalia bado limeandikwa tarehe 2/7/2021, ukija hapa ni la tarehe 9 Mwezi wa Saba. Kwa hiyo, utajiuliza, ni kweli sisi wote ni vipofu? Yaani Bunge, Wizara ya Madini, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wote hatuoni?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini yametokea haya? Yametokea haya kwa sababu tunajua Serikali inapotoa maelekezo, inatoa kwa nia njema sana na Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokwenda Mererani tarehe 2/7/2021, alitoa maelekezo kwamba Sheria ya Madini na Kanuni zake viweze kubadilishwa. Tarehe 8 wakabadilisha kanuni, Waziri akasaini, tarehe 9 tukai-gazette. Katika uharaka wa namna hiyo bila kushirikisha wadau, lazima kuwe na changamoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba sasa niende kwenye hoja ya msingi. Ukienda kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, ukurasa wa 37 kipengele cha 67, Mheshimiwa Gwajima alikuwa anashika documents zangu, isije ikawezekana kwamba ameziweka pembeni; inasema kwamba, “Serikali imeendelea kuimarisha usimamizi na kuanzisha masoko mapya ya madini na vituo vya ununuzi nchini kwa lengo la kupata takwimu sahihi za mauzo ya madini, kuongeza ukusanyaji wa maduhuli na kuwasaidia wachimbaji wadogo kupata soko la uhakika na kupata bei stahiki kwa bidhaa za madini.”
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu sote kwa mwaka, 2019 tulianzisha masoko ya madini. Arusha lilikuwepo, Mererani lilikuwepo na maeneo mengine mbalimbali katika nchi yetu. Kwenye masoko ya madini haya tulikuwa tunaruhusiwa kuuza madini ya aina zote, ukienda pale Arusha leo tuna madini kutoka Kongo DRC, kutoka Msumbiji, kutoka Ethiopia na kutoka Kenya, lakini tanzanite ambayo inapatikana Tanzania hairuhusiwi kwenda kuuzwa kwenye soko la Arusha. Maamuzi ya kubadilisha Kanuni yameipatia Serikali hasara kubwa sana naomba nikupe taarifa ifuatayo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, wakati linaanzishwa soko pale Arusha, nikichukua taarifa ya Julai hadi Disemba, 2019 tulipata carets 76,000 lakini kodi iliyopatikana ya Serikali ilikuwa ni shilingi milioni 487. Ukiangalia kwenye rough tanzanite tulipata kiasi cha kodi shilingi bilioni 1,300,000,000/= na point kadhaa. Ukija mwaka 2020 tuliweza kuwa na caret ya 85,000 tuliweza kupata kodi ya shilingi milioni 332 lakini kwenye rough tanzanite tuliweza kupata kodi ya shilingi bilioni 1.1.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuhamishia Mererani ukiangalia kipindi kile kile cha Julai, 2021 tumeacha Disemba hadi Januari, Serikali imepata kodi kiasi cha shilingi milioni 339 kutoka shilingi bilioni 1.3. Unaangalia kwenye upande wa caret tumeweza kuwa na caret 15,000 kutoka 85,000. Kwa hiyo, unaona kabisa maamuzi haya yamekwenda kuitia hasara Serikali lakini pia, kwa mujibu wa taarifa tulizokuwa nazo pale Arusha idadi ya dealers walikuwa ni 103, leo kuna dealers 48 tu kule Mererani. Kulikuwa kuna mashine za kukatia 427… (Makofi)
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.
T A A R I F A
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kumpa mtoa hoja taarifa kwamba madini ya tanzanite yapo katika Mkoa wa Manyara na katika takwimu zinaonyesha, Serikali imeweza kuongeza kipato toka soko liliporejeshwa katika Mji wa Mererani ambapo madini ndipo yanapochimbwa. Pia, imeweza kuwarahisishia wafanyabiashara pamoja na wachimbaji wadogo wadogo kuweza kuuza madini, kwa uhakika na usalama uliokamilika na kuendelea kuukuza Mji wa Mererani katika Mkoa wa Manyara. Hivyo, napenda kumpa mtoa mada taarifa kama anatamani madini ya tanzanite basi tunamkaribisha katika Mkoa wa Manyara, tuna maeneo makubwa bado tunahitaji wananchi wa kuja kuwekeza. Kwa hiyo, tunamkaribisha katika Mkoa wa Manyara ili apate madini. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Gambo taarifa hiyo.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwamba Wabunge watafute hoja za kuchangia sio tunadandia tu mradi tuonekane na wananchi wetu. Hapa tunaongea mambo serious, kwa hiyo sipokei taarifa yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna ajira ambazo zimepotea, ajira zaidi ya 413, kuna ma-broker pale kati ya 2,500 – 3,000 ambao pia wamekosa ajira. Hata hivyo, Serikali ikiwa imepata hasara Soko la Madini la Arusha inahusisha majengo ya AICC, NSSF na PSSSF. Serikali imepata hasara kiasi cha shilingi milioni 128 ambazo zilikuwa zinalipwa na wafanyabiashara wa madini kwenye maeneo hayo. Naomba nitoe mapendekezo na ushauri kwa sababu wote tunajenga nyumba moja. Mapendekezo yangu; la kwanza, tunaomba masoko ya madini ambayo yameanzishwa kwa mujibu wa taratibu za nchi hii, yaruhusiwe kuuza madini ya aina zote, maana inashangaza kuona leo Tanzanite unachukua Mererani… (Makofi/Kicheko)
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
NAIBU SPIKA: Kengele ya pili hiyo, malizia sekunde mbili, Mheshimiwa Gambo.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, unakwenda kuiuza India na Tanzania haipatikani. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Kengele hiyo ya pili, sekunde mbili malizia.
MHE. MRISHO M. GAMBO: Kwa hiyo, napendekeza pia Mererani ibaki sehemu ya uzalishaji wa tanzanite na soko la malighafi kwa mfumo wa mnada mara moja au mara mbili kwa wiki. Kwa sababu… (Makofi)