Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Hassan Zidadu Kungu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Na mimi pia niungane na Wabunge wenzangu kuipongeza bajeti hii ya Waziri Mkuu. Nimpongeze Waziri Mkuu pamoja na wataalam wote waliohusika kuiandaa bajeti hii. Lakini pili, nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kutupa miradi mingi kwenye majimbo yetu na sisi Wabunge wote ni mashahidi, tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa, nianze kwa kuchangia upande wa afya. Wilaya ya Tunduru tuna Hospitali ya Wilaya ambayo ni kongwe kweli kweli. Hospitali ile imejengwa mwaka 1905, majengo yake mpaka hivi sasa ni chakavu kweli kweli. Niliwahi kukutana na Waziri wa TAMISEMI, kwa kipindi kile, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, nilipiga picha ile hospitali majengo yake nikamuonyesha ili kutaka kuomba fedha ya ukarabati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ummy Mwalimu yeye mwenyewe akaridhia akasema kwamba, majengo haya kama tunakarabati ni sawa na kupoteza fedha za Serikali. Kwa hiyo, tukashauriana kwamba nitafute eneo ambalo tunaweza kupata hospitali mpya ya wilaya. Bahati nzuri tumepata hekari 20 ambapo tunaweza kujenga hospitali mpya ya wilaya, pamoja na nyumba za watumishi wa afya.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na uchakavu wa hospitali ile ya wilaya bado pia ina idadi chache sana ya watumishi. Ikama yake ni asilimia 55 katika 100. Lakini pia, katika hospitali ile tunao pia uhaba wa mtoa huduma wa mionzi, yupo mmoja tu. Sasa anapopata dharura ya kuugua ama akasafiri kwa muda wa wiki nzima maana yake huduma ya X-Ray inakosekana kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru hotuba hii ya Waziri Mkuu imezungumzia watumishi kwa hiyo, niombe watumishi watakapopatikana basi tuangaliwe sana katika Hospitali ya Wilaya ya Tunduru. Lakini pia, upande huo huo wa afya tukienda kwenye vijiji vyetu kuna zahanati, lakini katika zahanati zile bado watoa huduma wa afya ni wachache mno. Zahanati nyingi zina mtoa huduma wa afya mmoja mmoja. Tunazo zahanati takriban 11 ambazo zina mtoa huduma wa afya mmoja mmoja. Kwa mfano, Zahanati za Kidodoma, Nampungu, Majala, Cheleweni, Kitanda, Twende Mbele, Kajima, Kalulu, Mkowela pamoja na Zahanati ya Machemba. Hizi zote zina watoa huduma wa afya mmoja mmoja. Sasa, wanapopata changamoto ama dharura ya kawaida, ama siku wanakwenda kupokea mshahara mjini basi zahanati zile huwa zinafungwa na watu wanakosa huduma kabisa ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia upande wa elimu, nako kuna walimu wachache kweli kweli. Shule nyingi zina walimu wanne mpaka walimu watatu. Kwa hiyo tunaomba ajira hizi za walimu zikipatikana basi tuangaliwe kwa macho mawili kweli kweli.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kutupatia shule za sekondari, na shule zile tayari tumeanza kuzijenga. Lakini kuna jambo ambalo limejitokeza, ama BOQ inaeleza kwamba tujenge kwa kuilaza tofali. Sasa, tunaona, tangu tumeanza mwanzo shule nyingi zinajengwa kwa tofali za inchi sita, na tofali zile zinakuwa zimesimama na majengo yanadumu na yapo mpaka leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia, BOQ inaeleza kwamba tulaze tofali kwenye majengo yote. Sasa tukiangalia kwa namna ya wingi wa majengo na idadi ya fedha iliyopo kwa kweli tunaona kana kwamba bado haitoshi, na kwamba tutahitaji fedha iongezeke zaidi. Kwa hiyo, kwa namna ya kujenga tofali kwa kuilaza kwa kweli bila shaka tunaweza kuwalaumu Wakurugenzi, kwa sababu ya kwamba fedha haikidhi majengo ni mengi. Kwa hiyo, niishauri TAMISEMI, kupitia wakandarasi wake ama mainjinia waangalie namna nyingine ya kuweza kutoa BOQ, ambayo inaeleza tujenge tofali la inchi sita kwa kawaida kwa namna tunavyojenga ya kusimama badala ya kulaza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Tunduru tulikuwa na uwanja wa ndege. Uwanja wa ndege ule una miaka zaidi ya 20 sasa haufanyi kazi, na kwa tafsiri sahihi ni kwamba umesimama ama umefungwa kabisa, haupo; na eneo lile lipo katikati ya mji. Kwa hiyo nilikuwa naomba Serikali, ikiwezekana eneo lile litolewe na wagawiwe wananchi ili wafanye shughuli za maendeleo, kama vile ujenzi wa nyumba za makazi; nilikuwa naomba sana hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia kuhusu miundombinu ya elimu ya msingi, ambayo kwa kweli ni mibovu sana. Tunaishukuru Serikali kwa fedha ile za UVICO upande wa elimu ya sekondari tuko vizuri. Sasa, nilikuwa naomba tugeukie kwenye upande wa shule za msingi. Miundombinu ya elimu ya shule za msingi imechakaa mno, tena sana. Lakini pia, shule hizo hizo za msingi pamoja na miundombinu hiyo ya elimu hazina vyoo kabisa. Unakuta shule moja ina uhaba wa matundu 22, shule nyingine ina uhaba wa matundu 30. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana kwenye upande huu, basi na sisi tuweze kukaa sawa sawa na hatimaye tuweze kuboresha elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tunavyo vituo vya afya ambavyo vinafanya kazi vizuri lakini pia, vituo vile, kwa mfano Kituo cha Afya cha Nakapanya jengo la upasuaji limekamilika. Tunayo Ambulance, tunamshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuja kwenye kuomba kura tulimuomba na alituahidi kutuletea; na tunamshukuru tumepata Ambulance. Hata hivyo upasuaji haufanyiki kutokana na kwamba tumekosa baadhi ya vifaa vichache ili hospitali ile, tuweze kupata huduma ya upasuaji na hatimaye tumsaidie mama na mtoto. Vilevile katika Kituo cha Afya cha Matemanga majengo yote yamekamilika na vifaa vyote… (Makofi)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa, taarifa, taarifa.

NAIBU SPIKA: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nataka nimpe taarifa kaka yangu Hassan Kungu kwamba, ni kweli kabisa kile Kituo cha Afya cha Nakapanya, kutoka Nakapanya mpaka Makao Makuu ya Wilaya ni kilomita 80, ambapo wanawake wengi sasa wamekuwa wakijifungulia njiani. Sasa ni vizuri sasa Serikali ikasaidia kuleta hivyo vifaa kukamilisha kwa haraka sana ili wanawake hao wasiendelee kupata adha hii ambayo wanajifungulia barabarani. Ahsante. (Makofi)

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hii kwa mikono miwili. Lakini pia, kwa kuongezea hapo, akina mama wajawazito huwa wanakwenda Wilaya ya Jirani ya Nanyumbu kwenda kufuata huduma ya upasuaji, na hatimaye Mbunge wa kule huwa ananitania sana kwamba hatuna Vituo vya Afya. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Serikali tupate hivyo vifaa tukamilishe na tuweze kutoa hiyo huduma. Lakini pia, Kituo cha Afya cha Matemanga majengo yote yamekamilika vifaa vyote vipo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)