Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

Hon. Atupele Fredy Mwakibete

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busokelo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia katika mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa. Awali ya yote nianze kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametufanya tuwepo hapa. Pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi nzuri anayowafanyia Watanzania wote. Tatu, nikupongeze wewe Mheshimiwa Spika kwa namna ambavyo unaongoza Bunge hili kwa viwango hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamejadiliwa na Waheshimiwa Wabunge, nami niungane nao kwanza kwa kukubali mapendekezo ambayo wamependekeza katika Mpango huu hususani katika Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mengi yamezungumzwa, suala la Bandari, Reli, TAZARA, Meli, Barabara na Miundombinu yote yamezungumzwa. Aidha, nianze kwanza na Bandari ya Tanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Tanga kwa historia ilianzishwa tangu mwaka 1888 lakini mwaka 1891 ndipo ilipokamilika. Kulikuwa kuna changamoto za uendeshaji na ujenzi wa Bandari hii, ndipo Serikali ilipoamua kwamba tuiboreshe Bandari hii ya Tanga. Ilifanyika katika awamu mbili na awamu ya kwanza, ilikuwa ni kufanya dragging kutoka kwenye kina kirefu umbali wa kilometa 1.7 mpaka kwenye gati. Awamu ya pili, ilikuwa ni kwa ajili ya kujenga gati mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe ufafanuzi hapa kwa sababu kumekuwa na sintofahamu ya kuelewa kwamba kilometa 1.7 ya dragging kwa maana ya kuchimba kile kina iko katika awamu gani katika miradi hii yote miwili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza, ilihusisha ujenzi huo na kuchimba kina kutoka mita tatu mpaka mita 13 ili meli kubwa ziweze kupita na kufika kwenye gati ama Bandari yenyewe ya Tanga. Kwa bahati nzuri mradi huu ulianza mwaka 2019 na umekamilika tayari kwa 100% na thamani ya mradi huu ilikuwa ni bilioni 172.3.

Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya pili, ilikuwa ni kwa ajili ya kujenga gati mbili na hizo gati ni awamu ambayo imeanza mwaka Septemba, 2020 na thamani ya mradi kwa awamu ya pili ilikuwa ni kiasi cha silingi bilioni 256.8. Kwa awamu hii mradi huu una asilimia 79 maana yake Mkandarasi bado yupo site. Nimeona nitoe ufafanuzi huu ili ieleweke kwa Watanzania wote na Bunge kwa sababu kulikuwa na mkanganyiko wa taarifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka nilitolee ufafanuzi ni suala la Viwanja vya Ndege Nchini. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia kwamba ndege hazitui usiku, ni kweli Ndege hazitui kwa sababu viwanja vichache ndio vyenye taa. Tuna Kiwanja cha Mwalimu Nyerere kina taa, Songwe, Zanzibar na Mwanza. Katika mpango huu ambao sasa hivi Serikali imewekeza, tunakwenda kujenga viwanja vya ndege visivyopungua nane na tunakwenda kuweka na taa za kuongozea ndege usiku na mchana kikiwepo kiwanja chetu cha hapa Dodoma. Waheshimiwa Wabunge ninyi ni mashahidi kwamba kiwanja chetu hiki hakina taa na ndio maana ndege haiwezi kutua usiku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali tulilazimika kuendelea kukijenga kiwanja hiki na kukiboresha kutokana na kwamba Kiwanja kipya cha Ndege cha Msalato ambacho hivi karibuni Mheshimiwa Rais ameshuhudia utiaji saini wa zaidi ya shilingi bilioni 360 kitakamilika mpaka 2024/2025. Tukaona kwa sababu Serikali tayari imekwishahamia Dodoma, kulikuwa kuna hoja kwamba kwa nini hatukuona kwamba kuna umuhimu wa kukiacha vile vile tusubiri hiki Kiwanja cha Msalato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaambie Waheshimiwa Wabunge kwamba tumeona umuhimu wa kuboresha kiwanja hiki kwa sababu hapa ndipo Makao Makuu ya nchi, hapa ndio Makao Makuu ya Serikali na hapa ndio Makao Makuu ya Chama Tawala. Tukiwa na viwanja viwili katika mataifa mengine ndivyo wanavyofanya kwa maana ya kwamba hata kukiwa na emergence landing, inakuwa ni rahisi, inaweza kuwa kukawa na changamoto Kiwanja cha Msalato ndege ikatua hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanja huu tayari tumekwishasaini zaidi ya Sh.6,438,450,107/= kwa ajili ya ujenzi wa taa na Mkandarasi ataanza kazi mara moja ambaye anaitwa Jess Espaňiola ambaye ataanza wakati wowote katika Kiwanja chetu cha Dodoma. Vile vile kuna viwanja vingine ambavyo vinaendelea na ujenzi kuna Kiwanja cha Songwe ambacho karibia kina kamilika, Kiwanja cha Songea, Mtwara, Iringa, Manyara ambacho pia tutaanza, kuna Kiwanja cha Kigoma, Tabora, Shinyanga na maeneo mengine mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo ligine ambalo limezungumzwa sana hapa ni suala la ATCL kwamba ndege hazitoshi. Ni kweli hazitoshi, lakini katika Mpango huu Mheshimiwa Rais ametuagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kununua ndege tano mpya ikiwemo ndege ya mizigo ambayo itaingia nchini mwakani mwezi Machi.

Kwa hiyo tutakuwa na ndege 16 zaidi, kwa hiyo hata kwa hizi changamoto za route ambazo zinatokea sasa hivi kutokana na kwamba ndege ni chache, ikitokea tu hitilafu kidogo maana yake hiyo route inaharibu route nzima. Sasa zikiingia Ndege hizi tano katika Mpango huu ambao Waheshimiwa Wabunge wamependekeza nina hakika suala la usafiri wa anga litakwenda kuimarika zaidi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu ya muda naunga mkono hoja hii ya Mpango na yale yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wamesema hapa tunakwenda kuyaweka na hasa ambayo hayakuwepo. (Makofi)