Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Spika, nikiwa Mbunge ambaye kwenye Jimbo langu kuna wanajeshi wengi wastaafu, ninawajibika kutoa sauti yao ili pale ambapo itatokea Serikali itasikiliza basi na wao waweze kupata neema.
Kabla sijaanza mchango wangu nitambue mchango wa masemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni. Vilevile nitambue mchango mzuri sana wa Mheshimiwa Nahodha na aliyewahi kuwa Waziri wa Ulinzi. Ni imani yangu kwamba Mheshimiwa Mwinyi utayasikiliza na Serikali hii Wizara na Taasisi zake na Idara mbalimbali za Serikali zione zina jukumu la kufanya kazi collectively kwa sababu Serikali ni moja na siyo kila mtu anaibuka na la kwake ndiyo maana kunakuwa na mkanganyiko wa aina hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna hoja ambazo tulishazizungumza miaka miwili mitatu iliyopita. Imezungumzwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, suala la migogoro baina ya Jeshi na wananchi. Ninaomba Mheshimiwa Waziri utakapokuwa unahitimisha leo naomba utueleze hatma ya mgogoro wa Kijiji cha Tondoroni kipo Kisarawe, mwaka jana, mwaka juzi nilizungumza kwenye hotuba ya ya Wizara ya Ardhi. Ningependa vilevile utupe hatma ya Kijiji cha Ihumwa, Dodoma, lakini vilevile Makuburi kwenye Kambi ya Jeshi wananchi sasa hii ni tofauti kwa sababu kwenye suala la Makuburi ni wananchi waliingia eneo la Jeshi kukawa na utaratibu ambao umefanyika Jeshi likaweka beacons upya. Sasa haieleweki hali ikoje sasa hivi ni muhimu vilevile ukatolea tamko ili wananchi wa maeneo yale waweze kukaa kwa amani.
Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya pili ni pensheni ya wanajeshi wastaafu. Mheshimiwa Waziri huu ni mwaka wangu wa kumi na moja (11) Bungeni, katika kipindi chote hicho nikisimama kwenye hili Bunge Tukufu ninazungumzia suala la pensheni. Mheshimiwa Mkapa aliongeza kima cha chini kutoka shilingi 25,000 mpaka 50,000, Jakaya Kikwete akaongeza kima cha chini kutoka shilingi 50,000 mpaka 100,000, kima cha chini! (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaambiwa Sir Major kwa waliostaafu kipindi cha mwaka 2009 kushuka chini analipwa shilingi 190,000 kwa mwezi, kwa maisha ya sasa hivi hawa wanajeshi wetu wanaishije? Mheshimiwa Waziri, tunajua Rais ana dhamana ya kuongeza vima vya chini, tunajua Rais ana dhamana ya kuangalia hivi viwango, tunaomba hili suala lifanyiwe kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ninamshukuru Mwenyekiti wa Kamati amesema kuna mapendekezo, kwa sababu tulikuwa tukisema hizi hoja, yanakuja maelezo kwamba kwa mwaka 2009 mpaka sasa kwasababu ya mishahara yao na blah blah nyingi. Lakini tunafahamu kwamba mwaka 2008 na 2009 utafiti ulifanywa mapendekezo yakatolewa, hivi kizungumkuti ni nini, hivi shida kweli ni fedha? Leo tunalalamika kuna uhalifu wa kijeshi, mabenki yanaibiwa, hivi kama mtu unalipwa laki tano kwa miezi mitatu kwa sukari ya shilingi 4,000, sukari tu, shilingi 4,000 mpaka 6,000 hivi utaacha kwenda kuiba benki? Wakati una uwezo wa kutumia silaha? Kwa hiyo, ninakuomba Mheshimiwa Waziri, hawa wastaafu wetu tuwaangalie kwa jicho pana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka 2009 lilijibiwa swali hapa Bungeni, tunakumbuka kuna wanajeshi wetu hawa hawa wastaafu; mwaka 1978 walishiriki kwenye vita Uganda, mwaka 1978 na 1979. Serikali ya Uganda ikatoa kiinua mgongo cha shilingi bilioni 59; Mheshimiwa Khalifa aliuliza swali hapa 2009 miaka saba iliyopita, hii hela imetolewa. Serikali mkajibu hiki kifuta jasho kwa wanajeshi wetu tutawapa, miaka saba baadaye mmechikichia na mkwanja wa watu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunaomba leo mtujibu kwamba hiyo shilingi bilioni 59 ambayo ilikuwa ni kifuta jasho cha wanajeshi wetu waliopambana usiku na mchana kuokoa nchi yetu kiko wapi? Naomba ujibu leo hapa usije ukatuambia ooh, muda hautoshi, nataka ujibu, kwa sababu wanajeshi wastaafu wanataka wajue ile fedha imekwenda wapi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanajeshi wetu wanasema kama Serikali imeamua kwamba mnawapa hiki kiinua mgongo, ama pensheni ya chini chini, hivi kweli Serikali hatuwezi kufikiria kuandaa mfumo wa bima ya afya? Bima ya afya kwa nini, kwa sababu tunaweza tukatumia utaratibu huo huo wa hiyo pensheni ndogo wakati tunajipanga kuongeza kwa makato hayo hayo, ili wanajeshi wetu wastaafu waweze kwenda kupata tiba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wanasema mmewaambia wakiugua wataenda watatibiwa Lugalo. Mimi wakazi wangu wanajeshi wananiambia wakienda Lugalo wengi wao wananyanyapaliwa, wanachokwa! Unahudumiwa bure siku ya kwanza, na unajua uzee ni maradhi, siku ya pili, siku ya tatu unanyanyapaliwa. Wanasema kabisa tunaona wenzetu wakienda mwingine ana kufa, wa pili ana kufa, wa tatu ana kufa; wanahisi labda ukienda pale unadungwa sindano kumbe mtu tu amekufa kwa ugonjwa wake wa kawaida. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo sisi tunaomba Serikali ifikirie, tunaweza tukaitumia pensheni hii ndogo, kuwakata makato kidogo kukawa kuna uhakika wa kupata tiba hawa wastaafu wetu na watoto wao. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, matumizi ya Jeshi Zanzibar. Mimi ni miongoni mwa watu ambao ninalipenda sana Jeshi letu, wanafanya kazi kubwa mno…
MHE. SULEIMAN M. NCHAMBI: Taarifa Mheshimiwa Spika.
SPIKA: Taarifa Mheshimiwa...
MHE. HALIMA J. MDEE: Nakushukuru kwa kumsaidia kwa sababu siyo size yangu. (Kicheko)
Mheshimiwa Spika, nilikuwa namalizia hoja yangu kwa kusema hivi, natambua kazi nzuri sana ya Jeshi letu, lakini ni muhimu ikaeleweka kitu kimoja, tukiendelea kutumia haya majeshi Mheshimiwa Waziri kwenye ukurasa wako wa 19 unasema ugaidi na uharamia. Ni muhimu tukaelewa ugaidi unatengenezwa ndani, watu wanapokuwa oppressed na kuchoka na kukata tamaa wanajengewa fikra za kufanya mambo ambayo walikuwa hawafanyi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo unapoona mwenzio ananyolewa wewe tia maji. Kina Al Shabab, kina Boko Haram hawakuanza out of nowhere, watu walikuwa suppressed. Sasa for the sake of this country, for the sake ya kizazi kichanga, average ya kizazi cha Tanzania ni miaka 18, kwa hiyo haiingii akilini watu wazima wenye tamaa ya mamlaka wanalazimisha kubaki Zanzibar wakati Wazanzibar hawajawachagua kwa kutumia Jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Wabunge wa Zanzibar walikuwa wanakuuliza Mheshimiwa Waziri wa Ulinzi, wakati wa maandalizi ya kinachoitwa uchaguzi wa marudio, Mheshimiwa Waziri kuna mazombi, mazombi wanaandikisha madaftari, mazombi wanapiga watu, Waziri unakataa hakuna mazombi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini kipindi cha uchaguzi, kipindi kuelekea uchaguzi tunaona watu na mask, tunaona mazombi wamepigwa picha. (Makofi)
SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Halima, nakushukuru muda haupo upande wako. Tunashukuru kwa mchango wako, huku Bara mnatuacha barabarani ninaposikia mazombi najiuliza zombi ndiyo nini? (Kicheko)