Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Iramba Mashariki
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ALLAN J. KIULA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii na mimi kuweza kuchangia hotuba hii. Pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Iramba Mashariki kwa kuweza kuniamini niweze kuwawakilisha badala ya wao 188,000 kuingia humu ndani ya Bunge.
Mheshimiwa Spika, ninapongeza hotuba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, kwa maana mimi ni Mjumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, mambo mengi ambayo tuliyoyazunguza tuliyoyajadili kwenye Kamati yamepewa nafasi yake, ushauri umezingatiwa, kwa sababu ushauri umezingatiwa tunaamini kabisa kwamba utekelezaji wake utakuwa kama ulivyowasilishwa.
Mheshimiwa Spika, pia ninalipongeza Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa kazi kubwa linayofanya na limetoa taswira nzuri ndani ya nchi na nje ya nchi. Tunapozungumza mambo ya ulinzi na usalama ni masauala nyeti. Tunasema masuala nyeti kwa sababu yuko Mbunge hapa alizungumza akasema maendeleo yoyote tunayoyategemea, maendeleo ya viwanda, maendeleo ya kilimo, huduma nzuri za afya, lazima usalama uwepo.
Mheshimiwa Spika, tumeona matukio ya kigaidi, matukio ya uharamia, vituo vya polisi kutekwa, lakini Jeshi la Wananchi wa Tanzania ni nguvu ya ziada ya kuweza kuhakikisha kwamba kunakuwepo na usalama ndani ya nchi yetu na Taifa linakuwa salama na tunaweza kufanya shughuli zetu kikamilifu.
Mheshimiwa Spika, mama akipika maandazi nyumbani watoto wakila na wakishiba unaweza ukakuta wanacheza mpira, sasa mambo yote haya tunayasema kwa sababu kuna amani na utulivu, tunatembea tunavyotaka, tunafanya mambo yetu tunavyotaka, ndiyo maana tunaweza tuka-undermine au tusione mchango wa Jeshi letu na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Spika, katika kuchangia nianze suala la ufinyu wa bajeti; ndani ya hotuba ya Waziri amezungumzia maombi ya fedha na ufinyu wa bajeti. Hilo ni jambo muhimu ambalo Serikali inatakiwa isikie na ione. Kwa sababu Jeshi linapopewa fedha ambazo hazitoshelezi ina maana haliwezi kutekeleza programu zake mbalimbali ambapo programu zote zinazowekwa kwenye bajeti huwa ni Strategic Program, programu ambazo zinaaminika kabisa zina mchango kwa Taifa hili kwa ujumla wake. Kwa hiyo, suala la bajeti ya Wizara linatakiwa liangaliwe kwa macho mawili au kwa ukaribu zaidi.
Mheshimiwa Spika, jambo la pili ni suala la madeni. Tumeona kuna madeni karibu shilingi bilioni 483. Madeni hayo ni changamoto kubwa kwa Wizara, kama una madeni mengi namna hiyo au madeni makubwa kwa kiasi hicho hata moyo wa kutaka kutekeleza programu zingine unarudi nyuma kwa sababu ukipa fedha inabidi ulipe hayo madeni kwanza. Pia tunaposema madeni, Jeshi likidaiwa maana yake tunaathiri taswira ya Jeshi, kwa sababu Jeshi ni chombo ambacho hakitakiwi kudaiwa, ni chombo ambacho kinatakiwa kiwe salama salimini ili kiweze kuaminika na kiwe na taswira inayoeleweka. Kwa hiyo, nashauri kabisa, Wizara ya fedha iangalie namna ya kulipa madeni hayo ambayo mengine tunaambiwa ya kimkataba na hata madeni ya kimkataba yanapochelewa kulipwa ina maana yanatengeza riba, ina maana madeni hayo yatakua na kukua kwa maana hiyo, Jeshi litapata changamoto kubwa.
Mheshimiwa Spika, lakini jambo la tatu ambalo Wabunge wengine wameshalizungumzia ni maeneo ya Jeshi, ni muhimu maeneo ya Jeshi yote yakapimwa. Kwa hiyo, uchukuliwe mkakati wa maksudi wa kuhakikisha maeneo ya Jeshi yanapimwa, mipaka inafahamika siyo kwa wanajeshi tu na kwa wananchi wote na vijiji vinavyozunguka maeneo hayo, hiyo itasaidia kuondoa migororo ambayo tumekuwa tunaona inashamiri na inazidi kukua kwa sababu mgogoro unapokuwa mdogo, unapoona moshi ujue moto upo ndani yake. Kwa hiyo, lazima tuangalie namna ya kuondosha migogoro hii. Wakati tunasuburi fedha za kupima haya maeneo ni muhimu sasa Jeshi au Wizara ikachukuwa hatua ya kushirikisha vijiji husika kukawa na mazungumzo ya awali kuweka mipaka ya awali, kwamba baadaye tutapima mipaka hiyo, hapo tutakuwa tumeanza kutatua migogoro hiyo.
Mheshimiwa Spika, limezungumzwa suala la mafao ya askari wastaafu wa Jeshi. Wabunge wote tunasema yaanagaliwe upya, yapitiwe na wanajeshi wetu wasijione wanyonge, wametumikia, utumishi wao umekwisha, lakini sasa wanatakiwa waenziwe kwa utumishi wao na kwa amani ambayo wamekuwa wakiisaidia nchi hii kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Spika, iko changamoto ya maakazi ya askari, tumeona wanajenga nyumba 10,000 zimejengwa 4,000 bado haijapigwa hatua ya kutosha, ni muhimu ikatafutwa mikakati mingine ya ziada kuhakikisha kwamba askari wanakuwa na makazi yanayostahili.
Mheshimiwa Spika, kuhusu bajeti ya maendeleo. Mwaka huu tunasema kwamba asilimia 40 itakwenda kwenye bajeti ya maendeleo, lakini wenzetu wa Wizara hii wanayo miradi ambayo inahitaji kusukumwa kidogo sana ili iweze kusonga mbele. Kwa mfano, kuna mradi wa Mzinga, kile Kiwanda cha Mzinga kinaweza kufanya kazi kubwa, kikatoa bidhaa kwa ajili ya Jeshi la Polisi, Magereza na kikatoa hata kuuza nchi za jirani bidhaa zinazozalishwa pale, wenyewe wanaita mazao. Sasa ni muhimu kabisa mwaka huu wa fedha, fedha zikatolewa, idara hiyo ikaweza kujitegemea na ikasaidia katika maeneo mengine. Jambo hilo likifanyika litakuwa na mchango mkubwa.
Mheshimiwa Spika, tukizungumzia suala la afya, Jeshi lina hospitali zake, lakini kwenye hotuba ya Waziri tumeona wamezungumza kwamba pesa zinazotolewa hazikidhi na Waziri amefikia hatua ya kusema kwamba afya za wanajeshi zinakuwa mashakani, Sasa unapokuwa na wanajeshi wenye afya zilizo mashakani usalama huo utapatikana vipi?
Kwa hiyo, tunashauri kabisa kwamba pesa zilizotengwa mwaka huu ziende huko na zifanye kazi hiyo, wenzetu wamekuja na mbadala, mbadala wenyewe ni kwamba wanasema kuwe na aina ya bima ya afya, jambo hilo linatakiwa lifanyiwe kazi kwa haraka ili afya za askari ziweze kukaa vizuri.
Mheshimiwa Spika, kuna vyanzo vingine vya mapato ambavyo wenzetu wamezungumza, Mheshimiwa Azzan Zungu amezungumzia na msemaji mwingine amezungumza kuhusu UN Mission. Jambo kubwa tuliloliona ni kwamba UN Mission hizi hata zikienda vifaa havitoshi, kwa hiyo lazima tuweke mtaji wa kutosha, vifaa vinunuliwe ili tuweze kunufaika na hizo UN Mission. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, upo mradi wa mawasiliano ambao mwaka jana ulitekelezeka kwa kiwango kidogo sana, mwaka huu tunashawishi kabisa pesa zote zitolewe ili mradi huo wa mawasiliano uweze kukamilika.
Mheshimiwa Spika, kuhusu JKT, Wabunge tunashauri kwamba vijana kwanza wote waende JKT wanaostahili kwenda. Tunaposema wote waende maana yake nini, maana yake bajeti iongezwe waweze kwenda. Tuna SUMA JKT itumiwe kulinda Taasisi zote za Serikali na SUMA JKT walipwe, kwa sababu tumeona kwamba yapo madeni, wanalinda hawalipwi, maana yake nini? Nashauri kabisa kwamba wale wanaodaiwa, Wizara ichukue hatua za kupeleka madai yao kwa Mlipaji Mkuu ili pesa ziweze kukatwa juu kwa juu. Kwa sababu inaonekana zikishaingia kule basi kunakuwa na kiini macho ambacho kinaendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana na mchango wangu ndiyo huo. Naunga mkono hoja.