Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, napenda kuwapongeza kwa maandalizi ya hotuba nzuri ambayo imegusa maeneo mengi ya maisha ya wananchi. Nina ushauri/mchango katika baadhi ya masuala kama ifuatavyo: -

Kwanza, ujuzi kazi ukurasa wa 62-63; kwa mujibu wa taarifa za Wizara ya Elimu, katika nchi yetu asilimia 79.9 ya nguvu kazi yetu ni low skilled labour ambao majority ni wale waliomaliza darasa la saba. Asilimia 16.6 ni middle skilled labour wakati asilimia 3.6 ni high skilled.

Hata hivyo kazi kubwa ya shughuli za uzalishaji zinafanywa na hawa asilimia 79.9 ambao tukiwapa ujuzi kazi kama ambavyo inafanyika kupitia ile programu ya kukuza ujuzi tutakuwa tumewasaidia na tumelisaidia Taifa. Nafahamu juu ya ile national skills development through green house ambayo inajielekeza zaidi kwenye ujuzi kazi wa kilimo.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu tupanue wigo wa mafunzo na hapa nawasilisha ombi mahususi kwa ajili ya mafunzo ya ujuzi kazi kwa vijana wa maeneo ya Kilolo, Mafinga, Mufindi na Njombe ambako uchumi wetu unategemea sana mazao ya misitu. Vijana wetu katika maeneo hayo wakipata mafunzo ya ujuzi kazi katika suala la kuongeza thamani katika mazao ya misitu wanaweza kupata ajira rasmi katika viwanda na hivyo wakawa na mchango kupitia PAYE/SDL, lakini pia wanaweza kujiajiri wakajijengea uwezo hata wa kuajiri wenzao.

Mheshimiwa Spika, mafunzo haya yanaweza kufanywa kwa kushirikiana na TFS na asasi za kijamii kwa maana ya NGOs zinazojishughulisha na masuala ya misitu kama vile Panda Miti Kibiashara na Forestry Development Trust of Tanzania. Aidha, kupitia mifuko mbalimbali ya uwezeshaji kwa vijana, tunaweza kuwasaidia vijana hao kwa kuwapa mikopo ya vitendea kazi ili kusaidia ushiriki wao katika uchumi wa mazao ya misitu kwa kuongeza thamani. Kwa mfano hivi sasa zaidi ya asilimia 60 ya mti unapotea kama waste, lakini wakipata ujuzi kazi na vitendea kazi tunaweza kuhakikisha kuwa recovery rate kwa kila mti inapanda kutoka asilimia 40 ya sasa hadi asilimia 90 kwa sababu katika mti ukiacha mbao kuna bidhaa nyingine kama MDF, Plywood na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, nimeona benki za CRDB na NMB zimetenga fedha kwa ajili ya kilimo kwa mikopo ya riba kati ya asilimia tisa hadi kumi mikopo ambayo tungeweza pia kuelekeza katika sekta ya mazao ya misitu.

Pili ni kuhusu kushirikisha JKT katika uzalishaji wa bidhaa muhimu kama mafuta ya kula na sukari. Wakati wa usalama ni vema vyombo vyetu vikawezeshwa ili kushiriki katika shughuli za uzalishaji. Ninaamini mabilioni tunayotumia kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi tunaweza kuepuka na kujitosheleza kwa chakula ikiwa tu tutawezesha JKT na Magereza kuzalisha alizeti na ufuta kwa ajili ya viwanda vya ndani. Tukiwa wakweli wa nafsi ni aibu kama Taifa kushindwa kujitosheleza kwa mafuta ya kula wakati ardhi yenye rutaba tunayo bali ni suala la kuamua tu, tunahitaji political will katika suala hili, kama ambavyo tumewashirikisha JKT katika miradi ya ujenzi na tukiwakabidhi jukumu hili ndani ya muda mfupi tutakuwa tumejikwamua na tunaweza kuuza nje na pia kukabiliana na kilio cha kupanda bei kiasi ambacho we have less control na yawezekana ni mchezo wa waagizaji. Naomba kuwasilisha.

Mheshimiwa Spika, pamoja na kusimamia masuala ya kazi sehemu za kazi kama vile masuala ya OSHA na kadhalika, ninaamini Ofisi ya Waziri ni kichocheo cha uongezekaji wa ajira.

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni TANESCO wanasema wataanza kuagiza nguzo za umeme kutoka nje ya nchi, suala hili litaathiri sana ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja. Sekta ya mazao ya misitu ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuwa mgeni rasmi kwenye Kongamano la Mazao ya Misitu mwezi Novemba 2021 ni sekta ambayo imeajiri watu wengi vijana kwa wanawake.

Kwa hiyo, hatua ya kuamua kuagiza nguzo za umeme nje ya nchi itaathiri ajira za vijana na wanawake wa mikoa ya Njombe na Iringa na maeneo mengine ya nchi, kuna mnyororo mkubwa wa ajira na kipato, kuna wenye mashamba ya nguzo ambao ni wananchi lakini pia kuna Shamba la Serikali la Sao Hill ambalo ndio muuzaji mkubwa wa nguzo. Suala hili litaathiri kipato cha wafuatao; wenye mashamba ambao ni wananchi, Wakala wa Misitu (TFS) ambao wanamiliki Shamba la Serikali la Sao Hill, wakataji na wanaomenya nguzo, wanaopakia kwenye malori madogo, wanaosafirisha nguzo kutoka mashambani kufikisha kwa wenye viwanda, walioajiriwa na wenye viwanda, Halmashauri kwa sababu asilimia 30 ya mapato yetu ya own source ni kutokana na nguzo na pia Serikali kwa sababu katika shughuli za nguzo kuna sekta ya usafirishaji ambapo Serikali inapata fedha kupitia fuel levy.

Mheshimiwa Spika, ushauri; hoja za TANESCO/Serikali kwamba wazalishaji hawana uwezo sio sahihi kwa sababu kutoka viwanda vitano sasa kuna viwanda 18 ambapo uzalishaji kwa mwaka ni mpaka nguzo milioni tatu wakati uhitaji kwa mwaka ni wastani wa nguzo milioni moja, maana yake kuna ziada ya nguzo milioni mbili.

Suala la ubora, sio kweli kwa sababu kuna mfumo wa kupima ubora wa kwanza ukiwa ni moisture content ambapo haipaswi izidi asilimia 25 lakini pia suala la treatment, viwanda vina mitambo ya kisasa ambayo hata Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembela moja ya viwanda hivyo cha Sao Hill Industries.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu hiyo na kama kweli tuko serious na uchumi wa viwanda, nashauri Serikali iondokane na wazo la kuagiza nje ya nchi nguzo za umeme, nimetaja hapo juu mnyororo wa mapato ya sekta hii, kama Taifa kuanza kuagiza nguzo nje sio tu tunarudi nyuma bali pia tunaathiri suala zima la kazi na ajira. Katika hotuba ya Waziri Mkuu mmezungumzia ujuzi kazi kama kuna mapungufu ndio maana nmeshauri kuwa pamoja na vitalu shamba kwa maana ya ujuzi kazi katika kilimo, Serikali itusaidie kuwa na programu maalum ya mafunzo ya ujuzi kazi kwa ajili ya sekta ya mazao ya misitu. Naomba kuwasilisha.