Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nijielekeze kwenye umuhimu wa kukuza Pato la Taifa letu. Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu wa Makazi ya mwaka 2022 inatanabaisha kwamba idadi ya watu nchini ni takribani milioni 61.7 vilevile inaendelea kusema wastani wa ukuaji wa watu Tanzania kwa mwaka ni wastani wa asilimia 3.2. Nimejielekeza kwenye mpango huu pia unaelekeza kwamba uchumi wetu unakua kwa wastani wa asilimia 5.4. Kwa hiyo, ongezeko la watu lina mahusiano ya moja kwa moja na Pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, actual growth ya Pato la Taifa letu, ukuaji halisi wa uchumi wa Pato la Taifa letu siyo 5.4 ni 2.2 kwa sasa. Unawezaje kupata actual growth kwa maana ya wastani halisi? Unachukua wastani wa Pato la Taifa ambalo ni 5.4 unatoa wastani wa ukuaji wa watu ambao ni 3.2. Kwa hiyo wastani halisi kwa sasa nchini wa ukuaji wa Pato la Taifa ni asilimia 2.2 ambacho kile kimebaki baada ya ku-minus and I stand to be corrected.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa najiribu kueleza tunawezaje kutoka hapa? Tuna kila sababu ya kuongeza bidii kwenye vichochea Pato la Taifa, walau tufike kwenye asilimia nane au kumi. Nilikuwa najaribu kuwaza kwa sauti kama sasa hivi wastani wa ukuaji wa watu ni asilimia 3.2; je miaka hamsini ijayo Tanzania itakua ya aina gani? Tumejipangaje kama Taifa kwa idadi ya vizazi hivyo vijavyo? Bado kuna changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nijielekeze kwenye maeneo ambayo tukiwekeza tunaweza kufikia asilimia nane mpaka kumi ya ukuaji wa Pato letu la Taifa. Jambo la kwanza ni utafiti. Utafiti kwenye kilimo, utafiti kwenye viwanda, utafiti kwenye madini, utafiti kwenye masoko na biashara, hali kadhalika na utafiti kwenye mazao ya mifugo ya samaki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa najiuliza pia maswali kuna Chuo kama SUA hivi hatuwezi kubadilisha mfumo wa elimu tukaondokana na tafiti au academic research kwamba ili mtu apate Degree lazima awe amefanya thesis amefanya research fulani lakini ile inaenda kukaa kwenye kabati tu. Sasa hatuwezi kuwekeza kwenye Vyuo Vikuuu tukapata tafiti ambazo ni practical mbona Madaktari wanaweza? Kwa Madaktari wanafanya, Daktari Bingwa wa Moyo anakwenda kufanya tafiti lakini ni practical kwa nini watu wa kilimo wasifanye? Kwamba zao fulani linaweza linaweza likastawi sehemu fulani, ardhi fulani na ikiwezekana na bahati mbaya nilikuwa naona kengele ngoja niende haraka haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeona jitihada za Mheshimiwa Rais, ameenda China tumepata Soko la Parachichi sasa najiuliza maswali tumejiandaaje kukata hiyo market ya parachichi? Kwenye suala la kilimo, tunaona jitihada za sekta ya kilimo lakini tunawekeza nguvu hizi kwenye biashara ya kilimo kimkakati? Kwa mfano, Bonde la Mto Kilombero kuna Bonde la Hifadhi lakini kuna Bonde linalofaa kwa kilimo. Je, tumejifikiriaje kuweka Miradi ya Umwagiliaji? Kwenye Bonde la Mto Kilombero? Tuna mikakati gani ya kuwekeza eneo hilo? Sasa hayo ni mambo ya kuangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, nilikuwa nashanga sana leo hii korosho inalimwa Dodoma, Mwanza kila sehemu korosho tu jamani hii korosho inatija gani kwa nchi hii? Tuache Mtwara, walime korosho na sisi watu Mlimba, tuwe na zao maalum la mpunga tuzalishe mchele, lakini navyozungumzia viwanda, nazungumzia viwanda kwa maana siyo vile viwanda vya tunasema viwanda vikubwa nazungunzia agro-base industry ni viwanda vinavyochakata malighafi kuwa bidhaa hiyo ndiyo hoja yangu ya msingi. Tukiwekeza kwenye viwanda maana yake vijana watapata ajira lakini pia tutaongeza Pato la Kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naangalia Urari wa biashara nchini kwenye East Africa tunafanya vizuri na SADC Countries, lakini huko Duniani tuko mbali mno kwenye urari wa biashara ndani ya nchi yetu. Kwa hiyo, tunayo kazi ya kufanya ili tuweze ku-capture hiyo market. Pia kuna urari wa malipo tunasema balance of payment bado tunakwenda kwenye hasi unfavorable balance of payment kama Taifa. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri yupo hapa uchumi, Waziri wa Fedha atusaidie kwenye eneo hili, mipango hii tunayosema sisi basi ichukuliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende mwisho kwenye sekta ya ardhi. Nilikuwa nafuatilia sensa ya watu na makazi idadi ya majengo ni 13,907,951. Idadi kwa maana ya wakati kuna mapitio ya bajeti idadi ya viwanja vilivyopimwa ni Millioni Sita, idadi ya Hati Miliki nchini ni Milioni Mbili. Kwa hiyo kama idadi ya majengo yako Milioni 13 kuna idadi ya watu wenye majengo ambao hawajapimiwa zaidi ya Milioni Saba. Sasa hiyo ni sekta ya sehemu nyingine, pia kuna idadi ukitoa Milioni Mbili watu wenye Hati Miliki maana yake kuna idadi ya Million 11 ya Watanzania hawalipi kodi ya ardhi. Sasa hili eneo ni fursa kwetu nampongeza sana Waziri wa Ardhi anatatua migogoro kwa kutumia hii kliniki, nimeona juzi pale Kibaigwa. Mama anafanya kazi nzuri, kama kutatua migogoro kwa kutumia kliniki na nikuombe Mheshimiwa Waziri, kliniki hii ifanyike na kule Morogoro, isifanyike tu Dodoma. Kliniki endelevu tembezi inasaidia kutatua migogoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto tuliyonayo ukiangalia ardhi, nikuombe dakika moja tu nimalizie, samahani ahsante. Tusitazame sekta ya ardhi kama migogoro, migogoro ni matokeo ya kutokufanya vizuri kwa sekta. Kwa hiyo, tukijielekeza kwenye mipango bora ya matumizi ya ardhi hakika Taifa letu litaenda kutatua migogoro yote ya ardhi. Baada ya kusema hayo, ahsante sana na Mungu akubariki sana. (Makofi)