Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Ngorongoro
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa nafasi na mimi kuchangia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, kwanza niwapongeze Serikali kwa kazi nzuri wanayofanya. Kule Ngorongoro kazi kubwa imefanywa sana na Serikali kwa kutupa miradi mikubwa ya maji, hasa mradi wa vijiji Nane ambao unaitwa ni mradi wa Mageri. Nimpongeze na Waziri wa Maji kwamba ameweza kufika na kufuatilia kwa kila hatua, amefika zaidi ya mara tatu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakuwa sijawatendea wananchi haki nisipozungumzia suala la bei ya mafuta na vyakula. Kwa sasa hivi kule nje maisha ya wananchi ni magumu sana, kule Loliondo sasa hivi watu wananunua mafuta ya dumu la lita tano kwa Shilingi 40,000, sukari imeenda Shilingi 3,500 lakini tunakaa huku tunajifungia tunasema ni kwa sababu ya vita vya Ukraine, kuna tatizo kule nje.
Mheshimiwa Spika, ninaiomba Serikali na ninaishauri Serikali ni wakati muafaka sasa Serikali kupita kwa wazalishaji wote na kuangalia kwamba bei ya vyakula na bei ya mafuta je, ni uhalisia au ni artificial? Ni muhimu sana Serikali kuliangalia hili. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuna suala ambalo tunalizungumzia la barabara, Wilaya ya Ngorongoro haijaunganishwa na Mkoa wa Arusha haijaunganisha na nchi ya Jirani. Tunaishukuru Serikali kwamba imetupa barabara ya lami ya Kilomita 50 kutoka Loliondo mpaka Sale, lakini bado tunahitaji barabara ya lami kutoka Sale mpaka Mto wa Mbu au Kigongoni. Kwa hiyo, ninaiomba Serikali iweze kuiangalia Wilaya ya Ngorongoro kwa sababu maisha ya wananchi yanakuwa magumu kwa sababu hatujaunganishwa na Mkoa wetu wa Arusha na ndiyo maana hata bei ya vyakula inapanda kwa wakati.
Mheshimiwa Spika, kuna suala ambalo Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya kule Ngorongoro, ninashukuru kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu amekubali kupokea maoni ya wananchi kuhusiana na eneo la pori tengefu na Ngorongoro. Hiyo ni nia njema ya Serikali na nimshukru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu amekuwa tayari wakati wote tukizungumza na yupo tayari kuwapokea watu wangu, aliwapokea Maleigwanani, akazungumza nao na tukakubaliana kwamba tutamletea maoni ya wananchi. Kwa hiyo nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa hilo. Hiyo ni nia njema ambayo itatusaidia kutatua matatizo yaliyopo Ngorongoro. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kulielezea Bunge lako na kuelezea masikitiko yangu kwa mbaadhi ya mambo yanayoendelea sasa hivi. Wananchi wa Ngorongoro hawana shida na mtu yeyote ambaye ana hiari ya kutoka Ngorongoro naomba niweke wazi hilo, hakuna mtu mwenye shida na mtu yeyote pale. Wale wote waliojiandikisha kwa ajili ya kuondoka kama Serikali ilivyosema hakuna mtu ambaye anawazuia, ninawashangaa waliojitokeza kusema kwamba wanaomba ulinzi wasipewe ulinzi hakuna shida wataondoka kwa amani.
Mheshimiwa Spika, kuna tatizo moja kwa sasa hivi wale wanaobaki ambao watakuwepo Ngorongoro inaonekana kwamba Serikali inawawekea vikwazo vya kimaendeleo, kuna fedha ambazo zilipelekwa kwa ajili ya vituo vya afya, kwa ajili ya maji, kwa ajili ya madarasa, inaonekana sasa Serikali inahamisha zile fedha kwenda Halmashauri ya Handeni.
Mheshimiwa Spika, Walimu wameandikiwa vituo vya afya wameandikiwa kwamba hizo fedha zihamishwe ziende Handeni. Ninachojiuliza sasa Serikali imeona watu wa muhimu pale Ngorongoro ni wale wanaohiari kuondoka? Wale wanaobaki maisha yao yatakuwaje kama tunawanyima vituo vya afya, kama tunawanyima maji, kama tunawanyima shule; Je, wale wananchi watakuwa sehemu ya Watanzania?
Mheshimiwa Spika, suala lingine kwenye zoezi ambalo linaendelea chini ya ofisi ya Mheshimiwa Nape la anuani ya makazi, kule Ngorongoro hakuna zoezi hilo, Tarafa ya Ngorongoro hakuna zoezi hilo kwanini tusiwahesabu wananchi tukaendelea na program zingine?
SPIKA: Mheshimiwa Ole Shangai kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Innocent Bashungwa.
T A A R I F A
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa mchango wake mzuri, lakini ninapenda kumuondoa wasiwasi, wananchi wote ni wa kwetu kule Handeni tunapeleka miradi lakini hata Tarafa ya Ngorongoro kazi inaendelea. Kwa hiyo asubiri bajeti yangu tutamuonesha ni namna gani ambavyo tumejipanda kuhakiksiha hata Tarafa ya Ngorongoro miradi inaenda kama kawaida. Ahsante sana. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Ole Shangai unaipokea taarifa hiyo?
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, hiyo taarifa siIpokei.
Mheshimiwa Spika, kwa nini sipokei taarifa hiyo, wananchi gani hawa ambao unawasubirisha bajeti nyingine, wakati fedha ambazo zipo kwenye akaunti unaondoa kupeleka Handeni. Leo fedha Shilingi Milioni 500 ambazo zilikuwa kituo cha afya Nainokanoka mnahamisha kupeleka Handeni, fedha Shilingi Milioni 600 kwa ajili ya maji Kata za Alaitolei, Masamburai, Oloirobi na maeneo mengine mnahamisha kwa ajili ya kuwawekea wananchi vikwazo vya kimaendeleo.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, taarifa!
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, naomba ulinde muda wangu.
SPIKA: Mheshimiwa Ole Shangai kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Maji, Mheshimiwa Aweso.
T A A R I F A
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ninampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya katika Jimbo lake, lakini nataka nimhakikishie kwamba hakuna maelekezo yoyote ambayo Wizara ya Maji tumepewa tusiendelee na shughuli za maji pale.
Mheshimiwa Spika, tuna mitambo ambayo ipo inatekeleza uchimbaji pale katika Jimbo lake, nami kama Waziri wa Maji nimefika. Nataka nimhakikishie na shughuli zinaendelea na Mheshimiwa Waziri Mkuu ametupa maelekezo mahsusi ya kuhakikisha visima vile vinakamilika kwa wakati. Ahsante sana.
SPIKA: Mheshimiwa Ole Shangai unaipokea taarifa hiyo?
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Taarifa hiyo naipokea lakini anachozungumza Mheshimiwa Waziri yeye anazungumzia miradi ya maji inayoendelea Tarafa ya Sale na Loliondo siyo Tarafa ya Ngorongoro, hakuna mrdi wowote wa maji unaoendelea Tarafa ya Ngorongoro hakuna! Sasa hivi miradi yote imesitishwa na Serikali kwa sababu ya kuwawekea wananchi vikwazo vya kimaendeleo.
Mheshimiwa Spika, kwa nini tunawawekea vikwazo? Wananchi hawa wamekuwa pale kwa miaka 60, is it a nightmare tukawaondoa kwa siku moja? Kwa mfano, hospitali ya Enduleni ilikuwa inapata shilingi milioni 500 kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa ajili ya kuwatibu wananchi imeondolewa pia.
Kwa hiyo, watoto wadogo akinamama wanakufa kwa kukosa huduma!
Mheshimiwa Spika, sasa Serikali gani hii sasa ambayo inawawekea wananchi vikwazo? Kama tunataka kupunguza watuNgorongoro siyo kwa namna hiyo ya kuwawekea vikwazo vya kimaendeleo. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Ole Shangai kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya.
T A A R I F A
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze mwenzangu kwa mchango wake mzuri, lakini nimhakikishie tu na nimuondoe wasiwasi kwamba hata jana Shilingi Milioni 321 zimetengwa kupitia Global Fund kuelekea kwenye eneo analolitaja la Enduleni. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi kimsingi inawezekana source za taarifa zimemtisha lakini nikuombe tu kwamba hilo jambo litasimamiwa na uamini ambacho Waziri wa TAMISEMI amekisema na wengine wanachokuambia, tuanze kushirikiana kuanzia sasa tuone tunaenda Pamoja. Kama ambavyo Waziri Mkuu amekuwa akishirikiana na ninyi basi na hayo mengine tushirikiane kwa pamoja tutakwenda vizuri.
SPIKA: Mheshimiwa Ole Shangai unapokea taarifa hiyo?
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa hiyo kwa masharti, nendeni kwa wananchi mkawaambie mnachosema hapa. Kwa sababu, kinachosemekana hapa ni ili tu tumalize hapa, lakini kinachoendelea Ngorongoro kama walivyoshauri Wabunge wakati mwingine ni bora Bunge hili likajiridhisha kwamba yanayoendelea Ngorongoro siyo haki kwa wananchi wale!
Mheshimiwa Spika, wakinamama mpaka wasafiri Karatu wakapate huduma za afya sasa hivi, vituo havina dawa wananchi tunawawekea vikwazo vya kimaendeleo kwa ajili gani?
Mheshimiwa Spika, leo ukijaribu kwenda pale kupita kwenye geti la Ngorongoro wameweka vikwazo kibao, wananchi ili uingie ni lazima upekuliwe na wengine wanarudishwa hawajui pa kwenda kulala Karatu, unakuta ni mgonjwa alikuja Karatu anazuiliwa getini.
Mheshimiwa Spika, nadhani kwa Serikali inayojali utu, kwa Serikali inaowajali wananchi wake, ni muhimu sana tusifanye zoezi hili la watu kuhiari kutoka Ngorongoro kama ndiyo njia ya kuwaumiza wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro wanaobaki. (Makofi)
SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, hii itakuwa ni taarifa ya mwisho kwa mchangiaji Ole Shangai, Mheshimiwa Kundo. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mheshimiwa Mbunge katika yale ambayo anatamani wananchi wake wafanyiwe. Bahati nzuri tulifika katika Jimbo lake na Mheshimiwa Waziri Mkuu alitoa maelekezo kwa sababu ni Serikali kuhakikisha kwamba wananchi wake wanasogezewa huduma za msingi na kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, upande wa mawasiliano tunapeleka huduma ya mawasiliano kujenga minara zaidi ya 24 ndani ya Jimbo la Ngorongoro.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge awe na amani kabisa kwamba ndani ya Jimbo lake la Ngorongoro tunakwenda kufanya kazi nzuri sana, asiwe na wasiwasi kuhusu anuani ya makazi na Postcode. Nashukuru. (Makofi)
SPIKA: Mheshimiwa Ole Shangai unaipokea taarifa hiyo?
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Spika, sasa taarifa iliyotolewa na Naibu Waziri, Ngorongoro kuna Tarafa tatu, Tarafa ya Loliondo, Tarafa ya Sale na Tarafa ya Ngorongoro ambayo ndiyo naizungumzia. Kama Naibu Waziri ana uhakika kwamba anazungumzia Tarafa ya Ngorongoro naomba list ya Kata ambazo utapeleka minara hiyo, ziwe kwenye Tarafa ya Ngorongoro na siyo Tarafa ya Sale na Loliondo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala ambalo lipo liliwasilishwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu kwamba, sasa hivi tunaanzisha mashamba darasa ya kulima nyasi kwa ajili ya mifugo. Wakasema kuna moja lipo Loliondo, mimi ninaamini kwamba Serikali inatakiwa kutatua matatizo ya wananchi wake na tunatakiwa kutatua matatizo kwa muda mfupi na muda mrefu.
Mheshimiwa Spika, naamini kwamba kwa eneo letu la Loliondo, wananchi wataleta maoni yao chochote kile ambacho kinatakiwa kufanyika tuache mpaka maoni ya wananchi yafike kwanza, tuone wananchi wanavyofikiria kuhusiana na eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, baada ya hapo mimi nashukuru lakini wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro wasiwekewe vikwazo vya kimaendeleo. Nashukuru sana (Makofi)