Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. January Yusuf Makamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bumbuli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa fursa hii uliyonipa. Nami niungane na wenzangu kuwashukuru sana Wabunge wote waliochangia hoja hii na waliochangia kwenye eneo linalohusu sekta ya nishati.

Mheshimiwa Spika, yaliyochangiwa ni mengi, muda uliopo wa kuyajibu yote hautoshi. Kwa hiyo, tutayajibu kwa maandishi namba moja, namba mbili tutayajibu wakati wa bajeti yetu ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwa kifupi tu niseme kwa baadhi ya mambo hasa ndugu zetu wa Mikoa ya Iringa na Njombe kwenye masuala ya nguzo nataka niwahakikishie kwamba nitaenda wiki inayokuja tutakaa, tutayamaliza, tutaelewana kabisa bila wasiwasi wowote na mazao yao yatanufaika na ununuzi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nijielekeze kwenye mambo mawili hasa bei ya mafuta. Kwenye sekta ya mafuta kwa ujumla kuna masuala mawili, kuna bei na upatikanaji. Suala la bei limeongelewa kwa kirefu sana ikiwemo na Mawaziri mbalimbali, sababu na mwenendo wa bei ya mafuta umeongelewa.

Mheshimiwa Spika, mwenendo wa bei ya mafuta katika miezi 16 iliyopita umekuwa ni wa kupanda na umepanda katika nchi zinazozalisha mafuta na nchi zinazoagiza mafuta vilevile. Nchi ya kwanza katika uzalishaji wa mafuta duniani ni Marekani na kwenyewe hata huko bei imepanda. Kwa hiyo, mwenendo ni wa kupanda tofauti ni kwa kiwango na kasi, lakini tofauti pia ni je, hatua zinachukuliwa?

Mheshimiwa S[ika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha juzi aliongelea kuhusu hatua za kikodi kwenye jambo hilo. Mimi nitaongelea hatua za muda wa kati na mrefu katika kuhakikisha kwamba tunahimili katika kipindi kirefu na cha kati bei kubwa ya mafuta.

Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu tumekuwa na ndoto ya kuwa na hifadhi ya kitaifa ya kimkakati ya mafuta. Hatimae mwaka huu ndoto hiyo itatimia, tunaandika kanuni za kuiwezesha kuwepo vilevile tumepata washirika katika uwekezaji wa miundombinu ya ushushaji na uhifadhi wa mafuta ili kuwezesha hifadhi hiyo kufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, ndani ya Serikali tunazungumza kuhusu kuanzisha Mfuko wa Kuhimii Ukali wa Bei za Mafuta ambao ni Fuel Price Stabilization Fund ambayo katika siku zijazo itatusaidia kutuokea katika nyakati kama hizi.

Mheshimiwa Spika, vilevile tunaendelea na mazungumzo na wauzaji na wazalishaji mafuta hasa nchi rafiki ambao tuliyaanza tangu mwezi Oktoba mwaka jana ili tuone katika kipindi hiki kama tunaweza kupata nafuu ya kununua mafuta huko moja kwa moja. Kwa hiyo, kuhusu masuala mengine nje ya kikodi Wizara yetu inayafanyia kazi karibu kila siku.

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa suala la mfumo wa ununuzi wa mafuta kwa pamoja hapa mchango umetolewa, bulk procurement system, bahati nzuri mfumo huu ulikuja kutokana na mapendekezo na maelekezo ya Bunge mwaka 2011 na mimi nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini wakati huo na Bunge kwa kauli moja likaishauri Serikali kuanzisha mfumo huo. Mfumo huo ukaanza na umekuwepo kwa kipindi cha miaka 10. Sasa mfumo huu umewekwa na watu, unaendeshwa na watu. Tumepokea ushauri mzuri sana wa Waheshimiwa Wabunge kuhusu kuuboresha mfumo huu. Nasi tupo tayari tumepokea ushauri huo na kama kuna taarifa zozote zinazohusu udhaifu katika mfumo huo na namna ya kuchukua hatua pale kwenye mapungufu basi tuko tayari wakati wote kupokea na kuyafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, mfumo huu siyo Msahafu siyo Quran siyo Biblia unaweza kubadilishwa wakati wowote ili kutusaidia pale ambapo tunadhani utakuwa na manufaa makubwa kwa nchi. Kikubwa tu ni kuwa na mfumo ambao utatuhakikishia uhakika wa kupatikana kwa mafuta lakini na bei ambayo inahimilika.

Mheshimiwa Spika, wapo Waheshimiwa Wabunge wamesema kwamba wanao uwezo wa kuisaidia nchi kupata mafuta ya bei nafuu, kwamba yako baharini huko na meli, sisi tunasema mtu yeyote, pahala popote, Mtanzania yyyote mwenye taarifa au uwezo wa kuisaidia nchi kuleta mafuta ya bei nafuu karibu sana ofisini hata leo ili tuzungumze hilo jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kung’ang’ania kitu kumbe kuna kitu kingine kitatusaidia Zaidi, nchi hii hi yetu wote hatuna shaka yoyote. Kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge njoo ofisini, kikubwa tu ni kwamba hizo meli zilizopo zituhakikishie kwamba mafuta hayo yataingia consistence kwa wakati wote kuhakikisha kwamba supply ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni upatikana wa mafuta. Ni muhimu…

SPIKA: Sekunde 30.

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, nashukuru.

Mheshimiwa Spika, katika janga kubwa linaloweza kutokea ni kukosekana mafuta. Bei ni jambo tunaweza tukalizungumza lakini kukosekana mafuta kwenye vituo, kuwepo na foleni, kuwepo na vigaloni kwenye majumba yetu ni hatari kubwa zaidi. Nataka niwahakikishie Watanzania kwamba kwa nchi yetu ukilinganisha na majirani zetu mafuta yakutosha yapo juu ya kiwango cha kanuni tulizoweka ya siku 15. Kwa hiyo, mafuta yapo na Serikali itahakikisha kwamba yanaendelea kuwepo ili uchumi usisimame. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami naunga mkono hoja. Nakushukuru sana.